Jumatano, 5 Machi 2014

ST.FRANCIS WATOA NENO KWA SERIKALI KUHUSU ELIMU

 Mkuu wa shule hiyo, Sister Francisico Kwele.
 Picha ya pamoja kati ya Mkuu wa wilaya ya Rungwe, Crispin Meela na viongozi wa Tamongsco.
Mkuu wa wilaya ya Rungwe, Crispin Meela.
SHULE ya wasichana ya St. Francis iliyopo Jijini Mbeya, imesema ili shule za serikali ziweze kufanya vizuri katika matokeo ya mitihani ya kitaifa ni vema watumishi wake wakawa kitu kimoja.

Hayo yamesemwa na mkuu wa shule hiyo, Sister Francisico Kwele, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini hapa baada ya kukabidhiwa tuzo ya cheti cha shule iliyofaulisha katika kanda ya nyanda za juu kusini.

Tuzo za vyeti kwa shule zilizofanya vizuri zimetolewa na umoja wa shule za binafsi na vyuo (TAMONGSCO) jana, katika mkutano wao unaofanyika katika ukumbi wa Youth Center Jijini hapa.

‘’Siri ya mafanikio yetu ni kufanya kazi kama team work na comitment na hatutoi elimu kama biashara bali huduma, tunajenga ushirikiano wa walimu, wanafunzi ikiwa ni pamoja na kuwa na vifaa vyote vinavyohitajika zikiwemo maabara’’ alisema Kwele.

Mwenyekiti wa TAMONGSCO kanda ya nyanda za juu kusini, Padre Innocent Sanga, alisema wadau wengi wanashindwa kuwekeza katika sekta ya elimu kutokana na vikwazo kuwa vingi ikiwemo kero ya kodi inayotozwa na Mamlaka ya mapato Tanzania(TRA), Halmashauri na mawakala.

‘’Wanakwamisha uboreshaji wa shule, tunaomba kodi ziondolewe, shule binafsi zipewe ruzuku, riba za mikopo ziwe kati ya asilimia 5-7 tofauti na sasa ambapo riba ni asilimia 20 na kuwe na ushindani wa shule ili kuboresha ufaulu’’ alisema Padre Sanga.

Mwenyekiti wa umoja huo Taifa, Mahmoud Mringo, alisema elimu imefanyiwa maborsho makubwa lakini mtu hawezi kuona mpaka akutane nayo.

‘’Zama za serikali kutowasikiliza walimu ziliishia Mbeya baada ya Rais Jakaya Kikwete, kukutana nasi na kuandika kero zote kwa mkono wake kwenye diary yake, mnyonge mnyongeni lakini tumpe haki yake na serikali imetutambua ambapo wasimamizi wa elimu ni sisi Tamongsco na Tamisemi’’ alisema Mringo.

Makamu Mwenyekiti taifa wa umoja huo, Mboka Mwambusi, alizitaja shule zilizofanya vizuri na kutunukiwa tuzo za vyeti kuwa ni shule za Msingi Ilasi, Swilla, St.Marys, St.Aggrey zote za Mbeya na shule ya Msingi Mvimwa kutoka Nkansi Rukwa.
Kwa upande wa sekondari zilizofanya vizuri na kutunukiwa ni St. Francis, Kaengesa, Padahill, Uwata Boys na St. Marcus Chemichemi.

Mkuu wa wilaya ya Rungwe, Crispin Meela, alimwakilisha Mkuu wa mgeni rasmi, Mkuu wa wilaya ya Mbeya, Dr. Norman Sigalla, katika kikao hicho ambapo aliwapongeza na kwamba shule za binafsi zimeisaidia serikali kutoa elimu kwa wanafunzi wanaokosa nafasi.

‘’Waliokuwa wakikosa nafasi walikuwa wanaitwa majina mabaya kwamba wamefeli na tunashukuru shule za binafsi kwa sababu lengo ni kuwa na elimu bora na taifa la wasomi’’alisema Meela.

Aidha alitoa wito kwa shule ambazo hazikuweza kufanya vizuri kuiga na kujifunza maarifa kutoka kwa wenzao wa shule za dini ambazo zinaonekana kuongoza kufaulisha wanafunzi huku akionya kwa wale wanaoiba mitihani kuacha mara moja.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

NAIBU WAZIRI WA KILIMO MHE MWANJELWA AMUAGIZA MRAJIS KUFANYA UCHUNGUZI SACCOS YA MADIBIRA-MBARALI NDANI YA SIKU 14

Naibu Waziri wa Wizara ya Kilimo, Mhe Mary Mwanjelwa akisisitiza jambo wakati akizungumza na Viongozi mbalimbali wa Mkoa na kamati ya uli...