Jumatatu, 13 Januari 2014

TIBAIJUKA APONGEZWA KUTATUA MGOGORO WA WANANCHI NA MWEKEZAJI KAPUNGA MBARALI

 Kulia ni Mathayo Mwangomo, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya.

 Jofrey Mwangulumbi(kushoto), MNEC wa wilaya ya Mbarali(CCM), akizungumza mbele ya wanahabari Jijini Mbeya.

WANANCHI wa wilaya ya Mbarali, wamempongeza Waziri wa Ardhi, Nyumba na maendeleo ya makazi, Prof; Anna Tibaijuka kwa kutatua mgogoro uliokuwepo baina ya wananchi na Mwekezaji wa shamba la Kapunga tangu mwaka 2006. 

Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Mbarali, Mathayo Mwangomo na Mjumbe wa Halmashauri kuu ya Taifa(NEC), Jofrey Mwangulumbi, walitoa pongezi hizo leo tarehe 10/01/2014, walipokutana na waandishi wa habari Jijini Mbeya na kwamba Waziri Tibaijuka hana ndimi mbili za kubadili kauli zake na wala siyo mbabaishaji. 

Walisema maamuzi aliyoyatoa mwanzoni mwa wiki wilayani humo ya kumwamuru mwekezaji kuachia hekali 1870 kwa ajili ya wananchi ni sahihi na baada ya mwekezaji kufanya hivyo watafanya utaratibu wa kuwagawia wananchi. 

Mwangomo alisema, wakati wa ubinafsishaji, hati iliandaliwa kimakosa, kitendo kilichokuwa kikilalamikiwa na wananchi kwa muda mrefu ambapo eneo la kijiji liliingizwa ndani ya eneo la mwekezaji jambo ambalo Waziri Tibaijuka ameliona na kulitolea kauli ambayo wanaamini kuwa utekelezaji wake hautachukua muda mrefu. 

‘’Wamekuja viongozi mbalimbali wakiwemo mawaziri waliotangulia, Makamishina wa Ardhi na kushindwa kulitolea maamuzi suala hilo, lakini mwaka 2012 tulipompelekea Waziri huyu Dodoma, alisema atafuatilia ndipo alisema anakuja na akaja na kukutana na serikali ya kijiji na Mwekezaji’’Alisema Mwangomo. 

Alisema baada ya kubaini ukweli wa mgogoro huo, Waziri alimwamuru Mwekezaji arejeshe hekali hizo 1870 kwa hiari yake na kama hawezi kufanya hivyo, atamshauri Rais Jakaya Kikwete, afute hati ya shamba hilo lenye ukumbwa wa hekali zaidi ya 7,000. 

‘’Tutatoa elimu kwa wananchi wote kujua thamani ya ardhi ili wengine wasije kutelekeza na baadhi kuuza baada ya kugawiwa mchakato ukikamilika na kati ya hizo hekta 1870, kuna hekali zingine ni makazi na baadhi ni maeneo ya mashamba ya kilimo’’alisema Mwenyekiti huyo. 

Naye (MNEC)Jofrey Mwangulumbi, alisema shamba hilo linaweza kununuliwa hata na wawekezaji wa wilaya ya Mbarali wakiwemo wakulima wadogowadogo wa zao la Mpunga ambao wana vyama vyao vya ushirika.

 “Mwekezaji anakodisha mashamba baada ya kushindwa kuliendesha kinyume na mkataba, lakini pamoja na tatizo hilo la msingi, kuna mambo mawili makubwa ambayo yanajikita kwenye ukabaila ambao ni kukataa kunyanyaswa wananchi bali hatukatazi makubaliano’’ alisema Mwangulumbi. 

Alisema kwa sasa serikali inaendelea kujinyumbua na kwamba hatua iliyofikiwa ya kumtaka mwekezaji kurejesha hekali hizo, ni hatua ya ushindi katika mahusiano kati ya mwekezaji na wananchi.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

NAIBU WAZIRI WA KILIMO MHE MWANJELWA AMUAGIZA MRAJIS KUFANYA UCHUNGUZI SACCOS YA MADIBIRA-MBARALI NDANI YA SIKU 14

Naibu Waziri wa Wizara ya Kilimo, Mhe Mary Mwanjelwa akisisitiza jambo wakati akizungumza na Viongozi mbalimbali wa Mkoa na kamati ya uli...