Alhamisi, 26 Juni 2014

WAZAZI LUBALA SEKONDARI, WANAVYOLIPA KUNI NA MBOGA KAMA ADA

 
SHULE ya sekondari Lubala iliyopo wilayani Rungwe mkoani Mbeya, ni shule inayomilikiwa na Mbujah Brothers Association nan i moja kati ya shule zinazofanya vizuri kitaalum yakiwemo masomo ya Sayansi.
 
Kuwepo kwa shule hiyo katika eneo la kitongozji cha Lubala, Kijiji cha Lukata, kata ya Kinyala, Tarafa ya Ukukwe, kumesaidia kupatikana na kupanuka kwa miundombinu ya maji na umeme katika eneo hilo.
 
Wanakijiji pia wamepata ajira ndogondogo kama vile vibarua, wajenzi, wapishi na walinzi.
 
Mbali na faida hizo, pia wanafunzi walio jirani na shule hiyo wanapewa nafasi za kufundshwa bure nyakati za usiku na Jumamosi na walimu wa shule hiyo ili kukuza mahusiano na taaluma.
 
Wanafunzi wa shule hiyo, wanasema hakuna masomo mepesi kama ya sayansi kutokana na masomo hayo kuwa na hisia za viumbe hai.
 
Wanafunzi waliokutwa katika maabara ya somo la Biolojia shuleni hapo, waliliambia gazeti hili kuwa tangu waanze masomo katika shule hiyo, wamehamasika kusoma masomo hayo kutokana na shule hiyo kuwa na maabara na vifaa vya kutosha.
 
Mwanafunzi wa kidato cha pili, William Kulwa(15), anasema alifaulu kujiunga na kidato cha kwanza shule ya serikali ya Tukuyu Day, lakini wazazi wake wakampeleka katika shule hiyo ambapo malengo yake kwa baadae ni kuwa Daktari wa binadamu.
 
“Natarajia kuwa Daktari maaana masomo ninayosoma ya sayansi yana hisia za binadamu na viumbe hai jinsi wanavyoishi, ingawa somo la Fizikia bado linanisumbua kidogo’’ alisema mwanafunzi William.
 
Happy John(15) wa kidato cha pili, anasema kuwa anatarajia kuwa Injinia baada ya kuhitimu masomo yake hapo baadae.
 
Katika hafla fupi ya maazimisho ya miaka kumi ya mafanikio ya shule hiyo yaliyofanyika shuleni hapo mwanzoni mwa mwezi Mei mwaka huu, Mkurugenzi wa shule ambaye pia ni mkuu wa shule, Noah Mwasiposya, anasema shule hiyo imepata mafanikio makubwa kutokana na kuhamasisha kwa vitendo masomo ya sayansi.
 
“Mwaka 2004, tulianza na wanafunzi 215 na sasa tuna wanafunzi 1031 huku tukizidi kuimarisha taaluma, majengo na mazingira na tunaishukuru Hospitali ya Igogwe iliyopo karibu nasi, kwa ajili ya matibabu ya watumishi na wanafunzi’’ alisema Mkuu wa shule hiyo.
 
Kwa upande wake, Mwalimu Paison Mwalinga, anasema hamasa wanayoitia kwa wanafunzi kupenda masomo ya sayansi katika shule hiyo kwa vitendo, ndiyo nguzo moja wapo ya wanafunzi wao kupenda masomo hayo.
 
“Tunahamasisha vijana wengi kupenda masomo ya sayansi kwa kuwa na stream mbili za sayansi na kila mwaka zaidi ya vijana 60 wanajikita katika masomo hayo. Wanafunzi wengi wapo katika vyuo vya uuguzi na sekondari kidato cha tano na sita’’ alisema Mwakalinga.
 
Mwalimu Peter Nkanje, alisema mbali na mafanikio ya shule hiyo ya Lubala, changamoto wanayopata ni pamoja na kupata taarifa za wanafunzi wao wa kidato cha Nne wanaohitimu hapo na kujiunga na shule za sekondari katika masomo ya sayansi ambao wanashindwa kufaulu vizuri kutokana na shule wanazoenda kutokuwa na mazoezi ya mara kwa mara tofauti na shule yao.
 
Anasema mafanikio ya shule hiyo haiwezi kukamilika bila kuwataja baadhi ya watumishi wa shule hiyo ambao wapo zaidi ya miaka tisa tangu kuanzishwa shule hiyo.
 
Anawataja Noah Mwasiposya, yeye menyewe Peter Nkanje, John Charles Ngullah, Paison Mwakalinga, Yonathan Yaunde, Isaack Jonas na Maiko Maganga.
 
Wengine ni wafanyakazi wasio walimu ambao ni Alimundu Pasukali, Getruda Michael, Matrida Tosigwe, Rose Mwangamilo, Tumaini Samboma, Lucia Kabuje na Upendo Sambo.
 
Mwenyekiti wa bodi ya shule hiyo, Dr. John Mwakatage, anasema ni vema wazazi wa wanafunzi wanaohitimu katika shule hiyo kidato cha Nne na kufaulu, wakawabakiza watoto wao ili waendelee na kidato cha tano na sita hap badala ya kuwapeleka kwenye shule za serikali.
 
Anataja sababu kubwa ya hoja yake hiyo kuwa ni shule nyingi za serikali kumejaa migogoro mingi kati ya walimu na serikali na migomo ya mara kwa mara inayosababisha athari kubwa kwa wanafunzi.
 
“Mzumbe na nyingine zilikuwa shule nzuri, kwasasa wote tunashuhudia ilivyo, mwacheni mfugaji aendelee kulelewa na mfugaji aliyemzoea’’ anasema Mwenyekiti huyo wa bodi.
 
Afisa elimu Sekondari wa Halmashauri ya Rungwe, Anna Chigulu, anasema kuwa tangu utumishi wake, hajawahi kuona shule inayozawadia wanafunzi waliohitimu na kufaulu kama inavyofanya shule hiyo ya Lubala.
 
Mbali na mshangao huo, pia aliitaja shule hiyo kuwa ya mfano katika mkoa wa Mbeya kama siyo nchi nzima kwa ujumla, kutokana na uogozi kuruhusu wazazi maskini wa kipato cha fedha, kupeleka kuni ama mazao, kisha kuthaminishwa kuwa ada ya mwanafunzi.
 
“Wilaya ya Rungwe kwa mkoa wa Mbeya, tumeweza kuwa vinara wa matokeo makubwa sasa(BRN), shule ya Lubala imetupandisha chati’’ alisema Afisa elimu huyo.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

NAIBU WAZIRI WA KILIMO MHE MWANJELWA AMUAGIZA MRAJIS KUFANYA UCHUNGUZI SACCOS YA MADIBIRA-MBARALI NDANI YA SIKU 14

Naibu Waziri wa Wizara ya Kilimo, Mhe Mary Mwanjelwa akisisitiza jambo wakati akizungumza na Viongozi mbalimbali wa Mkoa na kamati ya uli...