Jumapili, 1 Februari 2015

CHAMA CHA WALIMU TANZANIA MKOA WA MBEYA



 Katibu wa chama cha Walimu Mkoa wa Mbeya (CWT)  Kasuku Bilago akitoa taarifa ya Mkoa
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI


Ndugu  Waandishi wa habari,
 CWT mkoa wa Mbeya kinawasilisha hoja mbalimbali za walimu kwa serikali yao kama ifuatavyo:- 

1.     MADAI YA WALIMU YA MUDA MREFU
Walimu wa mkoa wa Mbeya wana madai yao serikalini ambayo yalihakikiwa Septemba 2013. Baada ya uhakiki huo uliofanyika nchi nzima kiasi cha madai ya mkoa wa Mbeya yaliyokubaliwa na serikali yalikuwa kiasi cha zaidi ya sh. 4.6 Bilioni. Serikali haijaonyesha nia thabiti ya kumaliza madai haya kwa walimu wa mkoa wa Mbeya  kwani walimu bado wanaidai serikali kwa mchanganuo ufuatao:-


JUMLA YA MADENI YA WALIMU MKOA WA MBEYA MPAKA DISEMBA 2014
WILAYA
KIASI CHA DENI
MBEYA JIJI
   1,220,620,843.00
MBEYA VIJIJINI
       154,436,695.07
RUNGWE
       220,000,000.00
KYELA
       165,723,474.00
MBOZI/MOMBA
       998,554,540.83
ILEJE
       164,418,518.00
CHUNYA
       463,871,400.24
MBARALI
       230,666,235.66
JUMLA KUU
   3,618,291,706.80

Kwa hali hiyo CWT Mkoa wa Mbeya kinaitaka serikali kulipa madai haya kabla au ifikapo tarehe 30/4/2015 ili kurudisha ari ya ufundishaji kwa walimu. Kama serikali haitalipa madai haya Chama cha Walimu kitawaelekeza walimu kuchukua maamuzi magumu kwa serikali mwaka huu wa 2015. Aidha, ieleweke kuwa madai haya ni ya muda mrefu kuanzia 2007 hadi 2014 jambo ambalo CWT hakiwezi kuvumilia kuendelea kuona serikali inavunja Sheria na Kanuni za utumishi wa umma. Madai haya yalikubalika kwenye Kamati ya uhakiki. 

Aidha, kuna baadhi ya watendaji wa serikali ambao wamekuwa na upotoshaji mkubwa juu ya madai ya walimu kwamba yamelipwa yote au yamebaki kidogo sana kama milioni 200 tu. CWT inasikitishwa sana na kauli kama hizo kwani ni za uchochezi na kuwakatisha tamaa walimu. Mfano halisi ni madai yaliyohakikiwa mkoa wa Mbeya ambayo hayajalipwa hadi sasa ni zaidi ya 3.6 Bilioni. 


2.     MALIPO YA LIKIZO KUTOLIPWA
Tangu Desemba 2013 serikali ilibadili utaratubu wa kulipa walimu nauli za likizo kabla ya kwenda likizo zao. Hivyo, walimu wamekuwa wakienda likizo bila kulipwa stahili zao. Likizo zifuatazo walimu hawajalipwa; Desemba 2013, Juni 2014 na Desemba 2014 jambo linalokwenda kinyume na Kanuni za Utumishi wa Umma, 2003; Kifungu cha 97 (5) kinachomtaka mwajiri kulipa nauli ya likizo kwa kila mtum ishi wa umma mara moja katika kipindi cha miaka miwili.


3.     KUTOPANDA KWA MADARAJA YA WALIMU KWA WAKATI
Kwa kawaida walimu wanatakiwa kupanda madaraja yao kila baada ya miaka 3 kama hakuna tatizo la kiutumishi. Utaratibu huu umekiukwa na serikali kwa madai ya ukomo wa bajeti (ceiling) jambo linaloathiri maslahi na haki ya walimu ya kupanda daraja. CWT kinaitaka serikali kuwapandisha madaraja walimu wote wa mkoa wa Mbeya waliofikia muda wa kupanda ili kuwapa motisha wa kuipenda kazi yao. 


4.     KUUNGA MKONO TAMKO LA BARAZ LA CWT TAIFA
Chama cha Walimu Tanzania mkoa wa Mbeya kinapenda kuunga mkono maazimio manne ya Baraza la CWT taifa lililofanyika mjini Morogoro katika ukumbi wa Midland Hotel kuanzia tarehe 21-23 Januari, 2015. Maazimio haya yanataka uwajibikaji wa dhati wa Serikali ikiwa ndio mwajiri Mkuu wa walimu wote wa shule na Taasisi za Umma kama ifuatavyo:- 

(i)                Utekelezaji wa Waraka wa maendeleo ya utumishi Na.1 wa 2014 juu ya miundo ya utumishi wa kada za ualimu chini ya WEMU Kumb. Na.AC.87/260/01/G/9.15/7 wa 2014 unaohusisha miundo ya watumishi wa kada za walimu walio chini ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi uliopanua wigo wa ngazi za mishahara ya walimu na kuagiza utekelezaji wake kuanza tarehe 01 Julai, 2014. 

AZIMIO:       
Walimu wote waliogota muda mrefu kwenye ngazi zilizofunguliwa wapandishwe vyeo kuanzia tarehe 01 Julai, 2014 na kulipwa malimbikizo ya mishahara hiyo kabla au ifikapo tarehe 30 Aprili, 2015.


(ii)               Walimu/Wanachama wa CWT wamekopwa na Serikali stahili zao kwa muda mrefu.  Hadi mwishoni mwa Desemba, 2014 walimu wanaidai Serikali jumla ya T.sh 16 Bilioni. Kwa mujibu wa uhakiki uliofanyika Desemba, 2013.
AZIMIO:
Baraza linaitaka Serikali kuwa imelipa madeni yote ya walimu kabla au ifikapo tarehe 30 Aprili, 2015.
(iii)            Mamlaka ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) ilibadili vikokotoo vya mafao kwa ajili ya wastaafu bila kushirikisha wala kupata ridhaa ya wadau ambao ni wanachama wa Mifuko ya Hifadhi husika wakiwemo walimu.
AZIMIO:
Kuitishwe mjadala wa wadau wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii, wadau na SSRA kabla au ifikapo tarehe 30 Aprili, 2015 ili kutafuta ufumbuzi wa suala hilo.  Hiyo itakuwa ni kutekeleza ahadi ya Mhe.  Waziri Mkuu aliyoitoa katika hotuba aliyoitoa katika Sherehe za Siku ya Mwalimu Duniani iliyofanyika Mjini Bukoba-Kagera Kitaifa tarehe 5 Oktoba, 2014 juu ya kuliangalia upya suala hilo.

(iv)            Madai na kilio cha muda mrefu cha walimu tangu awamu ya tatu ya uongozi wa Taifa hili ni kuwa na mwajiri mmoja- Chombo kimoja cha kushughulikia huduma zote za walimu kuliko ilivyo leo ambapo walimu wanaajiriwa na kuhudumiwa na Wizara na Taasisi zaidi ya nne.  Sasa kilio hiki kifike mwisho kwa kuwa hata Bunge la 16 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilipitisha Azimio la kuanzishwa kwa chombo kimoja cha kuajiri walimu.
AZIMIO:
Baraza la Taifa lina tamka kuwa chombo kimoja cha ajira ya walimu kiundwe na kuanza utekelezaji wake kabla au ifikapo tarehe 30 Aprili, 2015.  Aidha mchakato wa Sheria ya kutaka walimu waajiriwe na Mamlaka za Halmashauri za Wilaya uachwe mara moja kwani hauna tija kwa walimu na Elimu ya nchi hii.

MWISHO:
CWT mkoa wa Mbeya kinaitaka serikali kuhakikisha kwamba inawalipa madai walimu wote pamoja na kuwapandisha madaraja wanaostahili sambamba na kulipa fedha za likizo zao. Endapo haya hayatatekelezwa kwa muda mwafaka  Chama kitawaelekeza walimu/wanachama wake kuchukua maamuzi magumu juu ya serikali mwaka huu wa 2015.


Taarifa hii imetolewa na:
84B83991
NELUSIGWE KAJUNI
MWENYEKITI CWT MKOA WA MBEYA
31/1/2015

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

NAIBU WAZIRI WA KILIMO MHE MWANJELWA AMUAGIZA MRAJIS KUFANYA UCHUNGUZI SACCOS YA MADIBIRA-MBARALI NDANI YA SIKU 14

Naibu Waziri wa Wizara ya Kilimo, Mhe Mary Mwanjelwa akisisitiza jambo wakati akizungumza na Viongozi mbalimbali wa Mkoa na kamati ya uli...