Serikali
imeupongeza Wakala wa ukaguzi wa madini nchini (TMAA) kwa kufanikiwa kuokoa
kiasi kikubwa cha madini yaliyokuwa yakitoroshwa kinyemela katika viwanja vya
ndege nchini hivyo kuokoa zaidi ya bilioni 15 zilizolipwa kama mrahaba tangu
ilipoanzisha ukaguzi maalum kwa wasafiri waendao nje ya nchi.
Pongezi
hizo zimetolewa na Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa
Umma, Bw. Hab Mkwizu alipokuwa akikagua utendaji kazi wa Wakala katika maonesho
ya maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayofanyika katika Viwanja vya
Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.
Bw.
Mkwizu alisema kuwa kwa muda mrefu sasa wafanyabiashara wasio waaminifu
wamekuwa wakiitia hasara Serikali kwa kukwepa ulipaji wa kodi wa madini
yaendayo nje ya Tanzania kinyume na utaratibu uliowekwa.
“Hongereni
sana kwa kuweza kuokoa kiasi kikubwa cha madini yaliyokuwa yakisafirishwa bila
kufuata taratibu zetu za usafirishaji wa madini yaendayo nje ya Tanzania,”
alisema Bw. Mkwizu.
Naibu
Katibu Mkuu Mkwizu aliwasihi viongozi na watumishi wa Wakala kuongeza uchapaji
kazi na uzalendo ili kuweza kukomesha kabisa tabia ya wafanyabiashara hao wasio
waaminifu.
Akikaribishwa
kwenye banda la Wakala kwenye Viwanja vya Mnazi Mmoja na Afisa Habari wa Wakala
hiyo, Mhandisi Yisambi Shiwa, Bw. Mkwizu alijulishwa kuwa moja kati ya
mafanikio yaliyofikiwa na Wakala mara baada ya ukaguzi wa ziada kwa wasafiri
waendao nje ya Tanzania, ni pamoja na kubainika mamia ya wafanyabiashara wa
madini ambao wamekuwa wakitorosha kinyemela madini ya thamani kubwa ya fedha
bila kufuata taratibu.
“Katika
kuboresha utendaji kazi wa Wakala, tulitambulisha mpangokazi mpya wa ukaguzi wa
ziada katika viwanja vyetu vya ndege vikubwa vya Dar es Salaam, Kilimanjaro na
kile cha Mwanza lengo ni kubaini wafanyabiashara wasio waaminifu na ndipo
tulipobaini wizi huu,” alisema Mhandisi Shiwa.
Akizungumzia
thamani ya madini hayo, Mhandisi Shiwa alisema kuwa kufuatia ukaguzi huu, mpaka
sasa Wakala imeweza kuokoa madini yenye thamani ya zaidi ya shilingi za
kitanzania bilioni 15.
“Ukaguzi
huu umesaidia kuokoa kiasi kikubwa cha madini yenye thamani ya shilingi bilioni
15.3 hadi kufikia mwaka na hivyo kuiongezea serikali yetu mapato ambayo
yalikuwa yatoroshwe na wafanyabiashara hao wasio waaminifu,” aliongeza.
Kwa
mujibu wa Mhandisi Shiwa, kiasi hiki cha fedha ni sehemu ya mrahaba wa kisheria
unaostahili kuchangiwa na wafanyabiashara hao kwa umiliki wao wa madini hayo
kabla ya kusafirisha nje ya nchi.
Mhandisi
Shiwa aliongeza kuwa katika kuendelea kudhibiti tabia hizi, Wakala kwa
kushirikiana na taasisi nyingine za serikali imekuwa ikishikilia na kutaifisha
madini yanayotiliwa shaka ama kumilikiwa isivyo halali yanayopatikana katika
viwanja hivyo.
Wakala
wa Ukaguzi wa Madini Tanzania ni Wakala wa Serikali ulioanzishwa tarehe 2
Novemba, 2009 chini ya Sheria ya Wakala wa Serikali, Sura ya 245. Tamko la
Waziri la kuanzisha Wakala lilichapishwa kwenye Gazeti la Serikali Namba 362 la
tarehe 6 Novemba, 2009.
Lengo
la Wakala ni kuhakikisha kwamba, Serikali inapata mapato stahiki kutoka kwenye
shughuli za uzalishaji na biashara ya madini nchini kupitia usimamizi na
ukaguzi makini wa shughuli za uchimbaji, na kuhakikisha kuwa shughuli hizo
zinafanyika kwa kuzingatia uhifadhi na utunzaji thabiti wa mazingira katika
maeneo ya migodi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni