Wananchi wakisikitika kutokana na majibu ya wakubwa....
Baadhi ya wazazi wakiwa wanaangalia majina ya watoto wao, katika ubao wa matangazo ya shule ya sekondari Usongwe.
BAADHI ya
wazazi wa kata ya Utengule Usongwe, wilaya ya Mbeya Vijijini, wametibua mpango
wa kuchangishwa fedha harakaharaka, ili watoto wao waanze kidato cha kwanza
kupitia elimu ya watu wazima.
Mpango huo
ulikuwa ukiratibiwa na kitengo cha Elimu ya watu wazima mkoa wa Mbeya chini ya
Mkufunzi mkazi wa taasisi hiyo Danstan Msamada, kupitia shule ya Sekondari
Usongwe iliyopo eneo la Mbalizi.
Baada ya
baadhi ya wananchi kushtukia suala hilo, walimpigia simu Diwani wa kata hiyo,
Elia Mkono(Chadema), ambaye alianza kufuatili kisha kuitisha mkutano wa wazazi,
walimu na Mkufunzi wa taassi hiyo.
Katika kikao
hicho kilichofanyika leo katika ukumbi wa shule ya Sekondari Usongwe, wananchi
waliuliza maswali 22, ambayo wakati wa kujibiwa, zilitokea zomeazomea kwa
kiongozi wa taasisi hiyo na baadhi ya walimu.
Mwananchi Harun
Abdalah, aliuliza kuwa iweje baadhi ya watoto wenye wastani wa alama C,
wachukuliwe kwenda taasisi ambayo inaendesha elimu katika mfumo usio rasmi?
Benard
Tawete, alisema kuwa huo ni mpango wa biashara (dili), kati ya Mkuu wa shule ya
Usongwe na taasisi hiyo ili kujipatia fedha kutoka kwa wazazi kwasababu iweje,
fomu wazazi wachukue katika shule ya Usongwe kisha wanafunzi wakasome Taasisi
iliyopo mbali na shule hiyo?
Wananchi wengi
waliulza maswali ambayo, yakawa mwiba kwa baadhi ya viongozi na kushindwa
kuyajibu kwa ufasaha kisha kuzomewa.
Afisa
Mtendaji wa kata hiyo, Godwin Kaunda, aliamua kujitoa katika zomea zomea hiyo,
kwa kuweka wazi kuwa ofisi yake baada ya kulipata jambo hilo aliwakataza wahusika
kubandika majina hayo kwenye ofisi yake kabla wananchi hawajaelimishwa, lakini
alishangaa kuona kuambiwa majina hayo yamebandikwa siku chache shuleni na
wazazi kuanza kuchukua fomu.
Ukweli huo
ulimwondoa katika doa la kuwa mmoja wa washiriki wa jambo hilo ambalo wananchi
walisema kuwa awali walilaghaiwa kuwa watoto wao walikuwa wamefaulu kwenda huko
na kutakiwa kulipa karo ya Tsh.200,000/=, na michango mingine zikiwemo fedha za
madawati Tsh.15,000/=, vitambulisho Tsh. 5,000/=, ulinzi Tsh. 5,000 na fomu
Tsh.5,000/=.
Diwani wa
kata hiyo, Elia Mkono ambaye pia ni mwenyekiti wa Kijiji cha Mbalizi,
aliwaambia wananchi kuwa yeye hawezi kuwaambia wananchi kuwa huko wanakotakiwa
wawapeleke watoto wao ni kuzuri au kubaya.
“Jaribuni
kupima wenyewe, kwasababu hata mimi nimepata takwimu za wanafunzi ambao majina
yao yameenda huko Taasisi baada ya kupambana na kulazimisha kupata taarifa
zaidi!’’ alisema Mkono na kuanza kufafanua zaidi.
Alisema mpaka
sasa, wanafunzi waliofaulu na kuchaguliwa kujiunga na shule mbili za serikali
zilizopo katika kata yake katika mfumo maalum ni 601.
Lakini alisema
kuwa wakati shule hizo mbili zina idadi ya wanafunzi 601, Taasisi ya elimu ya
watu wazima kwa shule moja, imechagua majina ya wanafunzi 493, hali ambayo
alisema wazazi wenyewe wachanganue kama wakiwapeleka watoto wao huko watapata
elimu bora au la.
Akijibu maswali
zaidi, Mkufunzi mkazi wa elimu ya watu wazima huku mara kadhaa akiomba radhi,
alisema kuwa taasisi hiyo ni ya serikali na majina hayo ameyatoa serikalini kwa
wanafunzi ambao wana wastani wa alama D.
‘’Kama
mnaona mfumo huu hamna imani nao msiwalete wanafunzi lakini kwa wale walioelewa
wawalete wanafunzi ambao watafundishwa na walimu kutoka hapa shule ya Sekondari
Usongwe, wakitoka kufundisha wanafunzi waliopo kwenye mfumo maalum’’ alisema
Msamada.
Baadhi ya
walimu wa shule ya Usongwe waliozungumza na Mwandishi wa habari hizi shuleni
hapo kwa makubaliano ya kutoandika majina yao, walisema wanashindwa kwenda
kufundisha vema katika taasisi ya elimu ya watu wazima kutokana na kupewa ujira
mdogo.
Waliutaja ujira
huo wanaolipwa kwa mwezi kuwa ni Tsh.20,000/= wakati hata wasipokwenda huko
hakuna sheria inayowabana kwasababu mikataba yao ya kazi haielezi kuwa watakuwa
na kazi nyingine ya kufundisha au kujitolea katika taasisi hiyo.
Kwa takwimu
zilizopatikana, zinaonesha kuwa, katika kata hiyo, kuna shule za msingi 13
ambazo zimetoa wanafunzi wa elimu katika mfumo rasmi kama ifatavyo na wanafunzi
kwenye mabano.
Shule ya
Msingi, Mlima reli(87), Jitegemee(60), Mapambano(35), Mtakuja(100),
Mkombozi(117), Mbalizi Moja(96), Onicar(37), Utengule(41), Itimba(5),
Idugumbi(6), Iwala(10), Igunga(6) na Iwanga(1).
Taasisi ya
elimu ya watu wazima imejinyakulia Mlimareli(47), Jitegemee(124),
Mapambano(35), Mtakuja(54), Mkombozi(46), Mbalizi Moja(31), Iwanga(32),
Itimba(30), Igunga(28), Iwala(23), Utengule(18) na Idugumbi(25).
Mkutano huo
uliisha huku baadhi ya viongozi akiwemo WEO, kuondoka na makubaliano yalikuwa
hakuna ulazima wa kumlazimisha mzazi kuchukua fomu ili wanafunzi hao waende
kusoma kwenye mfumo huo ambao siyo rasmi na ziachwe propaganda kuwa watoto hao
wamefaulu kwenda huko.
Chanzo; kalulunga.com
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni