Jumamosi, 22 Februari 2014

HOJA YA MWANAKIJIJI

Wapo wenye mapenzi na CCM, CDM isisahau hili!

KAMA nilivyodokeza wiki iliyopita naomba wiki hii niangalize jambo moja ambalo inaonekana kwa wale wapinzani na wengine wanaopenda mabadiliko ya kweli ya kisiasa wanaanza kulisahau; kuwa, wapo Watanzania wenye mapenzi kweli na Chama Cha Mapinduzi!
CDM kama chama kikuu cha upinzani nchini kinaonekana wakati mwingine kinajisahau katika hili na mara zote kinapofanya hivi kinajikuta kinashangazwa ama na matokeo ya kura au na mwitikio wa Wana CCM kutoka kwa viongozi wao.
Kosa kubwa sana la mtu kupendwa ni kudhani kuwa wewe peke yako ndiye unapendwa. Na wakati mwingine ukigundua kuwa na wengine wapo wanaopendwa unaweza kujisikia donge la kwanini na wao wanapendwa na hata unaweza usielewe kwanini na wao wanapendwa.
Watu wanapenda kwa sababu mbalimbali; wapo wenye kupenda kwa sababu za kihistoria, wengine wanapendwa kwa sababu ya vile wanavyofanyiwa na wale wanaowapenda au sababu nyingine mbalimbali.
Katika siasa ni hivyo hivyo; wapo watu wanapenda chama tawala kwa sababu mbalimbali na wengine wanapenda vyama vya upinzani.
Katika nchi yetu wapo watu wanaipenda CUF na wengine wanaipenda NCCR-Mageuzi; na wapo wenye kuipenda CDM kama vile wapo wenye kukipenda Chama Cha Mapinduzi.
Binafsi naamini makosa ya wapinzani – na hasa CDM – ni kufikiria (hata kwa mbali) kuwa hakuna watu wenye kuipenda CCM kwa dhati!
Wapo wenye sababu
Kuna watu watu wanaipenda kwa sababu mbalimbali; na sababu hizo zinatofautiana na ni nyingi kama idadi ya watu walionazo.
Wapo wenye kuipenda kwa sababu ya wazazi wao, wengine wanaipenda kwa sababu wana imani nayo, na wengine wanaipenda kwa sababu wanaona hakuna mbadala wake.
Na wengine wana sababu za ndani kabisa ya mioyo kiasi cha kuwa tayari kufanya lolote na vyovyote kuona kuwa CCM inaendelea kuwa madarakani.
Wapo wengine hawana sababu
Na wapo wengine ambao wanaipenda na ukiuwaliza sababu utaona hawana sababu zaidi ya kukubali tu kuwa “wanaipenda tu yaani”.
Huwezi kushangaa wengine wanaipenda kwa kuziona zile rangi tu za kijani na njano! Wengine wanaipenda kwa sababu rafiki zao, mashosti wao, au wenza wao wanaipenda!
Wapo wenye kuipenda kimkakati zaidi
Wengine wapo humo ndani na wanaipenda CCM kimkakati zaidi; wanaichukulia CCM kama ngalawa ambayo wanahitaji kuitumia kuwavusha wanakotaka kwenda.
Wanaweza wasikubaliane na sera zake, uongozi wake au hata kuchukia mfumo wake lakini kwa vile inawaahidi kuwapeleka sehemu basi wanavumilia na kuimba sifa zake!
Wengi wao hawa hujulikana wakati wa uchaguzi pale ambapo majina yao yasipopitishwa kugombea au wasipopata vile walivyodhani watapata kwa kubakia CCM.
Yanaweza kuwa ni mapenzi ya kinafiki lakini bado ni mapenzi kwani wakipata kile wanachokitaka utawaona hadi kwenye nyumba zao kuna bendera za CCM!
Wapo wanaoipenda kwa sababu wanaichukia CDM
Wapo wengine wanaipenda CCM na wanaichagua kila kukicha si kwa sababu nyingine, ila kuonyesha chuki na dharau yao dhidi ya CDM.
Hawa wanaipenda CCM kwa sababu hawawezi kuipenda CDM! Wanaweza kabisa kukubali mapungufu ya CCM, na wakakubali kuwa ina matatizo lukuki lakini watakuambia bila kupepesa macho kuwa “sijaona mbadala wa CCM” na wengine wanasema tu “siwezi kuipenda CDM”.
Mtu anaweza asielewe mantiki hiyo lakini ndani ya fikra za watu hao mawazo hayo yanaonekana kuwa na mantiki!
CDM ni lazima itambue jambo hili na inapofanya mikakati yake iliweke mawazoni. Kwamba, si watu wote wanaichukia CCM nchini na wapo ambao hata wakiitwa kuifia wataifia kuitetea!
Na hawa ambao wanaipenda CCM hivi ndio hawa hawa ambao watajiandikisha kupiga kura na wakati wa kupiga kura bila makeke wala mbwembwe wataenda na kuchagua wagombea wa CCM.
Hili ni muhimu kulifikiria ukiangalia matokeo mbalimbali ya uchaguzi. Katika mawazo ya kawaida unaweza kuamini kuwa katika Tanzania hakuna watu wenye kuipenda CCM kabisa.
Ukiangalia mikutano na hamasa ya CDM mijini na vijijini unaweza kuamini kabisa kuwa CDM inakubalika kila sehemu.
Ikifanyika mikutano ya kampeni unaweza kuamini kabisa kuwa kwenye eneo husika wapenzi wa CDM ni wengi kuliko wapenzi wa CCM. Lakini kura zinapokuja watu wanashangaa CCM wameshinda!
Ni rahisi kulaumu mfumo, kulaumu daftari la wapiga kura, au kulaumu matumizi ya vyombo vya dola. Ni kujaribu kuamini kuwa hivyo vyote visingekuwa vilivyo basi CDM wangeambulia kura zote na CCM isingeambulia hata moja.
Lakini ukweli ni kuwa hata daftari la wapiga kura likiboreshwa kila mwezi, hata polisi wakiwa huru bila upendeleo na mfumo ukawa wa haki kwa kiasi chote kinachowezekana bado utakuta kuwa wapo watu kwa maelfu bado wataipigia kura CCM!
Kwanini?
Kwa sababu binadamu si ng’ombe anayechungwa na kupelekwa kula anakotaka mchungaji na kupewa maji kwa jinsi anavyotaka mchungaji!
Mwanadamu ana uhuru wa kuamua kukubali au kukataa jambo hata kama jambo hili halina faida ya mara moja kwake.
Mwanadamu anaweza tu kushawishiwa katika siasa kufuata mrengo fulani au siasa za upande fulani lakini katika demokrasia hawezi kulazimishwa kukubali au kukataa siasa hizo.
Ni kwa msingi huo basi utaona kuwa CDM inaweza kujikuta kwenye matatizo ya mara kwa mara kudhania kuwa wote wanaokuja na kunyosha vidole viwili juu wakiimba “people’s power” ndio wana mapenzi!
Kuangalia picha za maelfu ya watu wakiangalia kwa matumaini wakishika vichwa kwa maombolezo na kufikiria kuwa wote hawa wanaiunga mkono CDM ni kujidanganya na kutokuielewa Saikolojia ya Siasa (Political Psychology).
Maandiko yanamnukuu Yesu akionya kuwa: “Si wote waniitao Bwana Bwana wataingia mbinguni”. Kwamba, wapo ambao hata watafanya miujiza na ishara lakini kumbe si wafuasi wake!
Hili ni kweli; wapo wenye kuvaa nguo za CDM, wenye kuimba na kusema lugha yote nzuri ya kiupinzani lakini wakati ukifika wanapiga kura zao kuichagua CCM.
Wale wenye kutaka mabadiliko na wapinzani kwa ujumla nchini tukitambua hili tutajipunguzia matumaini ya uongo na kuanza kupanga mikakati ambayo inalichukulia jambo hili kwa undani.
Mikakati ambayo itapangwa kuangalia ni jinsi gani tunaweza kuwashawishi watu wenye mapenzi na CCM kubadili upande. Maana kama tunaendelea kila kukicha kuwashawishi watu ambao tayari wameshashawishiwa tuna uhakika gani wa kufanya vizuri kama wale ambao wanatakiwa kushawishiwa hawajashawishiwa?
Jukumu na changamoto kubwa kwa CDM sasa hivi ni kutafuta njia ya kuweza kuwafikia wale ambao hawajaamua kuja kwenye upinzani na ambao bado wana imani na CCM.
Kama hawa hawajashawishiwa na mahubiri ya ufisadi, na hotuba za kina Lissu bungeni; kama watu hawajashawishiwa na hotuba kali za kina Mbowe na Slaa kwenye majukwaa ya kisiasa tangu 2010; hawa watashawishiwa na kitu gani?
Fikiria hakuna mahali popote ambapo umefanyika uchaguzi ambapo CDM ilishinda huku CCM ikipata kura sifuri! Kwani hata huko wapo masalia wa CCM!
Tukipata jibu la swali hili tutakuwa tumepata njia ya kuvuka kizingiti kikubwa zaidi cha kuweza kugeuza mwelekeo wa kura kuelekea uchaguzi wa Serikali za Mitaa na ule wa rais.
Hivi sasa ukiangalia sana utaona kuwa CCM bado ina wapenzi wengi tu tena wale walioapa na kuahidi kabisa kuwa “Mapinduzi Nitakulinda Mpaka Kufa”! Kama wale waliofanya hivyo kwa CDM.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

NAIBU WAZIRI WA KILIMO MHE MWANJELWA AMUAGIZA MRAJIS KUFANYA UCHUNGUZI SACCOS YA MADIBIRA-MBARALI NDANI YA SIKU 14

Naibu Waziri wa Wizara ya Kilimo, Mhe Mary Mwanjelwa akisisitiza jambo wakati akizungumza na Viongozi mbalimbali wa Mkoa na kamati ya uli...