Mkuu wa Wilaya ya Kalambo, mkoani
Rukwa, Moshi Chang’a amefariki dunia. Kiongozi huyo alifariki dunia
jana saa 10: 15 jioni katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, alikokuwa
amelazwa kwa zaidi ya siku 20.
Ofisa Habari wa hospitali hiyo, Aminieli Aligaesha
alisema DC Chang’a alifika hospitalini hapo Machi 29, mwaka huu akiwa
anaumwa na kulazwa.
Alisema madaktari wamekuwa wakimpatia matibabu, lakini ilipofika jana saa 9:30 alasiri hali yake ilibadilika ghafla.
“Walijitahidi kuokoa uhai wake bila mafanikio na
ilipofika saa 10: 15 alikata roho, alisema Aligaesha huku akikataa
kueleza tatizo lililokuwa linamsibu.
“Huyu ni kiongozi wa Serikali, bila shaka wakubwa huko serikalini wataeleza zaidi kuhusu kifo hicho,” alisema.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi),
Hawa Ghasia alithibitisha kutokea kwa kifo hicho mchana wa jana, baada
ya kiongozi huyo kusumbuliwa na ugonjwa wa shinikizo la damu.
Alisema amemwagiza katibu wake (wa waziri) na Mkuu
wa Mkoa wa Rukwa, Stella Manyanya kufuatilia na kushughulikia msiba huo
na taarifa zaidi kuhusu utaratibu zitapatikana leo baada ya kuzungumza
na familia.
Chang’a kabla ya kuhamishiwa katika Wilaya ya Kalambo alikuwa DC wa Wilaya Mpya ya Mkalama.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni