KITUO cha afya cha Aga khan, tawi la Mbeya, kimetoa msaada wa vifaa tiba katika Hospitali na vituo vya afya katika Halmashauri
4 za Mkoa wa Mbeya vyenye thamani ya zaidi ya shilingi Milioni 300.
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Abbas Kandoro kwa niaba ya
Halmashauri husika, alipokea msaada huo katika ukumbi wa Mkapa
uliopo jijini Mbeya.
Mratibu wa Mradi wa tuunganishe
mkono pamoja(JHI) Mkoa wa Mbeya, Abel Kide, ambaye pia ni Meneja wa Hospitali
ya Aga Khan alisema Halmashauri zilizonufaika na mradi huo ni Jiji la Mbeya, Kyela, Mbozi na Momba.
Alizitaja Hospitali na
zahanati zinazopatiwa vifaa hivyo kuwa ni Zahanati ya Ngana na Hospitali ya
Wilaya ya Kyela(Kyela), Zahanati ya Iyunga na kituo cha Afya Kiwanja Mpaka(Mbeya
jiji), Hospitali ya Wilaya ya Mbozi(Vwawa)na Zahanati ya Ivuna iliyopo wilayani
Momba.
Alivitaja vifaa hivyo kuwa ni
Vitanda vya kujifungulia wajawazito, vitanda vya wagonjwa wa kawaida, Mashine
za kuchemshia vifaa vya hospitalini, Mashine ya kumpa joto mtoto aliyetoka
kuzaliwa, Mashine ya Ultra Sound,Mashine ya kumtolea uchafu mtoto
mchanga,mashine za kupima uzito, joto, urefu na Presha na kwamba vyote jumla
vinagharimu zaidi ya shilingi Milioni 300.
Lengo la msaada huo ni kuboresha afya ya mama mjamzito, mtoto mchanga na mtoto
aliye chini ya miaka mitano ikiwa ni pamoja na kusogeza huduma za afya karibu na wananchi hususani kuokoa vifo
vinavyotokea wakati wa kujifungua.
Mkuu wa Mkoa wa
Mbeya, Abbasi Kandoro alipongeza Hospitali ya Aga Khan kwa Msaada waliotoa
katika Halmashauri hizo na kuziomba taasisi zingine kuungana na Serikali katika
mpango wa kuhakikisha vifo vya Wanawake wajawazito, watoto wachanga na
walio chini ya umri wa miaka mitano vinapungua.
Aliongeza kuwa ili kukomesha
kabisa vifo hivyo, Halmashauri zitenge bajeti za kununua mfumo wa huduma
tembezi(Mobile clinic) ili ziweze kufika hata maeneo ambayo hakuna huduma ya
afya kwa kuwasogezea wananchi huduma ili waweze kupata msaada wa matibabu
wakati wowote.
Sambamba na kupokea msaada huo
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya alizindua Mpango wa utekelezaji wa kupunguza kasi ya vifo
vitokanavyo na matatizo ya uzazi, watoto na watoto waliochini ya umri wa miaka
mitano.
Kandoro aliongeza kuwa mkakati
huo ni maagizo ya Raisi wakati wa uzinduzi wa kitabu cha Mkakati wa kitaifa
uliofanyika Mei 15 Mwaka huu ambapo aliagiza Kila Mkuu wa Mkoa kuutafakari
mkakati huo kulingana na mazingira wanakotoka.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni