Jumapili, 29 Desemba 2013

VYOO VYENYE USIRI VIJIJINI NI TAABU KWELIKWELI



ELIMU ya matumizi sahihi ya vyoo, mashimo ya taka na vichanja, inahitajika zaidi Vijijini ili kupunguza magonjwa ya milipuko.
 
 
Hayo yamebainika katika warsha ya wadau wa mpango wa usafi wa Mazingira(WASH), kutoka wilaya za Mbeya na Mbarali, iliyofanyika eneo la Mbalizi ukumbi wa Tughimbe, uliopo wilaya ya Mbeya Vijijini mkoani hapa.
 
 
Wadau hao walitembelea katika kata za Ihahi iliyopo wilaya ya Mbarali na kata ya Mshewe iliyopo wilaya ya Mbarali, na kujionea vyoo vya baadhi ya wananchi ambapo walikuta baadhi ya kaya hazina vyoo.
 
 
Katibu tawala msaidizi-Maji, ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Mbeya Mhandisi, Fredius Magige, alisema maafisa afya kwa kushirikiana na watendaji wa vijiji na kata, wanatakiwa kupeleka kikamilifu elimu hiyo kwa wananchi mara kwa mara ikiwa ni pamoja na ufuatiliaji.
 
 
‘’Kwa kuwa imebainika kuwa wahudumu wa afya ya msingi ya jamii(WAV) ni watu muhimu, ni vema wakatumika vizuri lakini kama wanajitolea bila kulipwa hawataweza kufanya kazi zao vizuri’’ alisema Mhandisi, Magige.
 
 
Akiwasilisha taarifa ya utafiti wa kundi la kwanza uliofanyika katika kijiji cha Mjele kata ya Mshewe, Afisa Afya wilaya ya Mbarali, Emedan Mgode, alisema;‘’Kijiji kina kaya 418, katika vyoo, maji na sabuni ya kunawia hakuna na kaya 117 zina matarajio ya kuwa na vyoo bora na kaya 38 hazina vyoo kabisa’’ alisema Mgode.
 
 
Alisema walitembelea pia shule ya Msingi Itega yenye wanafunzi 334, na  hali halisi ya miundombinu ya shule hiyo siyo mizuri na uwiano wa matundu ya vyoo kwa wasichana ni 1 ya 60 na wavulana ni 1 ya 153.
 
 
‘’Vyoo hivyo havina sakafu inayosafishika wala havina falagha, pia vina harufu na havina maji ya kunawa kutokana na tatizo la maji katika eneo hilo na vyoo vya walimu pia havina falagha wala maji ya kunawa mikono’’ alisema.
 
 
Alibainisha changamoto inayokikumba kijiji hicho kuwa ni tatizo la maji ambayo yanapatikana katika mto songwe umbali wa kilometa 10 kutoka kijijini hapo, hivyo suala la kutumia maji katika hatua nne muhimu za kunawa mikono ambazo ni wakati wa kutoka chooni, kabla na baada ya kula na baada ya kumuhudumia mgonjwa na wakakati wa kumuhudumia mtoto inakuwa vigumu.
 
 
Alitoa ushauri kuwa watu au jamii ihamasishwe juu ya uvunaji wa maji ya mvua katika kaya na taasisi na jamii iendelee kuhamasishwa kujenga vyoo vyenye faragha au usiri vilivyoezekwa na kuwekewa milango.
 
 
Naye Afisa elimu ufundi wilaya ya Mbeya, Florence Mbwele, aliwasilisha taarifa ya ziara ya kata ya Ihahi, akisema kuwa katika ziara yao walijionea hali mbaya ya vyoo hasa kwa jamii za wafugaji.
 
 
‘’Changamoto zilizochangia uchelewaji wa utekelezaji wa mpango wa WASH, ni pamoja na uhaba wa maji, vyoo havina viwango, jamii ya wafugaji haijawafikiwa na elimu ya matumizi ya vyoo na watendaji wana uhaba wa vitendea kazi’’ alisema Florence.
 
 
Alisema hali halisi ni kwamba kuna mwitikio wa wastani kuhusu masuala ya afya na usafi wa mazingira ikiwemo maofisini tofauti na hali mbaya iliyopo kwa jamii za wafugaji.
 
 
‘’Kuhusu elimu ya matumizi ya kibuyu chilizi(maji ya kunawa yanayotiririka) jamii imeipokea lakini imeeleweka tofauti, ambapo wanatoboa garoni kwa chini hivyo wakiweka maji yote yanaisha kabla ya kutumia’’ alisema mwasilishaji huyo.
 
 
Alisema kunahitajika nguvu ya ziada katika jamii za wafugaji kwasababu katika ziara hiyo walikosa hata mtu wa kutoa ushirikiano kupata taarifa na walipofika kwenye nyumba moja, mwenyeji alipoona gari aliingia ndani na kujifungia.
 
 
Wakichangia katika warsha hiyo, Afisa afya msaidizi wa kata ya Ihahi, Khatibu Kilumbu, alisema kuwa katika kata yake wamejiwekea mikakati ya kuendelea kutoa elimu kwa wananchi, kufanya mashindano ya usafi na kwamba ni wakati muhafaka kwa viongozi wote kuwa na mipango na tathimini shirikishi kuhusu suala la usafi wa mazingira.
 
 
Afisa afya mkoa wa Mbeya, Salehe Mwango, alisema kuwa katika kijiji cha Mjele kuna udhaifu wa mashimo ya takataka, ambapo mashimo yapo lakini hayatumiki hivyo aliwataka viongozi wa eneo hilo kufanyia kazi jambo hilo.
 
 
Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Mjele, Evarist, alisema jamii ina elimu ya masuaa ya usafi lakini haitaki kuitikia na katika suala la ujenzi wa vyoo vyenye kuta za nyasi katika eneo lake alisema ni kutokana na kijiji hicho kutokuwa na maji hivyo wanashindwa kufyatua tofali.
 
 
Kuhusu tatizo la upatikanaji wa takwimu sahihi kutoka kwenye kata na vijiji, Afisa Afya wilaya ya Mbeya, Emmanuel Mwaigugu, alisema kuwa ni kutokana na uhaba wa watumishi wa sekta ya afya akitolea mfano katika wilaya yake kuwa katika kata za Ilungu, Ilembo na Iwiji hakuna watendaji wa idara yake.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

NAIBU WAZIRI WA KILIMO MHE MWANJELWA AMUAGIZA MRAJIS KUFANYA UCHUNGUZI SACCOS YA MADIBIRA-MBARALI NDANI YA SIKU 14

Naibu Waziri wa Wizara ya Kilimo, Mhe Mary Mwanjelwa akisisitiza jambo wakati akizungumza na Viongozi mbalimbali wa Mkoa na kamati ya uli...