Hata hivyo, tunasikitika kwamba Haki ya Afya haijatambuliwa kwenye rasimu kama haki ya Msingi ya kila mwananchi. Tukiwa kama wadau wa Afya,
tunapenda kufafanua kuwa Afya ni kuwa mzima kiakili, kimwili,
kijamii, kimaadili na kimazingira, hivyo Afya ni haki ya msingi ya kila mwananchi. Mwananchi anapokosa haki hii ya msingi hushindwa kushiriki katika shughuli mbalimbali
za kuleta maendeleo, na kupata madhara
mengine yanayoweza kusababisha kifo.
Katika rasimu ya pili ya Katiba iliyokabidhiwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
kwa ajili ya kujadiliwa katika Bunge
la Katiba Februari 2014, Afya kama Haki ya msingi ya binadamu haijatambuliwa kama vile haki zingine zilivyotambuliwa kwa mfano elimu.
Tunatambua kwamba Katiba ndiyo sheria Mama, hivyo basi, pasipo kutambua
Haki ya Afya, sheria ndogondogo haziwezi kulitambua suala hili nyeti, na hivyo kuiweka jamii na vizazi
vijavyo katika hali hatarishi kiafya.
Juni 2013, Sikika iliomba na hatimaye
ikapata kibali rasmi kutoka Tume ya mabadiliko ya Katiba cha kutambuliwa kama Baraza la Katiba kwa ajili ya kuchambua na kukusanya maoni juu ya Rasimu ya Katiba.
Sikika
ilishirikisha wananchi na Asasi mbalimbali kama Tanzania Public Health Association (TPHA),
Medical Association of Tanzania (MAT) na Kituo cha Sheria
na Haki za Binadamu
(LHRC) katika
kuchambua rasimu ya kwanza ya Katiba na hatimaye kutoa mapendekezo ya kutambua haki ya afya kwenye Katiba.
Mapendekezo hayo yaliwakilishwa kwa Tume Agosti 2013 lakini hayakuchukuliwa, kwa sababu moja au nyingine.
Kutokana na umuhimu
wa Afya kwa kila mwanadamu, tunapendekeza Afya itambulike kama Haki ya msingi katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania na iwe ni wajibu wa kila mwananchi kutunza Afya yake, kushiriki na kusimamia masuala
yanayohusu afya ya jamii. Pia serikali ya Jamhuri ya Muungano, mamlaka za nchi pamoja na
taasisi zihakikishe kuwa Haki hii ya msingi inasimamiwa vyema.
Pia itambuliwe
kuwa ni kosa la jinai kwa
mwananchi kufanya tendo lolote linalohatarisha afya ya mtu mwingine na jamii kwa ujumla.
Pia tunaomba serikali
na wadau wa Katiba waangalie
na kutambua Afya kama suala la msingi
linalotakiwa lizingatiwe katika
sera zote za maendeleo ili kuweza kulinda afya ya Watanzania wote.
Aidha, tunapendekeza ibara
ya 41 inayozungumzia uhuru na haki ya mazingira
safi na salama iongeze masuala
haya;
(1) Serikali ihakikishe kuwa kila mwekezaji afanye tathmini ya kiafya kabla mradi haujaanza na utekelezaji wa mapendekezo ushirikishe wadau wote hususan,
ngazi ya jamii.
(2) Serikali na vyombo husika
vidhibiti uingizwaji na utumiaji wa vifaa/vyakula/madawa
vyenye viwango duni na pia kutoruhusu matumizi ya madawa au vyakula bila ya ushahidi
wa kitafiti unaothibitisha usalama wa mtumiaji/mlaji.
Kutompatia mwananchi haki ya afya ni sawa na kumnyima
haki ya kuishi kama ilivyoainishwa katika ibara 24 ya rasimu ya Katiba,
maana uhai wa mtu unategemea afya aliyo nayo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni