WAKAZI
jijini Mbeya, wametakiwa kuwa na bustani za mbogamboga ili kuweza kujikimu
kimaisha na kuimarisha afya zao na watoto wao.
Ushauri huo
umetolewa na Mratibu wa shirika lisilo la kiserikali la Anglican Church
dayosisi ya nyanda za juu kusini, Fadhili Nswilla, alipkuwa akizungumza na
waandishi wa habari jana, katika ukumbi wa Jiji la Mbeya.
Nswilla
alisema kuwa, kaya kuwa na kitalu cha mbogamboga, inapunguza utapiamlo kwa
jamii pamoja na umasikini wa chakula pale kaya husika inapokosa fedha za kununulia
mboga.
Alisema shirika
lake kwa kushirikiana na Pact Tanzania chini ya ufadhili wa USAID, wanatekeleza
mradi unaoitwa pamoja tuwalee, wenye lengo la kutete na kulea watoto wanaoishi
katika mazingira hatarishi.
“Jamii
ielewe kuwa suala la kulea watoto wanaoishi katika mazingira magumu siyo la
serikali pekee, bali ni la jamii” alisema Nswilla.
Alisema changamoto
kubwa wanayokumbana nayo katika kutekeleza mradi huo ambao unawajengea uwezo
wananchi na vikundi vya kulea watoto wanaoishi katika mazingira magumu badala
ya kuwapa fedha au vitu, ni pamoja na suala la wengi kutopenda kujinga.
“Tunaijengea
uwezo jamii kwa mujibu wa serikali ambapo jamii inapaswa kujitegemea na wala
siyo kupewa fedha ama vitu kama miradi mingine iliyopita, ambapo miradi ikiisha
wananchi walikuwa wakirudi kwenye umasikini uleule” alisema.
Aliisihi jamii
kuwa karibu na wahitaji ambapo kila mmoja akitimiza wajibu wake jamii
itaondokana na tatizo la watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi na
umasikini utapungua kwasababu ndani ya jamii kuna wataalam wa kila aina, wakiwemo
walimu, viongozi wa dini na wataalam wengine.
Mthamini na
mfuatiliaji wa mradi huo, Ebby Erasto, alisema Shirika la National youth
International Center(NICE), kwa kushirikiana na Anglican, wanatekeleza mpango
wa pili wa serikali wa kutoa stadi za kazi badala ya vitu kama ulivyokuwa
mpango wa kwanza wa serikali.
Alisema wanaiwezesha
kaya iliyokubali kupata stadi za maisha kujitegemea, ambapo mpaka sasa vikundi
21 vimeundwa na kuwezeshwa bure na kuwataka wafanyabiashara na wanajamii kwa
ujumla kuanza sasa kuona jukumu la kulea waishio mazingira hatarishi ni lao.
Kwa upande
wake afia ustawi wa jamii, Jijini Mbeya, Bupe Joel, alisema tatizo ni kubwa la
watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi jijini Mbeya, lakini tangu mwaka
2008 hajui takwimu sahihi katika eneo lake.
“Tatizo ni
kubwa sana, kwa mwaka 2006-2008 kwa kushirikiana na Pact, takwimu zilikuwa ni
watoto 18, 600 waliokuwa wakiishi katika mazingira hatarishi, lakini kwasasa
tunawategemea wenzetu hawa wa mashirika yasiyokuwa ya kiserikali yatuletee
takwimu za kipindi hiki’’ alisema Bupe Joel.
Mfanyabiashara
Jeremiah Mahenge, ambaye pia ni mmoja wa wadau walioalikwa kwenye kikao hicho,
alisema jamii ya watu wa mkoa wa Mbeya hawapendi kuhudhuria vikao vya msingi
vya kuhudumia jamii bali wengi wanapenda vikao vya harusi na kusahau kuwa
jukumu la kulea wahitaji ni la jamii nzima.
Aliyasema hayo
baada ya wadau wengine waliokuwa wamealikwa, kutohudhuria kikao hicho.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni