Ijumaa, 28 Februari 2014

MWIGULU NCHEMBA ASEMA SERIKALI HAITAONGEZA POSHO KWA WABUNGE WA BUNGE LA KATIBA

Nchemba katika mkutano wa uzinduzi wa kampeni za CCm Ifunda


NAIBU Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) ambaye pia ni Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba amewataka wabunge wa bunge maalumu la Katiba wanaotaka nyongeza ya posho kujiondoa katika bunge hilo kama hawaridhiki nayo.

“Ndio wachape mwendo; maana kuna wengine wanasema wana biashara zao zinawalipa zaidi ya Sh 300,000 zinazotolewa kwa siku na serikali, ni vizuri wakaenda kusimamia biashara zao,” alisema.

Akizindua kampeni za uchaguzi mdogo wa ubunge katika jimbo la Kalenga kwa kumnadi mgombea ubunge wa jimbo hilo kupitia CCM , Godfrey Mgimwa, Nchemba serikali haitawatendea haki watanzania kama itakubaliana na matakwa ya baadhi ya wabunge wanaotaka nyongeza ya posho.

 “Nimekataa, sitakubali serikali iongeze posho kwa kuzingatia sababu zilizotolewa na baadhi ya wabunge wanaotaka nyongeza hiyo.”

Alisema anajua kuwepo kwa kamati iliyokuwa ikilifanyia kazi suala hilo na mapendekezo yake kuyawasilisha kwa Rais Jakaya Kiwete.

“Rais ni mtu mwenye hekima na busara nyingi, amesikia kilio cha watanzania, anajua hali ya kiuchumi ya taifa hili, anajua mahitaji mengine mengi ya watanzania kwa kutumia rasilimali hizi hizi tulizonazo; ni lazima atatuomba ushauri sisi kama wasaidizi wake,” alisema.

Alisema posho wanayopewa wabunge hao inazingatia hali halisi ya nchi na kwamba hatakubali iongezwe.

Alisema badala ya kudai nyongeza ya posho, wabunge wanaoshiriki bunge hilo wanatakiwa kuonesha uzalendo kwa kujisifu kupata fursa hiyo muhimu ili wawakilishe watanzania wenzao kutengeneza sheria mama ya nchi.

“Ni mambo ya uzalendo; nakumbuka nikiwa mdogo kuna watu walisikitika kukosa fursa ya kwenda kupambana na Nduli Idd Amin wakati wavita ya Kagera, na wale waliokwenda walifuraji na kuonesha ushajaa wao pamoja na kwamba maisha yao yalikuwa hatarini,” alisema.

Alisema watu wanaotaka kuikomboa nchi yao wakitanguliza maslai yao mbele ni hatari kwa maendeleo ya Taifa.

Alisema wabunge wa bunge maalumu la Katiba hawajakodishwa, hawafanyi kazi kama washauri wataalamu, wanafanya kazi hiyo kwa niaba ya watanzania wengine wanaotaka kuona nchi inakuwa na Katiba Mpya.

Alisema wakati wabunge hao wakidai nyongeza ya posho wanasahau kwamba nchi hii ina mambo mengi yanahitaji fedha ili isonge mbele.

“Wanajua kwamba hatujalipa wakandarasi, wanajua kwamba walimu zaidi ya 36,000 wanaidai serikali na wanajua kwamba kuna baadhi ya watumishi wa serikali wanapata kwa mwezi chini ya kiwango wanacholipwa wao kwa siku,” alisema.

Alisema ili nchi ipate maendeleo ni lazima mambo yote ya msingi yaendelee kufanyika kwa kutumia rasilimali zilizopo.

“wanajua wananchi wanahitaji mbolea ya ruzuku, maji, barabara, umeme, huduma nzuri za afya, shule na mengine mengi” alisema.

Alisema wanaona kiasi hicho hakiwatoshi na wana matumizi zaidi ya Sh 300,000 kwa siku wakendelee na shughuli zinazowafanya wapate zaidi ya kiasi hicho.

Akimnadi Godfrey Mgimwa, Nchemba alikishangaa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kwa kuingia katika uchaguzi huo.

“Watanzania lazima waelewe dhana ya uchaguzi mdogo; uchaguzi huu hauendi kubadili serikali, serikali iliyopo ni ya CCM na inatekeleza Ilani yake,” alisema.

Alisema wananchi walikwishatoa ridhaa mwaka 2010 kwa kuchagua mbunge na madiwani wote wa CCM kwahiyo kinachofanyika katika uchaguzi huo ni kuziba nafasi.

“Haiwezekani mchezaji wa Simba akatolewa uwanjani akaingizwa wa yanga au wa Yanga akatolewa akaingizwa wa Simba; kwenye siasa hatuhitaji ushabiki, mpeni kura zenu mgombea wa CCM kwasababu yeye ndiye anayetekeleza Ilani ya CCM,” alisema.

Alisema CCM ina mkataba na wana Kalanga na imejipanga vyema kutekeleza Ilani yake kama ilivyoahidi wakati wa Uchaguzi Mkuu wa 2010.

Alisema hakuna litakalofanywa na mgombea wa Chadema katika kipindi kilichobaki kama atachaguliwa kuwa mbunge wao.

“Mkimchagua na mtakapomuuliza tena majibu yake yatakuwa yale yale, sijatekeleza ahadi zangu kwasababu serikali ya nchi hii imeundwa na CCM,” alisema. 
CREDIT; Bongo leaks 

MWIGULU ALIVYOZINDUA KWA KISHINDO KAMPENI ZA CCM KALENGA.

 Abdul Adam, Mtoto wa Spika wa Bunge wa zamani Chifu Adamu Sapi Mkwawa, akimpongeza mgombea wa CCM katika Uchaguzi mdogo jimbo la Kalenga, Iringa Vijijini, Godfrey Mgimwa, wakati wa mkutano wa uzinduzi rasmi wa kampeni za CCM uliofanyika Viwanja vya Ifunda, Februari 27, 2014.
 Wananchi wakinyoosha mikono kuunga mkono kuwa mgombea wa CCM anafaa, wakati wa mkutano wa uzinduzi rasmi wa kampeni za CCM uliofanyika Viwanja vya Ifunda, Februari 27, 2014.
 Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Bara), Mwigulu Nchemba akionyesha makada wa CCM,  Alphonce John (kushoto) na Musa Tesha, walionusurika kuuawa na watu wanaodaiwa kutumwa na Chadema kwa mmoja kumwagiwa tindikali na mwingine kutobolewa jicho kwenye kampeni zinazohusu udiwani na Ubunge, katika maeneo ya Igunga na Kahama, alipokuwa akieleza fuji za Chadema, wakati wa mkutano wa uzinduzi rasmi wa kampeni za CCM uliofanyika Viwanja vya Ifunda, Februari 27, 2014.
  Alfonce aliyetobolewa jicho Kahama akizungumza jukwaani.
  Mwigulu akihutubia, wakati wa mkutano wa uzinduzi rasmi wa kampeni za CCM uliofanyika Viwanja vya Ifunda, Februari 27, 2014.
 Mwigulu (4th) na mgombea wakitroti na Green Guard, wakati wa mkutano wa uzinduzi rasmi wa kampeni za CCM uliofanyika Viwanja vya Ifunda, Februari 27, 2014.
 Katibu wa CCM, wilaya ya Mufindi, Miraji Mtaturu, alionyesha mbao zenye misumari inayodaiwa kutegwa njiani na Chadema, kwa nia ya kudhuru msafara wa mgombea wa CCM ktk jimbo la Kalenga.
 Katibu wa CCM  mkoa wa Iringa, akishauriana jambo na Mwenyekiti wake Joyce Msavatavangu
 Mjumbe Kamati Kuu ya CCM, Pindi Chana,  akitema cheche jukwaani, wakati wa mkutano wa uzinduzi rasmi wa kampeni za CCM uliofanyika Viwanja vya Ifunda, Februari 27, 2014.

Godfrey Mgimwa-Mgombea wa CCM uchaguzi mdogo jimbo la Kalenga, Iringa.
Imetayarishwa na theNkoromo Blog

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

NAIBU WAZIRI WA KILIMO MHE MWANJELWA AMUAGIZA MRAJIS KUFANYA UCHUNGUZI SACCOS YA MADIBIRA-MBARALI NDANI YA SIKU 14

Naibu Waziri wa Wizara ya Kilimo, Mhe Mary Mwanjelwa akisisitiza jambo wakati akizungumza na Viongozi mbalimbali wa Mkoa na kamati ya uli...