Baadhi ya ndugu na jamaa wakisubiri muda wakuingia kuwaona ndugu zao
BAADHI ya wananchi wanaouguza ndugu zao
katika Hospitali ya Rufaa ya Mbeya wamelalakia kitendo cha uongozi wa Hospitali
hiyo kuwafukuza mawodini bila kuwa na utaratibu wala mahali pa kusubiri na
kuishi wakati ndugu zao wakitibiwa.
Wananchi hao wanaotoka maeneo tofauti
nje na ndani ya Mkoa wa Mbeya wamekuwa wakilala nje ya Hospitali hiyo kutokana
na wengi wao kukosa mahala pa kuishi hali inayowapelekea kuhatarisha maisha yao
kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha mkoani hapa.
Wakizungumza na Mbeya yetu baadhi ya
wananchi waliokutwa wamelala kando kando ya Hospitali hiyo walisema wanapata
usumbufu mkubwa na wanalazimika kulala nje kwa sababu wanafukuzwa wodini ili
hali wanajua ni wageni na wagonjwa wao wanatakiwa kupewa huduma za chakula na
usafi nje ya Hospitali.
Mmoja wa wananchi hao, Justina Aswile
mkazi wa Kapugi Wilaya ya Rungwe, ambaye anamuuguza ndugu yake alisema tangu
apewe rufani katika Hospitali ya Wilaya ya Rungwe Makandana hana hata ndugu wa
kukaa kwake bali analazimika kukesha nje kusubiria muda wa kuona wagonjwa ndipo
aingie Wodini.
Alisema ni bora serikali ama hospitali
hiyo ikajenga eneo la kupumzikia wanaouguza ndugu zao ili wapate sehemu ya
kupikia baadhi ya vyakula ili kuondoa usumbufu na gharama kubwa zinazowakabili
ikiwemo kulazimika kununua chakula wakati wanauwezo wa kupika.
Mwananchi mwingine Kufimba Kalinga
alisema anamuuguza baba yake mzazi tangu Februari 19, mwaka huu na tangu hapo
amekuwa akilazimika kulala kwa kuomba omba kwa watu mbali mbali jambo ambalo
linamletea usumbufu kutokana na kukosa uhuru wa kumuandalia chakula mgonjwa
wake.
Walisema wanaiomba serikali kuwajengea
sehemu ya kupumzikia na kulala kama zilivyo Hospitali zingine zilizotenga
majengo maalumu yanayowasaidia kulala na kuandaa chakula kwa ajili ya wagonjwa
wao.
Kwa upande wake Katibu wa Hospitali ya
Rufaa ya Mbeya, Aisha Mtanda, alikiri kuwepo kwa changamoto hiyo na kuongeza
kuwa tatizo hilo ni la muda muda mrefu lakini changamoto ni upungufu wa fedha
wa kuweza kutenga eneo la kupumzikia wanaouguza wagonjwa wao.
Mtanda alisema hivi sasa uongozi wa
Hospitali una mpango wa kuboresha moja wapo ya majengo yaliyopo ndani ya
hospitali ili yasaidie kupumzikia kutokana na mazingira wanaishi wananchi hao
kuwa magunjwa na hatarishi kwa magonjwa mbali mbali ikiwemo kupata madhara
kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha.
Aliongeza kuwa wanatarajia kuomba msaada
kwa wadau mbali mbali ili waweze kujenga eneo la kupumzikia watu hao ikiwemo
Halmashauri ya Jiji la Mbeya kuwapatia eneo la nje ya Hospitali
litakalowasaidia kuandaa vyakula na shughuli zenye msaada kwa wagonjwa wao.
credit;Mbeya yetu
|
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni