WAKATI
kukiwa na tetesi za kwamba baadhi ya wafanyakazi wa Jiji la Mbeya na baadhi ya
wafanyabiashara wakubwa Jijini hapa wamejigawia vyumba katika soko jipya la
Mwanjelwa, Mbunge wa viti maalum mkoa wa Mbeya, Dr. Mary Mwanjelwa, ameiomba
serikali kutupia macho soko hilo na kuhakikisha hata wafanyabiashara wa kawaida
wanapata nafasi.
Hayo
aliyasema jana wakati anachangia Hotuba ya Bajeti kuu ya serikali mjini Dodoma.
Alisema soko
hilo kwa sasa licha ya kutokamilika kwa wakati, serikali kupitia Waziri Mkuu,
Mizengo Pinda, Jiji la Mbeya limepata mkopo mwingine wa Bilioni tatu kwa ajili
ya kukamilisha ujenzi na wamepata mkandarasi mpya.
‘’Kama
unavyoelewa Mheshimiwa Spika, kule kwangu Mbeya, kuna soko la kimataifa na
Waziri Mkuu anajua na katika miezi nane ijayo soko litakamilika na ninaomba
Wizara ya Fedha itupatie gurantee ya 3.4 bilioni ili tuweze kupata mara moja na
wafanyabiashara wote wanufaike na soko ambalo lina jina langu la Mwanjelwa’’
alisema Dr. Mwanjelwa.
Pia aliiomba
serikali kuchepusha barabara ya magari makubwa kutoka Uyole mpaka Songwe Mbeya
Vijijini, ambako kuna uwanja wa Ndege ili kusaidia kuondoa msongamano wa magari
Jiji la Mbeya ambalo linapanuka kila siku.
Mbali na
jambo hilo, alichangia mambo mbalimbali likiwemo suala la misamaha ya kodi
inayotolewa na serikali kwa wafanyabiashara wakubwa, migodi na makapuni ya
simu, huku akieleza kuwa serikali inapaswa pia kufufua viwanda ili kupunguza
tatizo la ajira.
“Mheshimiwa
spika, uchumi wa nchi tunaambiwa kuwa unakua sana, sasa watanzania hawana
kipato na maisha yao yanazidi kushuka, sasa uchumi unakua kwa namna gani? Deni
la taifa linatishia usalama wa taifa, ongezeko la asilimia 29 najiuliza je
tutafika?’’ alihoji Mbunge huyo.
‘’Tumekuwa
tunazungumzia kuhusu walimu, naishauri serikali walimu wasikatwe maana
wafanyakazi wote Tanzania wanaokatwa, wakienda sokoni pia wanaendelea kukatwa
tena, wakati wanakatwa kodi mishahara yao’’.
Alishangaa
kuwa Bunge linaidhinisha bajeti lakini pesa haitoki na kwamba matumizi mengine
yanatumika bila kuidhinishwa, hivyo alihoji kama bunge hilo linatUmika kama
stempu au la.
Aliitaka
Wizara ya fedha pamoja na wabunge kurudi bungeni kuelezana mrejesho wa matumizi
ya fedha za serikali na kwamba ifike mahala wabunge wawe wakali na sheria kali zitungwe
ili wanaochelewesha fedha au kuhusika kwenye Fund Location na fund department wawajibishwe,
pesa zisipotolewa kwa wakati.
“Kuna
kipindi nilisimama hapa na kusema halmashauri zote zilizo na hati chafu
ziadhibiwe, kwanini mambo yanafichwafichwa, kuna nini? makampuni ya simu na
madini mbona hatuambiwi mikataba yake na misamaha ya kodi? Watanzania wajulishwe
na wawekwe wazi’’ alisema.
Alisema
watanzania wa kawaida wanaumia kutokana na bajeti ya kutegemea pombe na sigala
na vinywaji, kwasababu ndiyo wanaotumia vitu hivyo kila siku.
‘’Ninaomba
sana, tuangalie jinsi gani tufufue viwanda vyetu kusaidia ajira kwa vijana
wanaokimbilia mijini na haya ndiyo maendeleo yenyewe. Kwenye private sector
kule watu wanafanya kazi hakuna rongorongo na hii PPP, itasaidia kufufua
viwanda na kuongeza ajira’’ alisema.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni