Washiriki wa semina hiyo wakifuatilia kwa makini mafunzo yanayofanyika katika ukumbi wa Coffee Garden jijini Mbeya.
WANANCHI wametakiwa kupewa elimu juu ya
umuhimu wa uchaguzi wa serikali za mitaa ili kuwawezesha kupata viongozi bora
watakao saidia kutatua changamoto zinazoikabili jamii.
Aidha imeelezwa kuwa uchaguzi wa
serikali za mitaa ni muhimu kuliko uchaguzi mkuu kutokana na kupata viongozi wa
ngazi ya chini ya Vitongoji na Vijiji ambako ndiko wananchi wenye hali ngumu
wanapatikana hivyo kutokana na elimu itasaidia kupata viongozi bora.
Hayo yamebainishwa na Afisa
Uhusiano wa Mtandao wa Jinsia Tanzania(TGNP), Deo Temba katika mafunzo ya
wanahabari wa Mkoa wa Mbeya kuhusu namna Waandishi wa habari wanavyochangia
kutatua changamoto zinazoikabili jamii, yaliyofanyika katika ukumbi wa Coffee
Garden iliyopo jijini hapa.
Alisema Wanahabari wanapaswa kuwa wa kwanza
kuelimishwa kuhusu uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika Mwaka
huu ili wao wakatoe elimu hiyo kwa wanajamii ili kuona umuhimu wa kushiriki
katika uchaguzi huo kwa manufaa ya maendeleo yao.
Alisema viongozi wa vijiji na vitongoji
ndiyo wanaoishi na wananchi kwa ukaribu na kuzijua changamoto mbali mbali
zinazoyakabili maeneo husika ambapo wananchi wanapaswa kupewa elimu jinsi ya
kupata viongozi watakaowafaa na kusaidia kutatua changamoto zao na siyo bora
kiongozi.
Mbali na hayo Afisa huyo aliongeza kuwa
Wajumbe wa bunge maalum la kupitia mchakato wa katiba mpya
unaoendelea mkoani Dodoma wanapaswa kuhakikisha maswala yote yanaigusa
jamii yapewe kipaumbele na kutamkwa wazi katika Katiba mpya na siyo kuzungumzia
muundo wa Serikali.
Aidha katika mafunzo hayo, Waandishi, na
Mtandao wa jinsia(TGNP) walijadili changamoto zinazowakabili katika kuibua
maswala ya jinsia katika jamii na namna ya kukabiliana nayo, Uchaguzi wa
Serikali za Mitaa pamoja na mchakato wa Katiba mpya na umuhimu katika jamii.
Na Mbeya yetu
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni