Ijumaa, 23 Mei 2014

DR.MWANJELWA ASAIDIA WAATHIRIKA MAFURIKO KYELA

Mbunge wa Viti maalum mkoa wa Mbeya, Dr. Mary Mwanjelwa, akimkabidhi mashuka Mkuu wa Wilaya ya Kyela, Magreth Malenga na Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya hiyo, Clemens Kasongo, kabla ya kwenda kuwakabidhi wananchi walioathirika na mafuriko mwaka huu 2014.

Mbunge wa Viti Maalum mkoa wa Mbeya, Dr. Mary Mwanjelwa, akiwasalimu wanawake na kuwapa pole katika Kijiji cha Nyerere wilayani Kyela mkoani Mbeya.

Pokea mkono wa Baraka.....
 
Mbunge wa Viti Maalum mkoa wa Mbeya, Dr. Mary Mwanjelwa, akivuka daraja la mianzi katika Kijiji cha Mpunguti.


MBALI na Mbunge wa Jimbo la Kyela mkoani Mbeya, Dr, Harrison Mwakyembe, kutoa misaada kwa waathirika wa mafuriko Jimboni humo,  Mbunge wa viti maalum (CCM), Mkoa wa Mbeya, Dr. Mary Mwanjelwa, naye amejitokeza na kutoa misaada ya kiutu kwa wananchi wa wilaya hiyo.


Akizungumza na wananchi katika Mkutano wa hadhara wa Kijiji cha Nyerere, Dr. Mary Mwanjelwa, alisema mbali na kwamba mafuriko hayo yameathiri kaya nyingi, lakini ana uhakika kuwa wanawake na watoto ndiyo walioathirika zaidi.

“Maandiko yanasema lieni na wanaolia, najua wakati mafuriko yanatokea wengine yamewakuta wakiwa wajawazito, ninyi siyo wakiwa, tupo pamoja, nilipopata taarifa hii sikuweza kukaa na amani pale Bungeni, nimeacha posho na kuja kuwapa pole ndugu zangu’’ alisema Dr.Mwanjelwa huku akipiga magoti.


Diwani wa kata ya Bujonde, Paul Mwambafula, alisema Kata yake ndiyo kata iliyoathirika zaidi katika wilaya hiyo ambapo kaya 2,400 zilikumbwa na mafuriko hayo, lakini kaya 1800, ziliathirika zaidi.

Mwenyekiti wa Umoja wa wanawake Tanzania(UWT), Pricila Mbwaga na Katibu wa UWT Mkoa wa Mbeya, Mariam Yusuph, waliwaambia wananchi wa Kijiji cha Nyerere na Mpunguti kuwa, tatizo hilo siyo la kwao peke yao, maana dunia imelisikia.

Mkuu wa wilaya ya Kyela, Magreth Malenga na Afisa tarafa ya Unyakyusa, Kheri William, walimshukuru Mbunge, Dr. Mwanjelwa kuwa mstari wa mbele kujitoa kusaidia wenye uhitaji na kwamba kamati ya maafa ya wilaya hiyo, itamalizia kusaidia kaya zilizoathirika katika Kijiji cha Nyerere.

Dr. Mwanjelwa alitoa mashuka 150 katika Vijiji vya Nyerere na Mpunguti na kutoa wito kwa taasisi na watu binafsi kujitokeza kuwasaidia wananchi wa wilaya hiyo walioathirika na mafuriko hayo.

Baadhi ya mashuka yalitolewa na benki ya NMB baada ya Mbunge huyo kuiomba taasisi hiyo ya kifedha, ambayo mbali na mashuka, ilimkabidhi madawati 83 kwa ajili ya shule za Msingi.

“Benki ya NMB inatoa huduma zake katika jamii ya watu mbalimbali. Wanafunzi, watoto, watu wazima, wazee, mashirika na makampuni na wateja mbalimbali. Sis kwetu hawa wote ni wadau ambao ndio wanafanya NMB iendelee kuwepo’’ alisema Meneja wa NMB Kanda ya Nyanda za juu kusini, Lucresia Makiriye.

Akishukuru kwa niaba ya wananchi wenzake wa Kijiji cha Mpunguti, Mzee Water Butungulu, alienda mbali na kumweleza Dr. Mwanjelwa kuwa endapo atawania nafasi ya Ubunge mwakani, atashinda kutokana  na juhudi zake za kuhudumia jamii.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

NAIBU WAZIRI WA KILIMO MHE MWANJELWA AMUAGIZA MRAJIS KUFANYA UCHUNGUZI SACCOS YA MADIBIRA-MBARALI NDANI YA SIKU 14

Naibu Waziri wa Wizara ya Kilimo, Mhe Mary Mwanjelwa akisisitiza jambo wakati akizungumza na Viongozi mbalimbali wa Mkoa na kamati ya uli...