JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
OFISI YA RAIS, TUME YA MIPANGO
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Mkutano wa Maafisa Mipango kufanyika Oktoba
Ofisi
ya Rais, Tume ya Mipango ipo katika maandalizi ya mkutano wa mwaka wa wachumi
na maafisa mipango unatarajiwa kufanyika Oktoba 2014 jijini Dar es Salaam kwa
lengo la kujadili masuala mbalimbali yanayohusiana na usimamizi wa uchumi na
mipango hapa nchini.
Mkutano
huu ambao ni wa kitaalamu unawakutanisha
wataalamu mbalimbali kutoka tasnia za mipango, uchumi, takwimu na maendeleo,
wenye wajibu wa kusimamia uchumi na mipango ambao hukutana kwa ajili ya
kujadili na kubadilishana uzoefu juu ya sera, mipango na kujenga mtandao wa
masuala ya maendeleo ya kitaaluma.
Mkutano
huu unatoa fursa kubwa ya kuwakutanisha kwa pamoja wataalamu hao na kujenga
uelewa wa pamoja juu ya uendeshaji wa shughuli mbalimbali za Serikali. Pia
hutoa fursa za kujadiliana kwa pamoja juu ya mafanikio na njia za kukabiliana
na changamoto kwa kubadilishana uzoefu na ujuzi kwenye masuala hayo.
Mkutano
huo ni muhimu katika kuimarisha utendaji kazi wa kada hizi kwa minajili ya kusukuma
gurudumu la maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini.
Kwa
kutilia mkazo masuala mbalimbali ya kimaendeleo yanayojitokeza hivi sasa, mkutano
wa mwaka huu utajikita katika kujadili masuala yafuatayo;
i)
Maendeleo ya Tasnia ya Wapanga Mipango
(wachumi, maafisa mipango na watakwimu);
Mkutano
utajadili fursa, na changamoto zilizopo katika kuleta maendeleo katika nchi. Huko nyuma kada hizi zilikuwa zinaratibiwa na iliyokuwa
Wizara ya Mipango Uchumi na Uwezeshaji. Kwa sasa watakuwa chini ya uratibu wa
Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango. Hatua hii itarahisisha utekelezaji wa mipango
mbalimbali ya nchi.
ii) Maandalizi ya Mpango wa Pili wa Maendeleo
wa Miaka Mitano (2015/16 – 2020/2021);
Utekelezaji
wa Mpango wa Kwanza wa Taifa wa Maendeleo 2011/12 – 2015/16) unaendelea na
tayari Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango imeanza kufanya mapitio ya utekelezaji
wake ili kujua mafanikio na changamoto. Hivyo, katika mkutano huo wapanga mipango
wanaandaliwa waweze kuanza kufanya maandalizi kwa ajili ya Mpango wa Pili wa Maendeleo
(2015/16 – 2020/21).
iii) Mwongozo wa Usimamizi
wa Uwekezaji katika Sekta ya Umma;
Serikali
imeandaa mwongozo wa Usimamizi wa Uwekezaji katika sekta ya Umma, lengo likiwa
kuimarisha utendaji, ufanisi na uwajibikaji katika matumizi ya rasilimali za
umma zilizotengwa kwa ajili ya miradi na program za maendeleo.
iv) Jinsi ya Kujiandaa
na Uchumi wa Gesi
Mkutano
utajadili ni kwa jinsi gani Tanzania inajipanga kufaidika na rasilimali ya gesi
asilia. Kwa kifupi masuala ya yanayohusu uwekezaji katika gesi asilia,
usimamizi na jinsi ya kutumia rasilimali na menejimenti ya mapato yatokanayo na
gesi, pamoja na ushiriki wa wananchi katika fursa mbalimbali zinazotokana na
ujio wa gesi hiyo.
Utayarishaji wa wataalam katika eneo hilo la gesi husani
vyuo vya ufundi, vyuo vikuu na kadhalika.
Washiriki
wa mkutano huu ni pamoja na wakurugenzi wa sera na mipango, maafisa mipango
kutoka kwenye wizara, Serikali za Mitaa, idara na wakala wa Serikali, pamoja na
taasisi za kitaaluma na watafiti wanaojishughulisha na masuala ya maendeleo na
uchumi.
Mkutano
wa mwisho wa mwaka wa maafisa mipango ulifanyika mkoani Morogoro tarehe 12
Machi 2010 ambapo uliandaliwa na Wizara ya Fedha. Mada nne zilizowasilishwa na kujadiliwa zilikuwa
ni;
i.
Wajibu wa wataalamu wa mipango katika Maendeleo ya Uchumi:
Mipango ya Kiuchumi, Utekelezaji na Uandaaji wa Taarifa;
ii.
Soko la Pamoja la
Afrika ya Mashariki;
iii.
Ujasiriamali na
Usimamizi wa Biashara kwa Wafanyabiashara Wadogo na Wakati; na
iv.
Ufanisi wa Uwekezaji
kutoka nje katika Uchumi wa Tanzania
MWISHO
Imetolewa na:
Ofisi ya Rais, Tume ya
Mipango
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni