Alhamisi, 11 Septemba 2014

MKURUGENZI, WANAHABARI NA WANANCHI MBEYA, KUISAFISHA MBALIZI


 Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mbeya, Upendo Sanga

MKURUGENZI wa halmashauri ya Mbeya, Upendo Sanga, baadhi ya wanahabari mkoani Mbeya, wananchi na wakuu wa idara za Halmashauri hiyo, wanatarajia kuongoza kampeni endelevu ya kuuweka safi mji wa Mbalizi wilayani humo na kutoa elimu ya uhifadhi wa mazingira.



Kampeni hiyo ya usafi, inaratibiwa na kikundi cha Vijana wanaofanya kazi ya kutunza na kuhifadhi mazingira kwa kujitolea mkoani hapa, wanaojulikana kwa jina la Vijana wazalendo Mbalizi(UVIWAMBA).



Akizungumza na waandsishi wa habari jana, mratibu wa kikundi hicho, Gordon Kalulunga, alisema kuwa, itakuwa mara ya pili kwa Mkurugenzi huyo na baadhi ya waandishi wa habari kuungana na juhudi za vijana wanaojitolea kufanya usafi katika mji huo.



“Ni faraja kubwa sana kwetu kuona Halmashauri yetu inaungana nasi katika kutimiza wajibu wetu kwa taifa, hasa tunapoona Mkurugenzi na waandishi wa habari wanakuja huku chini na kuona umuhimu wa kutoa support kwa kada ya watu tunaoamua kujitolea” alisema Kalulunga.



Alisema usafi huo utafanyika katika eneo la makao makuu ya Kanisa la Uinjilisti Tanzania mpaka eneo la stendi ya Umalila, na kuhitimishwa kwa kubadilishana mawazo endelevu ya usafi katika mji huo wa Mbalizi kati ya wananchi watakaojitokeza na wageni watakaoongozwa na Mkurugenzi wa halmashauri hiyo.



Naye makamu Mwenyekiti wa kikundi hicho, Ayas Yusuph, alisema kikundi chao kinafanya usafi kila siku ya Juma mosi ya juma kwa kushirikiana na baadhi ya wananchi wa mji huo.



“Mkurugenzi kuungana nasi ni jambo kubwa sana ambalo linatuongezea hamasa ya kuendelea kujitolea na hivi sasa tayari tumebandika matangazo kwa ajili ya kuwaeleza wananchi wenzetu kuwa kila mmoja siku hiyo afanye usafi kwa hiari katika makazi na maeneo anayofanyia kazi’’ alisema Ayasi.



Kwa upande wake Mkurugenzi Upendo Sanga, alisema, ataungana na vijana hao pamoja na baadhi ya wakuu wa idara ya mazingira, kufanya usafi katika mji huo ambao ni kioo cha wilaya na mkoa wa Mbeya kwa wageni wanaotumia usafiri wa ndege wa kimataifa wa Songwe.



“Nitashiriki katika zoezi hilo la usafi siku ya Jumamosi. Ni wajibu wangu na wananchi wote, maana Mbalizi ni kioo cha mkoa wa Mbeya kupitia uwanja wa Ndege wa kimataifa wa Songwe, ambao upo katika wilaya yetu na mgeni yeyote anayetaka kwenda katikati ya Jiji la Mbeya, lazima apite Mbalizi” alisema Upendo Sanga.


 AKISHIRIKI KUZIBUA MIFEREJI NA VIJANA WA MBALIZI AMBAO WAMEJITOLEA KUFANYA USAFI KATIKA MJI HUO.

 AKIWA NA VIJANA ENEO LA KAZI MBALIZI MWAKA JANA 2013.

Kushirki katika kazi hiyo ya usafi kwa Mkurugenzi huyo, kutakuwa kwa awamu ya pili, ambapo awali mwaka jana, alishiriki katika kuzibua baadhi ya mitaro iliyokuwa imeziba katika stendi kuu ya wilaya hiyo, iliyopo eneo la Tarafani katika mji wa Mbalizi.



Kwa sasa Serikali, inaendelea kukamilisha ujenzi wa barabara ya kiwango cha lami katika mji huo.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

NAIBU WAZIRI WA KILIMO MHE MWANJELWA AMUAGIZA MRAJIS KUFANYA UCHUNGUZI SACCOS YA MADIBIRA-MBARALI NDANI YA SIKU 14

Naibu Waziri wa Wizara ya Kilimo, Mhe Mary Mwanjelwa akisisitiza jambo wakati akizungumza na Viongozi mbalimbali wa Mkoa na kamati ya uli...