Na
Saidi Mkabakuli, Kyela
Kufuatia
adha ya usafiri wa majini inayowakabili wakazi waishio katika fukwe za Ziwa
Nyasa, Mamlaka ya Bandari Tanzania kupitia kituo chake cha Kyela ipo mbioni
kujenga meli ya abiria na mizigo ili kuwahudumia wakazi hao.
Hayo
yaliwekwa bayana na Mkuu wa Bandari ya Kyela, Bw. Percival Ntetema wakati timu
wakaguzi wa miradi ya maendeleo kutoka Ofisi ya Tume ya Mipango ilipotembelea
na kukagua bandari za Itungi na Kiwira zilizopo wilaya ya Kyela, mkoani Mbeya.
Bw.
Ntetema alisema kuwa Mamlaka imeshakamilisha mchakato wa manunuzi na tayari imempata
mkandarasi M/S Songoro Marine Transport Ltd kwa ajili ya ujenzi wa meli yenye
uwezo wa kubeba jumla ya tani 200 za mizigo na abiria 200.
“Mamlaka
ipo kwenye hatua za mwisho za kuandaa mkataba unaotarajiwa kutiwa saini mwezi
ujao na kazi itaanza mwanzoni mwa mwaka
ujao,” alisema.
Bw.
Ntetema aliongeza kuwa mpaka sasa Bandari ya Kyela imeshaanza maandalizi ya
kuvuta umeme uliofadhiliwa na Wakala wa Umeme Vijijini pamoja na kuaanza kwa
kujenga matishari mawili ili yaweze kurahisisha utoaji wa huduma mara meli hiyo
itakapoanza kazi mwishoni mwa mwaka ujao.
Akizungumza
wakati wa ziara hiyo, kiongozi wa timu ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo kutoka
Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango, Bibi Florence Mwanri aliupongeza uongozi wa
Mamlaka kwa hatua yake hiyo kwani itaongeza tija ya shughuli za kiuchumi katika
kanda hiyo ya Ziwa Nyasa.
“Ninaupongeza
uongozi wa Mamlaka ya Bandari kwa kuanza mchakato huu utakaofungulia fursa za kiuchumi
na maendeleo kwenye ukanda huu, hivyo kuunga mkono jitihada za serikali za
kupunguza vikwazo mbalimbali vinavorudisha kasi ya kusaka kupunguza umaskini
nchini,” alisema.
Bibi
Mwanri aliongeza kuwa kukamilika kwa mradi huo kutatoa fursa za kuhudumia
shehena na abiria kutoka mikoa ya Mbeya, Njombe, na Ruvuma. Pamoja na kuhudumia
nchi za jirani ikiwemo Malawi, Msumbiji na Zambia.
Kwa
mujibu wa Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2011/2012 – 2015/2016) bandari
ni mojawapo ya vipaumbele vitano vya kimkakati vyenye lengo la kufungulia fursa za ukuaji uchumi wa nchi ili
kuweka misingi wa uchumi kwa watu walio wengi.
Msisitizo umewekwa katika kuvutia, kuanzishwa na kuendeleza viwanda vinavyotumia malighafi zinazopatikana nchini (kama vile viwanda vya nguo, mbolea, saruji, makaa ya mawe, chuma na bidhaa za chuma) na pia sekta ya madini kwa lengo la kuongeza mapato ya Serikali.
Pamoja na kipaumbele cha Maendeleo ya rasilimali watu na ujuzi: Mpango unahimiza kuwekeza katika elimu (hasa katika elimu ya juu na vyuo vya ufundi) na huduma za afya (kuongeza ubora na upatikanaji wa huduma) katika kujenga nguvu kazi itakayotuletea maendeleo ya kiuchumi na kijamii; na Utalii, Biashara, na huduma za Fedha ambapo jitihada zimewekwa kwenye uendelezaji uwezo wa kuuza katika masoko ya ndani na nje, kuongeza idadi ya watalii na matumizi yao wawapo nchini, na kuongeza upatikanaji wa huduma za kifedha.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni