Alhamisi, 19 Juni 2014

DR. MWANJELWA ATAKA WAFANYABIASHARA MBEYA WAPATE NAFASI SOKO LA KIMATAIFA




WAKATI kukiwa na tetesi za kwamba baadhi ya wafanyakazi wa Jiji la Mbeya na baadhi ya wafanyabiashara wakubwa Jijini hapa wamejigawia vyumba katika soko jipya la Mwanjelwa, Mbunge wa viti maalum mkoa wa Mbeya, Dr. Mary Mwanjelwa, ameiomba serikali kutupia macho soko hilo na kuhakikisha hata wafanyabiashara wa kawaida wanapata nafasi.

Hayo aliyasema jana wakati anachangia Hotuba ya Bajeti kuu ya serikali mjini Dodoma.

Alisema soko hilo kwa sasa licha ya kutokamilika kwa wakati, serikali kupitia Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Jiji la Mbeya limepata mkopo mwingine wa Bilioni tatu kwa ajili ya kukamilisha ujenzi na wamepata mkandarasi mpya.

‘’Kama unavyoelewa Mheshimiwa Spika, kule kwangu Mbeya, kuna soko la kimataifa na Waziri Mkuu anajua na katika miezi nane ijayo soko litakamilika na ninaomba Wizara ya Fedha itupatie gurantee ya 3.4 bilioni ili tuweze kupata mara moja na wafanyabiashara wote wanufaike na soko ambalo lina jina langu la Mwanjelwa’’ alisema Dr. Mwanjelwa.

Pia aliiomba serikali kuchepusha barabara ya magari makubwa kutoka Uyole mpaka Songwe Mbeya Vijijini, ambako kuna uwanja wa Ndege ili kusaidia kuondoa msongamano wa magari Jiji la Mbeya ambalo linapanuka kila siku.

Mbali na jambo hilo, alichangia mambo mbalimbali likiwemo suala la misamaha ya kodi inayotolewa na serikali kwa wafanyabiashara wakubwa, migodi na makapuni ya simu, huku akieleza kuwa serikali inapaswa pia kufufua viwanda ili kupunguza tatizo la ajira.

“Mheshimiwa spika, uchumi wa nchi tunaambiwa kuwa unakua sana, sasa watanzania hawana kipato na maisha yao yanazidi kushuka, sasa uchumi unakua kwa namna gani? Deni la taifa linatishia usalama wa taifa, ongezeko la asilimia 29 najiuliza je tutafika?’’ alihoji Mbunge huyo.

‘’Tumekuwa tunazungumzia kuhusu walimu, naishauri serikali walimu wasikatwe maana wafanyakazi wote Tanzania wanaokatwa, wakienda sokoni pia wanaendelea kukatwa tena, wakati wanakatwa kodi mishahara yao’’.

Alishangaa kuwa Bunge linaidhinisha bajeti lakini pesa haitoki na kwamba matumizi mengine yanatumika bila kuidhinishwa, hivyo alihoji kama bunge hilo linatUmika kama stempu au la.

Aliitaka Wizara ya fedha pamoja na wabunge kurudi bungeni kuelezana mrejesho wa matumizi ya fedha za serikali na kwamba ifike mahala wabunge wawe wakali na sheria kali zitungwe ili wanaochelewesha fedha au kuhusika kwenye Fund Location na fund department wawajibishwe, pesa zisipotolewa kwa wakati.

“Kuna kipindi nilisimama hapa na kusema halmashauri zote zilizo na hati chafu ziadhibiwe, kwanini mambo yanafichwafichwa, kuna nini? makampuni ya simu na madini mbona hatuambiwi mikataba yake na misamaha ya kodi? Watanzania wajulishwe na wawekwe wazi’’ alisema.

Alisema watanzania wa kawaida wanaumia kutokana na bajeti ya kutegemea pombe na sigala na vinywaji, kwasababu ndiyo wanaotumia vitu hivyo kila siku.

‘’Ninaomba sana, tuangalie jinsi gani tufufue viwanda vyetu kusaidia ajira kwa vijana wanaokimbilia mijini na haya ndiyo maendeleo yenyewe. Kwenye private sector kule watu wanafanya kazi hakuna rongorongo na hii PPP, itasaidia kufufua viwanda na kuongeza ajira’’ alisema.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

NAIBU WAZIRI WA KILIMO MHE MWANJELWA AMUAGIZA MRAJIS KUFANYA UCHUNGUZI SACCOS YA MADIBIRA-MBARALI NDANI YA SIKU 14

Naibu Waziri wa Wizara ya Kilimo, Mhe Mary Mwanjelwa akisisitiza jambo wakati akizungumza na Viongozi mbalimbali wa Mkoa na kamati ya uli...