Alhamisi, 18 Desemba 2014

KAGERA KUJIVUNIA UWANJA WA NDEGE WA KISASA


Na Saidi Mkabakuli, Kagera
Mkoa wa Kagera na maeneo ya jirani wataanza kujivunia uwanja wa ndege wa kisasa kufuatia kukamilika kwa Kiwanja cha Ndege cha Bukoba.
Akizungumza na Wakaguzi wa Miradi ya Maendeleo toka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango, Meneja Mradi wa Upanuzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kagera, Mhandisi Suleiman Athuman, amesema kwamba maendeleo ya ujenzi wa jengo la abiria la kiwanja hicho upo kwenye hali nzuri na mkandarasi atabidhi kazi hiyo mapema mwakani.
“Katika mwaka wa fedha wa 2013/14 kazi zilizopangwa ni ukarabati na upanuzi wa miundombinu ya kiwanja, ikijumuisha barabara ya kuruka na kutua ndege, maegesho ya ndege, barabara ya kiungio, kwa sasa ujenzi unaendelea vizuri na Mkandarasi atatukabidhi kazi mapema mwakani,” alisema Mhandisi Athuman.
Akitoa taarifa ya maendeleo ya ujenzi wa Kiwanja cha Bukoba, Mhandisi Mshauri wa ujenzi wa kiwanja hiko, Mhandisi Pius Gobolo amesema kuwa kazi za usimikaji wa mfumo wa taa za kuongozea ndege, ujenzi wa jengo jipya la abiria na uzio wa usalama zimeshakamilika kwa asilimia 80.
“Kama unavyojionea, sehemu kubwa ya kazi imekamilika, kwa makadirio ni zaidi ya asilimia 80 ya ujenzi wa kiwanja hiki imeshakamilika,” aliongeza   Mhandisi Gobolo.
Kwa mujibu wa mpangokazi wa ujenzi wa kiwanja hicho hadi kufikia mwezi Juni 2014, hatua iliyofikiwa ni pamoja na kukamilika kwa ukarabati wa barabara ya kuruka na kutua ndege, barabara ya kiungio na maegesho ya ndege kwa kiwango cha lami; na ujenzi wa jingo jipya la abiria kufikia hatua ya usimikaji wa paa na mifumo ya maji safi, maji taka na umeme; na kuendelea kwa ujenzi wa jengo la abiria na kituo cha umeme.
Naye, Kiongozi wa Timu ya Ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango, Bibi Florence Mwanri amesema kuwa Serikali imeazimia kuendelea kuboresha miundombinu ya viwanja vya ndege hususan miradi iliyoibuliwa katika Programu ya Matokeo Makubwa Sasa.
“Kwa mujibu Programu ya Matokeo Makubwa Sasa, serikali kupitia Mamlaka ya Viwanja vya Ndege nchini ipo kwenye mkakati wa kuuendeleza viwanja vya ndege vyote ili viwe na kiwango kizuri kwa watumiaji wa viwanja hivyo,” alisema Bibi Mwanri.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

NAIBU WAZIRI WA KILIMO MHE MWANJELWA AMUAGIZA MRAJIS KUFANYA UCHUNGUZI SACCOS YA MADIBIRA-MBARALI NDANI YA SIKU 14

Naibu Waziri wa Wizara ya Kilimo, Mhe Mary Mwanjelwa akisisitiza jambo wakati akizungumza na Viongozi mbalimbali wa Mkoa na kamati ya uli...