Jumanne, 5 Desemba 2017

MHE MWANJELWA AWATOA HOFU WAKULIMA WA NYANYA MKOANI IRINGA

Naibu Waziri wa Wizara ya Kilimo Mhe Mary Mwanjelwa akisisitiza jambo wakati akizungumza na Uongozi wa Mkoa wa Iringa mara baada ya kusomewa taarifa ya maendeleo ya sekta ya kilimo Mkoani humo na Mkuu wa Mkoa wa Iringa Mhe Amina Masenza, Jana Disemba 4, 2017. 
Naibu Waziri wa Wizara ya Kilimo Mhe Mary Mwanjelwa akisalimiana na Meneja uzalishaji wa kiwanda cha kutengeneza Achali ya nyanya/TOMATO SOURCE cha Chai Bora Ltd/Dabaga Ndg Sanjay Rai kilichopo Kijiji cha Ikokoto Kata ya Ilula Wilayani Kilolo Mkoa wa Iringa alipotembelea kiwanda hicho sambamba na kufanya mkutano na wawakilishi wa wakulima. Mwingine ni Mkuu wa Wilaya ya Kilolo Mhe Asia Abdalah Juma, Jana Disemba 4, 2017.
Naibu Waziri wa Wizara ya Kilimo Mhe Mary Mwanjelwa akisalimiana na Meneja uzalishaji wa kiwanda cha kutengeneza Achali ya nyanya/TOMATO SOURCE cha Chai Bora Ltd/Dabaga Ndg Sanjay Rai kilichopo Kijiji cha Ikokoto Kata ya Ilula Wilayani Kilolo Mkoa wa Iringa alipotembelea kiwanda hicho sambamba na kufanya mkutano na wawakilishi wa wakulima. Jana Disemba 4, 2017.
Mkuu Wa Mkoa wa Iringa Mhe Amina Masenza akisoma taarifa ya hali ya sekta ya chakula katika mkoa huo mbele ya mgeni rasmi Naibu Waziri Wa Kilimo Mhe Mary Mwanjelwa . Jana Disemba 4, 2017.
Picha ya pamoja Naibu Waziri wa kilimo Mhe Mary Mwanjelwa (Wa tatu kulia) Mkuu Wa Mkoa wa Iringa Mhe Amina Masenza (Wa pili kulia) Katibu Tawala wa Mkoa wa Iringa Bi Wamoja Ayubu, Mkuu wa Wilaya ya Mufindi Mhe David Willium Jamhuri na wataalamu wa Kilimo Mkoa wa Iringa. Jana Disemba 4, 2017.

Na Mwandishi Wetu

Wakulima wa zao la Nyanya wametakiwa kuondoa wasiwasi wa kufikiri kupunguza kasi ya kilimo kutokana na viwanda vya nyanya kununua tani chache za nyanya tofauti na uzalishaji.

Naibu Waziri wa Wizara ya Kilimo Mhe Mary Mwanjelwa ameyasema hayo wakati akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Ikokoto kilichopo Kata ya Ilula Wilayani Kilolo Mkoa wa Iringa mara baada ya kutembelea kiwanda cha kutengeneza Achali ya nyanya/TOMATO SOURCE cha Chai Bora Ltd/Dabaga.

Alisema kuwa kuanzishwa kwa kiwanda hicho kipya ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za Mhe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli kuelekea Tanzania ya viwanda hivyo kitawanufaisha wakulima hao wa nyanya ambao soko lao linasuasua.

Alisema kuwa kiwanda hicho ambacho kilianza uzalishaji Octoba mwaka huu kwa kuchakata nyanya kwa Tani 16 mpaka Tani 20 kwa masaa 8 pindi kitakapokamilika na kuanza kufanya kazi kwa masaa 24 kitaongeza uzalishaji hivyo wakulima wa nyanya watapata soko la uhakika.

Mhe Mwanjelwa aliwahakikishia wakulima hao kuwa serikali itaendelea kuweka mazingira mazuri kwa wakulima nchini ili waweze kunufaika na kilimo kwani inafahamika kuwa asilimia zaidi ya 75 ya watanzania wanajihusisha na kilimo.

Aliwasihi wakulima hao Kulima nyanya kwa awamu tofauti na hivi sasa ambapo wanalima kwa msimu kwani kufanya hivyo itawasaidia kupata kipato wakati wote huku viwanda vikiwasaidia kununua mazao hayo wakati wote kwani kwa sasa viwanda hivyo vinafungwa kutokana na msimu wa nyanya kumalizika.

Aidha amewasihi wamiliki wa kiwanda cha kutengeneza Achali ya nyanya/TOMATO SOURCE cha Chai Bora Ltd/Dabaga kuwa na bei rafiki kwa wakulima kwani kufanya hivyo itakuwa ni msingi wa kuinua kipato cha mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla wake.

Sambamba na hayo pia alisisitiza Uongozi wa Vijiji na Kata kusaidiana na wataalamu wa ushirika na maendeleo ya jamii kuendelea kuhamasisha wakulima kujiunga katika vikundi vya Vyama vya ushirika ili waweze kupata mikopo ya fedha, pembejeo na kupata mafunzo ya ugani na kuanzisha viwanda vidogo vya kusindika mazao wanayozalisha.

Wakati huo huo Naibu Waziri huyo wa kilimo Mhe Mary Mwanjelwa amesifu juhudi za uongozi wa Mkoa wa Iringa unaoongozwa na Mkuu wa Mkoa huo Mhe Amina Masenza kwa kazi kubwa anayoifanya ikiwa ni pamoja na kuanzisha kampeni ijulikanayo kama “Mkoa Wetu, Viwanda Vyetu” yenye lengo la kuwezesha wakulima kupata masoko ya uhakika kwa mazao wanayozalisha.

Aidha, ameelekeza kuchukuliwa hatua kali za kisheria kwa wafanyabiashara wote watakaobainika kukiuka bei elekezi ya mbolea katika Mkoa wa Iringa na Taifa kwa ujumla.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

NAIBU WAZIRI WA KILIMO MHE MWANJELWA AMUAGIZA MRAJIS KUFANYA UCHUNGUZI SACCOS YA MADIBIRA-MBARALI NDANI YA SIKU 14

Naibu Waziri wa Wizara ya Kilimo, Mhe Mary Mwanjelwa akisisitiza jambo wakati akizungumza na Viongozi mbalimbali wa Mkoa na kamati ya uli...