SHULE ya
sekondari Lubala iliyopo wilayani Rungwe mkoani Mbeya, ni shule inayomilikiwa
na Mbujah Brothers Association nan i moja kati ya shule zinazofanya vizuri
kitaalum yakiwemo masomo ya Sayansi.
Kuwepo kwa
shule hiyo katika eneo la kitongozji cha Lubala, Kijiji cha Lukata, kata ya
Kinyala, Tarafa ya Ukukwe, kumesaidia kupatikana na kupanuka kwa miundombinu ya
maji na umeme katika eneo hilo.
Wanakijiji pia
wamepata ajira ndogondogo kama vile vibarua, wajenzi, wapishi na walinzi.
Mbali na
faida hizo, pia wanafunzi walio jirani na shule hiyo wanapewa nafasi za
kufundshwa bure nyakati za usiku na Jumamosi na walimu wa shule hiyo ili kukuza
mahusiano na taaluma.
Wanafunzi wa
shule hiyo, wanasema hakuna masomo mepesi kama ya sayansi kutokana na masomo
hayo kuwa na hisia za viumbe hai.
Wanafunzi
waliokutwa katika maabara ya somo la Biolojia shuleni hapo, waliliambia gazeti
hili kuwa tangu waanze masomo katika shule hiyo, wamehamasika kusoma masomo
hayo kutokana na shule hiyo kuwa na maabara na vifaa vya kutosha.
Mwanafunzi
wa kidato cha pili, William Kulwa(15), anasema alifaulu kujiunga na kidato cha
kwanza shule ya serikali ya Tukuyu Day, lakini wazazi wake wakampeleka katika
shule hiyo ambapo malengo yake kwa baadae ni kuwa Daktari wa binadamu.
“Natarajia
kuwa Daktari maaana masomo ninayosoma ya sayansi yana hisia za binadamu na
viumbe hai jinsi wanavyoishi, ingawa somo la Fizikia bado linanisumbua kidogo’’
alisema mwanafunzi William.
Happy John(15)
wa kidato cha pili, anasema kuwa anatarajia kuwa Injinia baada ya kuhitimu
masomo yake hapo baadae.
Katika hafla
fupi ya maazimisho ya miaka kumi ya mafanikio ya shule hiyo yaliyofanyika
shuleni hapo mwanzoni mwa mwezi Mei mwaka huu, Mkurugenzi wa shule ambaye pia
ni mkuu wa shule, Noah Mwasiposya, anasema shule hiyo imepata mafanikio makubwa
kutokana na kuhamasisha kwa vitendo masomo ya sayansi.
“Mwaka 2004,
tulianza na wanafunzi 215 na sasa tuna wanafunzi 1031 huku tukizidi kuimarisha
taaluma, majengo na mazingira na tunaishukuru Hospitali ya Igogwe iliyopo
karibu nasi, kwa ajili ya matibabu ya watumishi na wanafunzi’’ alisema Mkuu wa
shule hiyo.
Kwa upande
wake, Mwalimu Paison Mwalinga, anasema hamasa wanayoitia kwa wanafunzi kupenda
masomo ya sayansi katika shule hiyo kwa vitendo, ndiyo nguzo moja wapo ya
wanafunzi wao kupenda masomo hayo.
“Tunahamasisha
vijana wengi kupenda masomo ya sayansi kwa kuwa na stream mbili za sayansi na
kila mwaka zaidi ya vijana 60 wanajikita katika masomo hayo. Wanafunzi wengi
wapo katika vyuo vya uuguzi na sekondari kidato cha tano na sita’’ alisema
Mwakalinga.
Mwalimu
Peter Nkanje, alisema mbali na mafanikio ya shule hiyo ya Lubala, changamoto
wanayopata ni pamoja na kupata taarifa za wanafunzi wao wa kidato cha Nne
wanaohitimu hapo na kujiunga na shule za sekondari katika masomo ya sayansi
ambao wanashindwa kufaulu vizuri kutokana na shule wanazoenda kutokuwa na
mazoezi ya mara kwa mara tofauti na shule yao.
Anasema mafanikio
ya shule hiyo haiwezi kukamilika bila kuwataja baadhi ya watumishi wa shule
hiyo ambao wapo zaidi ya miaka tisa tangu kuanzishwa shule hiyo.
Anawataja Noah
Mwasiposya, yeye menyewe Peter Nkanje, John Charles Ngullah, Paison Mwakalinga,
Yonathan Yaunde, Isaack Jonas na Maiko Maganga.
Wengine ni
wafanyakazi wasio walimu ambao ni Alimundu Pasukali, Getruda Michael, Matrida
Tosigwe, Rose Mwangamilo, Tumaini Samboma, Lucia Kabuje na Upendo Sambo.
Mwenyekiti wa
bodi ya shule hiyo, Dr. John Mwakatage, anasema ni vema wazazi wa wanafunzi
wanaohitimu katika shule hiyo kidato cha Nne na kufaulu, wakawabakiza watoto
wao ili waendelee na kidato cha tano na sita hap badala ya kuwapeleka kwenye
shule za serikali.
Anataja sababu
kubwa ya hoja yake hiyo kuwa ni shule nyingi za serikali kumejaa migogoro mingi
kati ya walimu na serikali na migomo ya mara kwa mara inayosababisha athari
kubwa kwa wanafunzi.
“Mzumbe na
nyingine zilikuwa shule nzuri, kwasasa wote tunashuhudia ilivyo, mwacheni
mfugaji aendelee kulelewa na mfugaji aliyemzoea’’ anasema Mwenyekiti huyo wa
bodi.
Afisa elimu
Sekondari wa Halmashauri ya Rungwe, Anna Chigulu, anasema kuwa tangu utumishi
wake, hajawahi kuona shule inayozawadia wanafunzi waliohitimu na kufaulu kama
inavyofanya shule hiyo ya Lubala.
Mbali na
mshangao huo, pia aliitaja shule hiyo kuwa ya mfano katika mkoa wa Mbeya kama
siyo nchi nzima kwa ujumla, kutokana na uogozi kuruhusu wazazi maskini wa
kipato cha fedha, kupeleka kuni ama mazao, kisha kuthaminishwa kuwa ada ya
mwanafunzi.
“Wilaya ya
Rungwe kwa mkoa wa Mbeya, tumeweza kuwa vinara wa matokeo makubwa sasa(BRN),
shule ya Lubala imetupandisha chati’’ alisema Afisa elimu huyo.