Timu
ya Ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango
ikiwa katika picha ya pamoja katika jiwe la msingi la uzinduzi wa
maghala ya kuhifadhia mizigo katika Bandari ya Kasanga. Maghala hayo
yalifunguliwa rasmi na Makamu wa Rais, Mhe. Dkt. Mohamed Gharib Bilali
tarehe 22 Februari 2012.
Mkuu
wa Bandari ya Kasanga, Bw. Mponjoli Thompson Mwamafupa (Kushoto)
akimfafanualia jambo Kiongozi wa Timu ya Ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo
kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango, Bibi Florence Mwanri (Kulia)
wakati akimkabidhi taarifa ya maendeleo ya bandari hiyo.
Na Saidi Mkabakuli, Sumbawanga
Serikali imeazimia kuanza
kuiboresha bandari ya kimkakati ya Kasanga inayohudumia nchi za Burundi, Rwanda
na Kongo iliyopo katika Ziwa Tanganyika, mkoani Rukwa.
Ahadi hiyo imetolewa na Kiongozi
wa Timu ya Ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya
Mipango, Bibi Florence Mwanri wakati walipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya
miundombinu katika Bandari ya Kasanga.
Bibi Mwanri alisema kuwa serikali kupitia Mamlaka ya Bandari Tanzania imepanga
kuboresha bandari zote ili kuwa malango kuu la biashara kwa soko la ndani na
kwa nchi jirani ili kuongeza uwezo wa kuhudumia shehena kwa ufanisi.
“Tumedhamiria kuendelea kuboresha miundombinu ya bandari hususan miradi
iliyoibuliwa katika Programu ya Matokeo Makubwa Sasa ikiwemo Bandari ya Kasanga
ili kuweza kukidhi mahitaji ya utoaji wa huduma katika eneo hili,” alisema.
Bibi Mwanri aliongeza kuwa serikali pia imejipanga kuendelea kuboresha
miundombinu na ununuzi wa vifaa mbalimbali vya kuhudumia shehena katika bandari
za Dar es Salaam, Tanga, Mtwara, Kasanga na Kigoma na kukamilisha maandalizi ya
ujenzi wa bandari mpya za Mwambani (Tanga), Mbegani (Bagamoyo) na Bandari Kavu
ya Kisarawe.
Akizungumza na ugeni huo, Msimamizi Mkuu wa Bandari ya Kasanga, Bw.
Mponjoli Thompson Mwamafupa alisema kuwa Bandari hiyo ina fursa nyingi katika
kuhudumia shehena na abiria wanaopitia bandarini hapo.
“Bandari yetu ina fursa kubwa za kibiashara kwani tuna wateja wengi
kutoka ndani na nje ya nchi wanaotumia bandari yetu kupitishia bidhaa zao,
pamoja na abiria wanaosafiri kwenda nje na ndani ya Tanzania,” alisema.
Kwa mujibu wa Mpango wa Maendeleo kwa mwaka ujao wa fedha Serikali
imedhamiria kuboresha mazingira yatakayowezesha sekta binafsi kuwekeza katika
kujenga miuondombinu na kuboresha usafirishaji wa mizigo katika bandari zote
nchini.
Pia, Mpango huo
unaweka bayana kuendeleza na ukarabati na ununuzi wa vyombo vya usafiri na
usafirishaji katika maziwa.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni