Vijana wa kikundi cha usafi na uhifadhi wa mazingira cha Umoja wa vijana wazalendo Mbeya(UVIWAMBE), kutoka Mbalizi Mbeya, wakiwa katika picha ya pamoja mjini Iringa wakati wa ziara yao ya mafunzo.
HALMASHAURI
ya Manispaa ya Iringa, imesema inajivunia kuwa ni moja ya Halmashauri zenye
mazingira safi nchini, kutokana na juhudi za uelimishaji wananchi wake, ikiwa
ni pamoja na kutumia vyombo vya habari.
Hayo yalielezwa
juzi katika ukumbi wa mikutano wa Manispaa hiyo na Afisa Afya wa Manispaa hiyo,
Christian Ndenga, alipokuwa akitoa taarifa ya maarifa wanayoyatumia kuweka mji
safi, alipotembelewa na kikundi cha usafi na uhifadhi wa mazingira cha Vijana
wazalendo Mbeya(UVIWAMBE), kutoka wilaya ya Mbeya Vijijini, mkoani Mbeya.
Ndenga
alisema kuwa, manispaa hiyo imepata tuzo ya mshindi namba moja kuhusu usafi wa
mji, kutokana na jitihada kubwa zinazofanywa baina ya serikali, vikundi vya
usafi na wadau wengine wakiwemo wafanyabiashara.
“Tunajivunia
mafanikio haya kutokana na kwanza kuwepo kwa sheria zinazodhibiti wachafuzi wa
mazingira ambao hutozwa faini isiyozidi Shilingi Elfu Hamsini, kukasimu
madaraka ya masuala ya usafi ngazi za kata, uwepo wa vikundi vya usafi na
kutosubiri makontena ya uchafu yajae ndipo yakamwagwe” alisema Ndenga.
Alitaja pia
vyombo vingine wanavyotumia ili kuhakikisha mji unakuwa safi kuwa ni pamoja na
kuwatumia viongozi wa dini, shule na vyuo, huku akisema kuwa waandishi wa
habari wamekuwa mstari wa mbele kufika katika ofisi za manispaa kuhoji kama
kuna sehemu wameona uchafu jambo ambalo alisema kuwa linawapa msukumo wa
kufanya vizuri zaidi na kutoa elimu kwa wananchi.
Alisema kwa
sasa, wanapanga mpango wa miaka 20 ijayo kuandaa eneo la kutupia taka badala ya
kusubiri eneo walilonalo kwa sasa mpaka hapo litakapojaa.
Baada ya
taarifa hiyo, kikundi cha Uviwmbe waliongoza na afisa mmoja wa Manispaa hiyo
kitengo cha Afya, Ezekiel Mbushi, kwenda kutembelea soko la Iringa mjini na
kukutana na uongozi wa kikundi cha usafi cha mjini hapo kijulikanacho kwa jina
la Kikundi cha wafanyabiashara wa masoko(KWBS).
Mwenyekiti
wa kikundi hicho Augustino Ngao na katibu wake Aldo Kaduma, walisema kuwa, ili
wananchi waweze kutii sheria za usafi ni muhimu wakapatiwa elimu kwanza kabla
sheria haijaanza kufanya kazi ambapo walikiri kuwa pamoja na baadhi kupata
elimu katika manispaa hiyo, lakini bado wanakuwepo wanaokaidi.
“Changamoto
tunayopata katika kutekeleza kazi za usafi ni pamoja na baadhi kukaidi kutii
sheria, watu wa haki za binadamu kutukamata wanapowakuta baadhi ya vibarua wa
kikundi wakifanya kazi bila kuvaa grovu na pia vifaa kuwa duni yakiwemo
matolori ambayo ni tofauti na yale yaliyokuwa yakitengenezwa Mbeya na kiwanda
cha ZZK ambacho kilikufa” alisema Kaduma.
Mwanasheria wa
Halmashauri ya Mbeya, Prosper Msivala, ambaye aliongozana na wana kikundi cha
Uviwambe, alisema kuwa yeye alikuwa mwanasheria wa Manispaa ya Iringa na ni
mzawa wa mkoa huo, ambapo anaikumbuka historia mbaya ambayo iliwezesha manispaa
hiyo kufika hapo ilipo kuhusu suala la usafi.
“Hapa Iringa
mwaka 1988, kulitokea mlipuko wa kipindupindu ambapo kwa siku zaidi ya wananchi
50 walikuwa wakifa na kuzikwa, jambo ambalo lilihamasisha jamii nzima kuanza
kuzingatia suala la usafi na kuna wakati tulifikia mahala tukavunja vibanda
vilivyowekwa kiholela na baadhi ya nyumba na tukatishiwa kuuawa, lakini kwa
sasa mambo safi” alisema Msivala.
Mwenyekiti
wa kikundi cha Uviwambe, Ayas Yusuph, aliishukuru Halmashauri ya Mbeya kwa
kugharamia safari hiyo na Manispaa ya Iringa kwa kuwapa elimu na kuwaunganisha
na kikundi cha usafi cha KWBS na kwamba elimu na maarifa waliyopata katika
ziara hiyo ya mafunzo wataitumia vema.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni