Mbunge wa
Viti maalum mkoa wa Mbeya, Dr. Mary Mwanjelwa, akimkabidhi mashuka Mkuu
wa Wilaya ya Kyela, Magreth Malenga na Mkurugenzi wa Halmashauri ya
wilaya hiyo, Clemens Kasongo, kabla ya kwenda kuwakabidhi wananchi
walioathirika na mafuriko mwaka huu 2014.
MBALI na Mbunge wa Jimbo la Kyela mkoani Mbeya, Dr,
Harrison Mwakyembe, kutoa misaada kwa waathirika wa mafuriko Jimboni humo, Mbunge wa viti maalum (CCM), Mkoa wa Mbeya,
Dr. Mary Mwanjelwa, naye amejitokeza na kutoa misaada ya kiutu kwa wananchi wa
wilaya hiyo.
Mbunge huyo wa viti maalum, alifika wilayani Kyela Mei
22, mwaka huu.
Akizungumza na wananchi katika Mkutano wa hadhara wa
Kijiji cha Nyerere, Dr. Mary Mwanjelwa, anasema mbali na kwamba mafuriko hayo
yameathiri kaya nyingi, lakini ana uhakika kuwa wanawake na watoto ndiyo
walioathirika zaidi.
“Maandiko yanasema lieni na wanaolia, najua wakati
mafuriko yanatokea wengine yamewakuta wakiwa wajawazito, ninyi siyo wakiwa,
tupo pamoja, nilipopata taarifa hii sikuweza kukaa na amani pale Bungeni,
nimeacha posho na kuja kuwapa pole ndugu zangu’’ anasema Dr.Mwanjelwa huku
akipiga magoti.
Diwani wa kata ya Bujonde, Paul Mwambafula, anamshukuru
Mbunge huyo kwa kusema Kata yake ndiyo kata iliyoathirika zaidi katika wilaya
hiyo ambapo kaya 2,400 zilikumbwa na mafuriko hayo, lakini kaya 1800,
ziliathirika zaidi.
Mwenyekiti wa Umoja wa wanawake Tanzania(UWT), Pricila
Mbwaga na Katibu wa UWT Mkoa wa Mbeya, Mariam Yusuph, waliwaambia wananchi wa
Kijiji cha Nyerere na Mpunguti kuwa, tatizo hilo siyo la kwao peke yao, maana
dunia imelisikia.
Mkuu wa wilaya ya Kyela, Magreth Malenga na Afisa tarafa
ya Unyakyusa, Kheri William, wanamshukuru Mbunge, Dr. Mwanjelwa kuwa mstari wa
mbele kujitoa kusaidia wenye uhitaji na kwamba kamati ya maafa ya wilaya hiyo,
itamalizia kusaidia kaya zilizoathirika katika Kijiji cha Nyerere.
Dr. Mwanjelwa alitoa mashuka 150 katika Vijiji vya
Nyerere na Mpunguti na kutoa wito kwa taasisi na watu binafsi kujitokeza
kuwasaidia wananchi wa wilaya hiyo walioathirika na mafuriko hayo.
Baadhi ya mashuka yalitolewa na benki ya NMB baada ya
Mbunge huyo kuiomba taasisi hiyo ya kifedha, ambayo mbali na mashuka,
ilimkabidhi madawati 83 kwa ajili ya shule za Msingi.
“Benki ya NMB inatoa huduma zake katika jamii ya watu
mbalimbali. Wanafunzi, watoto, watu wazima, wazee, mashirika na makampuni na
wateja mbalimbali. Sis kwetu hawa wote ni wadau ambao ndio wanafanya NMB
iendelee kuwepo’’ alisema Meneja wa NMB Kanda ya Nyanda za juu kusini, Lucresia
Makiriye.
Akishukuru kwa niaba ya wananchi wenzake wa Kijiji cha
Mpunguti, Mzee Water Butungulu, alienda mbali na kumweleza Dr. Mwanjelwa kuwa
endapo atawania nafasi ya Ubunge mwakani, atashinda kutokana na juhudi zake za kuhudumia jamii.
Mbali na msaada huo kwa waathirika wa mafuriko, Mbunge
huyo anasema ‘’Kuanzia mwaka 2010, kwa kukumbuka baadhi ya niliyoyafanya ni
pamoja na kujumuika na kuwasaidia yatima,
kusaidia vikundi vya akina mama na kufadhili semina za madiwani wa vyama
vyote juu ya utendaji bora’’ anasema Dr. Mwanjelwa.
Anaeleza kuwa ni mambo mengi ya jamii aliyoshiriki na
mengine ameyasahau lakini anakumbuka pia aligawa magodoro 250 katika hospital
za serikali katika wadi za wazazi wilaya ya Ileje, Mbozi, Chimala(Mbarali),
Ruanda na hospitali ya Rufaa ya Mbeya kitengo cha wazazi Meta Jijini Mbeya.
Sanjali na vitu hivyo, anasema kuwa alitoa pia viti vya
walemavu wa viungo katika Jiji la Mbeya mbele ya Askofu kiongozi wa kanisa la
Moravian Tanzania Alinikisa Cheyo siku alipokuwa akimshukuru Mungu kwa kumponya
na mauti katika ajali mbaya aliyoipata mwaka jana 2012.
Katika masuala ya uongozi, anasema aliendesha semina kwa
madiwani wa vyama vyote vya siasa na atazidi kufanya hivyo kwa kufadhili
mafunzo/semina za mara kwa mara kwa Madiwani wote wa Mkoa wa Mbeya, juu ya
Uongozi na uwajibikaji.
‘’Mbali na mafunzo ya madiwani hao, nimewahi kuendesha
mafunzo/semina kwa watendaji wote wa ngazi ya kata juu ya Uongozi na
uwajibikaji na nitazidi kufanya hivyo’’ anasema.
Kabla ya kujikita katika masuala ya siasa alikuwa
Mkurugenzi wa shirika la PSI Tanzania ambako historia haimuhukumu hata baada ya
kutoka huko kwa kile kinachojieleza kuwa alitoka na utumishi uliotukuka.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni