Na GORDON
KALULUNGA, MBEYA
WANAJIITA
Single Mother. Yaani walezi pekee. Wana umri kati ya miaka 14-25. Wanauza
vizibo vya soda na bia. Ndiyo maisha yao. Ni wasichana waliopata mimba wakiwa
masomoni wilaya ya Mbeya Jijini hapa.
Jamii
imekuwa ikiamini kuwa tatizo kubwa la wasichana lipo Vijijini, lakini wasichana
hawa wanasema huo siyo ukweli.
Wamejirejeshea
furaha ya maisha na kuuondoa unyonge wa kushushwa thamani na jamii. Jamii
inawaheshimu kutokana na uchumi walionao sasa. Mbali na kujutia kupata ujauzito
wakiwa masomoni.
Wanajutia
kukatishwa masomo, lakini wanasema hawana tena ndoto za kuajiriwa. Wamejiajiri
wenyewe. Wanalipana mishahara kwa masaa. Wanasema wameushinda unyonge wa uchumi.
Ni wasichana
Flora Mwapinga(22), Fausta James(23), Magreth Kalumyana, Halengo Zambwe na
Vaileth(22).
Wasichana
hao ni kati ya wengi ambao tayari ni wazazi. Lakini wamejivika ushujaa wa
kupamba na maisha kwa kujiinua kiuchumi.
Msichana
Frola Mwapinga, anatoa ujumbe mzito kwa wenzake kote nchini kwa kusema kuwa, kupata
mimba siyo mwisho wa maisha na kwamba wasichana wanaopata mimba wasijaribu
kujiua.
Anasema
alikuwa kidato cha pili mwaka 2008, katika shule ya Sekondari Hayombo iliyopo
pembezoni mwa Jiji la Mbeya, ndipo alipokutana na kijana wa kiume aliyemwita
mpenzi wake, kumbe alikuwa akihitaji ngono! ambaye alikuwa ni mtumishi wa kituo cha
mafuta.
Baada ya
mchezo wa ngono, alipata ujauzito! Alimweleza kijana huyo anayemwita(mpenzi wangu),
baada ya kusikia taarifa ya ujauzito, mwanaume huyo akaacha kazi akakimbia mji.
Anasema
wazazi wake walipotambua kuwa ana ujauzito, walimwambia kuwa asithubutu kutoa
mimba, kwa ahadi kuwa akijifungua atarejeshwa shuleni.
''Baada ya
kujifungua na mtoto kuendelea vizuri, wazazi wakanitafutia chuo cha Afya, nikaanza
kusoma, kumbe chuo hakikusajiliwa, serikali ikaja ikakifunga, nikarudi
nyumbani’’ anasema Frola.
Anaeleza
kuwa, wazazi wake hawakukata tamaa, wakamwambia kuwa atafute nafasi VETA.
Akafaya hivyo, akaambiwa aandike barua na kwenye barua kuwe na anuani ya
sanduku la posta, lakini kumbe sanduku la Posta alilokuwa ametumia kwenye
maombi, lilikuwa limefungwa! Hivyo hakuweza kupata majibu na muda ukawa
umeenda.
Akajiunga na
kampuni zinazosambaza vyakula kwenye sherehe ambako alipata akili ya kwenda
kujifunza masuala ya ujasiliamali na haki za watoto.
‘’Mwaka 2012
nilifika SIDO hapa hapa Mbeya, ambako nilikutana na mzungu aliyekuwa akiitwa
Yoko Imamula, ambaye baada ya kuona kipaji changu na baadhi ya wenzangu kuweza
kutengeneza heleni, Nectay, na mapambo mengine ya kike, tulimuomba atutafutie
masoko’’ anasema msichana huyo.
Anasema
Yoko, alikubali kufanya hivyo na kuamua kuwapiga picha na kupiga picha za
bidhaa zao na kutuma kwenye mitandao ambapo walianza kupata soko mkoani Arusha,
Iringa, Dar es Salaam na Japan.
Fausta
James, (Mama Patricia)(3), anaeleza kwa ujasiri huku akitabasamu kama
wafanyavyo wasichana wengine ambao bado wapo masomoni lakini wakiendelea na
mchezo wa Ngono.
Anasema
alikuwa na elimu ya matumizi ya njia ya uzazi wa mpango, lakini hakutaka
kutumia kwasababu hakuona umuhimu ili ajipime kuwa ni mwanamke kamili.
‘’Nilijua
sana njia za uzazi wa mpango, lakini ukiniambia suala la uzazi wa mpango mtu
ambaye sijazaa, nakushangaa! Nilikuwa nikitumia kalenda, ikanibwaga’’ anasema
Fausta.
Anasema
mwanaume aliyempa ujauzito ni Mwalimu Jijini Mbeya, ni mwenyeji wa mkoa wa
Tanga, alikataa ujauzito na kukimbia, lakini sasa amerejea na wana mahusiano
mema.
‘’Kuna watu
walikuja mtaani kwetu Nsalaga, wakatuhitaji tuliozalia nyumbani au walea pekee,
lakini wenzangu wengi hawakupenda kujitokeza. Tuliojitokeza wakatupa semina ya
kujiamini’’ anaeleza huku akitabasamu.
Kwa sasa
analima na kufanya biashara ya Mgahawa, huku akiwa mmoja wa wana kikundi cha
walea pekee kiitwacho Mama ubunifu.
Mwenyekiti
wa Kikundi cha Mama Ubunifu, ni Frola Mwapinga, anasema katika kikundi chao,
wapo wasichana 209.
Anatoa
ujumbe kwa wasichana wengine ambao wamezalia nyumbani kuwa ujauzito siyo mwisho
wa maisha yao, na wao katika kikundi chao wanatoa semina kwa wenzao wanaohitaji
kujazwa ujasiri.
‘’Tunawafundisha
jinsi ya kuanza kujiamini na kufanya kazi za ujasiliamali.
Mimi kwa sasa sihitaji kuajliwa wala kuolewa mpaka hapo mwanangu atakapokuwa mkubwa ingawa wanaume wengi wananihitaji kunioa baada ya kuwa na mwanga wa uchumi na ninamiliki mgahawa’’ anasema Mwenyekiti huyo wa walea pekee.
Mimi kwa sasa sihitaji kuajliwa wala kuolewa mpaka hapo mwanangu atakapokuwa mkubwa ingawa wanaume wengi wananihitaji kunioa baada ya kuwa na mwanga wa uchumi na ninamiliki mgahawa’’ anasema Mwenyekiti huyo wa walea pekee.
Mwalimu
Cecilia Ndele, anasema wanafunzi wa kike na kiume wamekuwa waathirika wakubwa
katika ndoa zenye migogoro na kufikia hatua ya talaka.
Anasema
wanandoa wanaotarakiana, watoto wao wanabeba mzigo wa kulea familia na
kushindwa kuhudhuria vema masomo huku baadhi ya watoto wa kike wakijiingiza
katika vitendo vya ngono za utototni.
‘’Maadili
yameporomoka, baadhi ni kutokana na Mama zao ambao wamekithiri kwa matusi na
malezi ya kuiga nchi za magharibi ndiyo maana leo hii watoto wa kike wenye
miaka 10-12 hawana bikra zao na wakiolewa wanaachika haraka’’ alisema Mwalimu
Cecilia Ndele.
Ripoti ya
wizara ya afya na ustawi wa jamii ya mwaka 2011 inaonyesha kwamba, asilimia 25 ya wanawake walio katika
umri wa kuzaa ambao wangependa kupumzika, kupangilia uzazi, hawatumii njia yoyote za uzazi wa mpango.
Akihutubia
Mkutano wa kimataifa wa uzazi wa mpango uliofanyika Juni mwaka 2012, London,
Uingereza, kwa uratibu wa asasi ya Bill and Melinda Gates Foundation na
serikali ya uingereza, Rais Jakaya Kikwete alisema kwasasa tiba zilizopo
zinawafikia wanawake milioni 2.4 nchini Tanzania.
Alisema
Tanzania inahitaji Sh bilioni 140 kusaidia kutekeleza mipango ya huduma ya
uzazi wa mpango kwa wanawake milioni 3.2 ifikapo mwaka 2015.
Utafiti wa
Shirika la afya Duniani (WHO) na (UNFPA), kuhusu masuala ya mimba za utotoni,
unaonyesha kuwa wasichana milioni 14 mpaka 15, wanakuwa tayari wana watoto kwa kila mwaka, hii ikionyesha kuwa ni sawa
na asilimia 10 ya uzazi
kwa dunia nzima.
Malengo ya
Milenia yaliyotamkwa na nchi 193
wanachama wa Umoja wa Mataifa (UN) mwaka 2005 mjini New York Marekani, yamelega
kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2015,
watoto wote wa kiume na wa kike waweze kumaliza masomo yao ya elimu ya msingi.
credit to;
Mwandishi wa
makala haya anapatikana kwa simu 0754 440749, barua pepe; kalulunga2006@gmail.com
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni