Jumamosi, 18 Oktoba 2014

89 MBEYA MJINI, WAIKIMBIA CHADEMA NA KUJIUNGA CCM

 Mbunge wa viti maalum mkoani Mbeya, Dr. Mary Mwanjelwa, akizungumza na baadhi ya vijana waliotoka Chadema na kujiunga na CCM jimbo la Mbeya mjini jana.
 Mbunge wa viti maalum mkoani Mbeya, Dr. Mary Mwanjelwa, akizungumza na baadhi ya vijana waliotoka Chadema na kujiunga na UVCCM jimbo la Mbeya mjini jana kisha akawakabidhi jezi.

VIJANA 89 waliokuwa wanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Jimbo la Mbeya mjini linaloongozwa na Mbunge Joseph Mbilinyi(Sugu), wamekihama chama hicho na kujiunga na Chama Cha Mapinduzi(CCM).

Wanachama hao wapya wa CCM, walijiunga na chama hicho jana katika kata za Ilomba na Ruanda wakitokea katika maeneo ya Ilomba, Mama John, Makunguru, Mwanjelwa na Kabwe.

Akiwapokea na kuwakabidhiwa kadi zao mpya za CCM na UVCCM, Mbunge wa Viti maalum mkoani Mbeya, Dr. Mary Mwanjelwa, aliwapongeza kwa uamuzi wao wa kurejea na wengine kujiunga na kuchukua kadi za chama hicho.

“Nawapongezeni wote maana hamjakosea kurejea kwenye chama salama ambacho kinajali vijana kwa kuwawezesha kuwa wajasiliamali”alisema Dr. Mwanjelwa.

Awali akisoma risala ya chama tawi la Ilomba, Katibu wa tawi hilo Lucian Kapinga, alisema kuwa wakati wa vurugu zilizotokea Jijini Mbeya na kupachikwa jina la “Maandamano ya machinga”, baadhi ya wajumbe walinusurika kufa baada ya ofisi hiyo kuvamiwa na vijana na kuichoma moto wakati wajumbe wakiwa kwenye kikao.


Alisema kutokana na uhalibifu huo, jengo lao liliungua na kulazimika kulifumua na kulifanyia ukarabati ambapo kwa sasa umebaki ukarabati mdogo unaogharimu kiasi cha Tsh.6000,000/=.

Dr. Mwanjelwa aliwapa pole na kuchangia kiasi cha Tsh.200,000/= huku akiwaasa vijana kuepukana na mkumbo wa siasa za vurugu, huku akiwapatia jozi moja ya jezi na mipira minne kwa ajili ya vijana wa kike na kiume.

Nape nnauye akumbushwa ahadi.

Katika mfululizo wa ziara za Mbunge Dr. Mary Mwanjelwa Jimbo la Mbeya Mjini za kupokea wanachama wapya kutoka Chadema, alisomewa risala ya kumkumbusha Katibu wa itikadi na uenezi wa CCM Taifa, Nape Nnauye aliyowaahidi vijana wa mtaa wa Blue house Kabwe Mwanjelwa, kuhusu ujasiliamali.

Akisoma risala hiyo kwa niaba ya wenzake 50,ndani ya ukumbi wa Mfikemo Hotel, Mariam Hamisi, alisema kuwa Nape alitembelea eneo hilo na kuwaahidi vijana hao kuwapatia mtaji endapo watafungua akaunti benki, ambapo kwa sasa tayari wamefungua akaunti na kuunda kikundi chao kinachojuliakana kwa jina la Halimpya kasi mpya.

“Sisi tumebadilika na kurejea CCM, wapo wengi nyuma yetu, tunakiomba chama kimsimamishe mtu anayekubalika ili kukomboa jimbo la Mbeya mjini na sisi tuna imani na wewe, tunaomba pia ututangaze hata kwa marafiki zako ili tuwe mfano kwa wenzetu kuhusu uchumi” alisema Mariam.
Baada ya risala hiyo, kundi lingine la vijana walijitokeza na kutamka kuwa nao wanahitaji kujiunga na CCM na kuwa na kikundi kilichosajiliwa ili wawe wajasiliamali na kwamba wametumikishwa vya kutosha na Chadema bila kupewa maarifa ya kujikwamua kiuchumi.

Akijibu risala na maoni ya waliojitokeza katika eneo hilo, Dr, Mwanjelwa aliwahakikishia kuwa risala hiyo ataifikisha kwa Nape Nnauye na yeye akawakabidhi Tsh. 200,000/= na kumwagiza Katibu wa UVCCM wilaya ya Mbeya Mjini, Julius Msaka kuwa akutane na vijana wanaohitaji kurejea na kujiunga na CCM na kutaka kuwa wajasiliamali ili wapange jinsi ya kuanzisha kikundi na utaratibu wa kupewa kadi za chama hicho.


Mbali na mambo mengine, aliwasihi wanachama hao wapya na wengine kujitokeza kujiandikisha katika uboreshaji wa daftari la kudumu, zoezi ambalo alisema litaanza mwezi ujao.

Sanjali na hayo alitetea suala la rasimu ya tatu ya katiba kuwa imejaa maslahi ya wananchi likiwemo suala la hamsini kwa hamsini kwa wanawake ambalo aliwasihi wanawake kutolitumia vibaya ikiwemo kuvuruga maadili na utu wa mwanamke matokeo yake litavunja ndoa.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

NAIBU WAZIRI WA KILIMO MHE MWANJELWA AMUAGIZA MRAJIS KUFANYA UCHUNGUZI SACCOS YA MADIBIRA-MBARALI NDANI YA SIKU 14

Naibu Waziri wa Wizara ya Kilimo, Mhe Mary Mwanjelwa akisisitiza jambo wakati akizungumza na Viongozi mbalimbali wa Mkoa na kamati ya uli...