Alhamisi, 21 Novemba 2013

DR. MARY MWANJELWA; MWANAMKE SHUPAVU WA SIASA ZA VITENDO




Na, Marymwanjelwa Reporter-Mbeya

UNAPOPATA kujua historia za wanasiasa wanawake nchini Tanzania wanaofanya vizuri katika majimbo ama mikoa yao, ni dhahili huwezi kukosa jina la Dr. Mary Mwanjelwa.

Mwanamke huyo ni Mbunge wa Viti maalum kutokea mkoani Mbeya kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Sifa yake ya kwanza ni ucheshi ambao yeye anasema kuwa ucheshi wake unatokana na wokovu alionao(kumcha Mungu).

Kabla ya kujikita katika masuala ya siasa alikuwa Mkurugenzi wa shirika la PSI Tanzania ambako historia haimuhukumu hata baada ya kutoka huko kwa kile kinachojieleza kuwa alitoka na utumishi uliotukuka.

Katika mahojiano na Mwandishi wa makala haya, Dr. Mary Mwanjelwa anasema kuwa alipata ubunge kupitia viti maalum mwaka 2010.

Anasema kwa sasa katika mkoa wa Mbeya, kuna wabunge wa viti maalum wawili ambao ni yeye na Hilda Ngoye.

‘’Najivunia nafasi niliyonayo maana imenipa na nafsi ya kuwa Mbunge wa Bunge la Ulaya nikiwakilisha Tanzania’’ anasema Dr. Mwanjelwa.

Alipoulizwa kuwa tangu achaguliwe kuwa Mbunge wa mkoa huo amefanya nini cha kujivunia mpaka sasa, alisema ameweza kuwainua makundi mbalimbali hasa wanawake wa wilaya zote za mkoa wa Mbeya.

Anasema anapenda sana kushiriki katika shughuli za kimaendeleo za jumuiya na hata familia moja moja.

‘’Kuanzia mwaka 2010, kwa kukumbuka baadhi ya niliyoyafanya ni pamoja na kujumuika na kuwasaidia yatima,  kusaidia vikundi vya akina mama na kufadhili semina za madiwani wa vyama vyote juu ya utendaji bora’’ anasema Dr. Mwanjelwa.


Elimu.
Anataja maeneo ambayo amewahi kujumuika na jamii kuhusu elimu kuwa ni  kushona sare za shule nguo na viatu kwa watoto yatima 100 kata za Kambasegele na Kiwira wilayani Rungwe.


Anasomesha watoto yatima 2 wa kike kila wilaya za mkoa wa Mbeya ambazo ni Mbeya mjini, Kyela, Rungwe, Mbeya Vijijini, Mbarali, Chunya, Ileje na Mbozi.

Si hayo tu bali nimesaidia ujenzi wa sekondari kata ya Itagano-Jiji la Mbeya, mifuko ya saruji tani Moja, ujenzi wa sekondari ya kata ya Ruanda saruji tani Moja na niligawa vitabu katika sekondari 9 zote za mkoa wa Mbeya, kila wilaya shule Moja na Kugawa vitanda 19 katika hosteli ya wasichana Sekondari ya Isansa ’’ anasema Mbunge huyo.


Ujasiliamali
Anasema amefanikiwa kuanzisha vikundi vya ujasiriamali kwa kina mama kila wilaya -zote za mkoa wa Mbeya na  kufadhili Mashine za kutotolea vifaranga na kutoa pesa za mitaji wilaya zote za mkoa wa Mbeya.

‘’Nilitoa mafunzo ya ujasiriamali kwa kina mama juu ya incubators hizo nilizowafadhili ili waweze kuendelea kujitegemea katika kukuza uchumi wao badala ya kuwa wategemezi kila wakati na niliendesha mafunzo ya ujasiriamali kwa wana Mbeya kwa kuzingatia jinsia’’ anasema Mbunge huyo.

Aliwezesha kaya 300 mbuzi wawili wawili  kaya -kata ya Kambasegela na Kiwira wilayani Rungwe.

Afya
Anaeleza kuwa ni mambo mengi ya jamii aliyoshiriki na mengine ameyasahau lakini anakumbuka pia aligawa magodoro 250 katika hospital za serikali katika wadi za wazazi wilaya ya Ileje, Mbozi, Chimala(Mbarali), Ruanda na hospitali ya Rufaa ya Mbeya kitengo cha wazazi Meta Jijini Mbeya.

Aidha anasema amegawa vitanda 19 katika hosteli ya wasichana Sekondari ya Isansa iliyopo wilayani Mbozi, kutoa gari ya sinema katika Jiji la Mbeya juu ya uelimishaji Umma katika Tiba kwa Kadi kupitia mfuko wa Bima ya afya ya Taifa(NHIF).

Kushiriki kampeni ya kufanya usafi katika Jiji la Mbeya.
‘’Nilitoa vyakula katika vituo cha watoto yatima cha Iwambi na kugawa nguo na mablanketi katika kituo cha watoto yatima cha Uyole vyote vya Jijini Mbeya’’ anasema Dr. Mwanjelwa.

Sanjali na vitu hivyo, anasema kuwa alitoa pia viti vya walemavu wa viungo katika Jiji la Mbeya mbele ya Askofu kiongozi wa kanisa la Moravian Tanzania Alinikisa Cheyo siku alipkuwa akimshukuru Mungu kwa kumponya na mauti katika ajali mbaya aliyoipata mwaka jana 2012.

Uongozi.
Katika masuala ya uongozi, anasema aliendesha na atazidi kufanya hivyo kwa kufadhili mafunzo/semina za mara kwa mara kwa Madiwani wote wa Mkoa wa Mbeya, juu ya Uongozi na uwajibikaji.

‘’Mbali na mafunzo ya madiwani hao, nimewahi kuendesha mafunzo/semina kwa watendaji wote wa ngazi ya kata juu ya Uongozi na uwajibikaji na nitazidi kufanya hivyo’’ anasema.

Anajipambanua kuwa pia amewahi kuendesha mafunzo/semina kwa wenyeviti na makatibu wa umoja wa wanawake wa chama chake UWT katika wilaya zote za mkoa wa Mbeya jinsi ya Uongozi na Uwajibikaji.

Mbali na kazi za kijamii, anasema mara kadhaa huwa anashiriki kazi za kusaidia vikundi, waimbaji na hata makanisa ambapo hivi karibuni alitoa vyombo vya Muziki Kanisa la Ruanda Moravian kwaya Kuu Jiji la Mbeya.

Mbali na makanisa anaeleza kuwa anashiriki pia kusaidia michango mbali mbali ya kijamii kama vile-michango misikitini, makanisani, matamasha, harambee n.k

Alipoulizwa kuwa kuwa anapenda nini katika utumishi wake wa Ubunge, anasema anapendelea sana na atazidi kuhimiza/kuhamasisha uanzishwaji wa vikundi vya aina  mbali mbali vya ujasiriamali, Sanaa n.k. kwa wa kina mama, vijana na wazee.

Kuhusu ajali aliyoipata

Anasema kwa sasa alirudi nyuma kidogo katika kufanya kazi hizo za kuikomboa jamii kiuchumi kutokana na ajali mbaya aliyoipata mwaka jana 2012 katika mteremko wa mlima Iwambi eneo la Mbalizi wilaya ya Mbeya ambayo ilisababisha kifo cha msaidizi wake.

‘’Ajali mbaya niliyopata mwaka jana ilinikwamisha mambo mengi nilikuwa nimepanga kuendelea kuteketeleza Ilani ya CCM lakini namshukuru Mungu afya yangu inaimarika na nitazidi kuwatumikia ndugu zangu wa Mbeya kutoka rohoni, ndivyo nilivyo asili mwana jamii hata kabla sijawa Mbunge, Mungu anisaidie niwatumikie kwa maendeleo na tukishirikiana wote vema tutajikomboa katika mengi’’ anasema Dr. Mary Mwanjelwa.

Kuhusu kugombea tena mwaka 2015, anasema kuwa Mungu akimpa kibali na afya njema atagombea na anaamini sifa anazo za kuendelea kuwa Mbunge wa Jimbo ama viti maalum.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

NAIBU WAZIRI WA KILIMO MHE MWANJELWA AMUAGIZA MRAJIS KUFANYA UCHUNGUZI SACCOS YA MADIBIRA-MBARALI NDANI YA SIKU 14

Naibu Waziri wa Wizara ya Kilimo, Mhe Mary Mwanjelwa akisisitiza jambo wakati akizungumza na Viongozi mbalimbali wa Mkoa na kamati ya uli...