Alhamisi, 10 Aprili 2014

KIMBUNGA CHAHARIBU NYUMBA 104, MSAADA WAHITAJIKA HARAKA


Juu na chini ni Kamanda wa UVCCM wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya, Ibrahimu Ismail(Mwakabwanga),(Kulia) akimkabidhi bati 96, Mwenyekiti wa Kijiji cha Manienga, Cosmas kasoli, baada ya kijiji hicho kuezuliwa na kimbunga nyumba 104 wilayani humo

  Kamanda wa UVCCM Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya, Ibrahimu Ismail(Mwakabwanga), akiwapo pole baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Manienga wilayani humo, baada ya kukumbwa na kimbunga ambacho kiliezua nyumba 104 na kuziacha familia 86 zikiwa hazina makazi, ambapo kamanda huyo alitoa msaada ya bati 96.

WAZAWA wa wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya, wameombwa kujitokeza kusaidia familia 86, zilizokumbwa na kimbunga eneo la Manienga wilayani humo na kuezua jumla ya nyumba 104.

Tukio hilo lililoleta madhara makubwa na kuhitaji msaada wa kiutu, lilitokea April 7, mwaka huu.

Akizungumza na wananchi wa eneo hilo, Mwenyekiti wa Vijana wa UVCCM, wilayani humo, Amin Kimulungu, aliviomba vyombo vya habari kufikisha taarifa ya tatizo hilo kwa wazawa wote wa Mbarali waliopo ndani na nje ya wilaya hiyo, kujitokeza kusaidia familia zilizoathirika.

Kimulungu aliyasema hayo alipoongozana na Kamanda wa UVCCM wilayani humo, Ibrahimu Ismail(Mwakabwanga), alipowatembelea wananachi hao na kutoa bati 96 kwa uongozi wa Kijiji hicho cha Manienga.

Akikabidhi bati hizo, Ibrahimu, alisema kuwa, aliguswa na tatizo hilo na alionya kuwa msaada wake hauendani na masuala ya kisiasa.

‘’Hapa siyo mahala pa kupiga siasa, naomba mpokee bati hizi 96 na uongozi wa Kijiji utajua uzigawanye kwa mtiririko upi’’ alisema Ibrahimu Ismail(Mwakabwanga), ambaye pia ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Usangu Logistics.

Afisa Mtendaji wa Kijiji hicho Modestus Mjimu, alito taarifa kuwa, kimbunga hicho licha ya kusababisha hasara kubwa ya mazingira, kiliezua nyumba 104, makazi 86 na nyumba za taasisi zikiwa 7.

Naye Mwenyekiti wa Kijiji hicho, Cosmas Kasoli, alisema nyumba 34 zilikuwa za nyasi, madhara ya kibinadamu pia yalijitokeza ambapo wananchi 9 walijeruhiwa.

‘’Majeruhi walikuwa tisa ambao wote walipelekwa hospitali ya wilaya ya Mbarali(Rujewa), wanaume walikuwa wawili na wanawake saba na tathimini yote tumemkabidhi Mkuu wa wilaya na kamati yake ya Ulinzi na usalama ’’ alisema Kasoli.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

NAIBU WAZIRI WA KILIMO MHE MWANJELWA AMUAGIZA MRAJIS KUFANYA UCHUNGUZI SACCOS YA MADIBIRA-MBARALI NDANI YA SIKU 14

Naibu Waziri wa Wizara ya Kilimo, Mhe Mary Mwanjelwa akisisitiza jambo wakati akizungumza na Viongozi mbalimbali wa Mkoa na kamati ya uli...