ELIMU ya
matumizi sahihi ya vyoo, mashimo ya taka na vichanja, inahitajika zaidi
Vijijini ili kupunguza magonjwa ya milipuko.
Hayo
yamebainika katika warsha ya wadau wa mpango wa usafi wa Mazingira(WASH),
kutoka wilaya za Mbeya na Mbarali, iliyofanyika eneo la Mbalizi ukumbi wa
Tughimbe, uliopo wilaya ya Mbeya Vijijini mkoani hapa.
Wadau hao
walitembelea katika kata za Ihahi iliyopo wilaya ya Mbarali na kata ya Mshewe
iliyopo wilaya ya Mbarali, na kujionea vyoo vya baadhi ya wananchi ambapo
walikuta baadhi ya kaya hazina vyoo.
Katibu tawala
msaidizi-Maji, ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Mbeya Mhandisi, Fredius Magige, alisema
maafisa afya kwa kushirikiana na watendaji wa vijiji na kata, wanatakiwa
kupeleka kikamilifu elimu hiyo kwa wananchi mara kwa mara ikiwa ni pamoja na
ufuatiliaji.
‘’Kwa kuwa
imebainika kuwa wahudumu wa afya ya msingi ya jamii(WAV) ni watu muhimu, ni
vema wakatumika vizuri lakini kama wanajitolea bila kulipwa hawataweza kufanya
kazi zao vizuri’’ alisema Mhandisi, Magige.
Akiwasilisha
taarifa ya utafiti wa kundi la kwanza uliofanyika katika kijiji cha Mjele kata
ya Mshewe, Afisa Afya wilaya ya Mbarali, Emedan Mgode, alisema;‘’Kijiji kina
kaya 418, katika vyoo, maji na sabuni ya kunawia hakuna na kaya 117 zina
matarajio ya kuwa na vyoo bora na kaya 38 hazina vyoo kabisa’’ alisema Mgode.
Alisema
walitembelea pia shule ya Msingi Itega yenye wanafunzi 334, na hali halisi ya miundombinu ya shule hiyo siyo
mizuri na uwiano wa matundu ya vyoo kwa wasichana ni 1 ya 60 na wavulana ni 1
ya 153.
‘’Vyoo hivyo
havina sakafu inayosafishika wala havina falagha, pia vina harufu na havina
maji ya kunawa kutokana na tatizo la maji katika eneo hilo na vyoo vya walimu
pia havina falagha wala maji ya kunawa mikono’’ alisema.
Alibainisha
changamoto inayokikumba kijiji hicho kuwa ni tatizo la maji ambayo yanapatikana
katika mto songwe umbali wa kilometa 10 kutoka kijijini hapo, hivyo suala la
kutumia maji katika hatua nne muhimu za kunawa mikono ambazo ni wakati wa
kutoka chooni, kabla na baada ya kula na baada ya kumuhudumia mgonjwa na
wakakati wa kumuhudumia mtoto inakuwa vigumu.
Alitoa ushauri
kuwa watu au jamii ihamasishwe juu ya uvunaji wa maji ya mvua katika kaya na
taasisi na jamii iendelee kuhamasishwa kujenga vyoo vyenye faragha au usiri
vilivyoezekwa na kuwekewa milango.
Naye Afisa
elimu ufundi wilaya ya Mbeya, Florence Mbwele, aliwasilisha taarifa ya ziara ya
kata ya Ihahi, akisema kuwa katika ziara yao walijionea hali mbaya ya vyoo hasa
kwa jamii za wafugaji.
‘’Changamoto
zilizochangia uchelewaji wa utekelezaji wa mpango wa WASH, ni pamoja na uhaba
wa maji, vyoo havina viwango, jamii ya wafugaji haijawafikiwa na elimu ya
matumizi ya vyoo na watendaji wana uhaba wa vitendea kazi’’ alisema Florence.
Alisema hali
halisi ni kwamba kuna mwitikio wa wastani kuhusu masuala ya afya na usafi wa
mazingira ikiwemo maofisini tofauti na hali mbaya iliyopo kwa jamii za
wafugaji.
‘’Kuhusu
elimu ya matumizi ya kibuyu chilizi(maji ya kunawa yanayotiririka) jamii
imeipokea lakini imeeleweka tofauti, ambapo wanatoboa garoni kwa chini hivyo
wakiweka maji yote yanaisha kabla ya kutumia’’ alisema mwasilishaji huyo.
Alisema
kunahitajika nguvu ya ziada katika jamii za wafugaji kwasababu katika ziara
hiyo walikosa hata mtu wa kutoa ushirikiano kupata taarifa na walipofika kwenye
nyumba moja, mwenyeji alipoona gari aliingia ndani na kujifungia.
Wakichangia
katika warsha hiyo, Afisa afya msaidizi wa kata ya Ihahi, Khatibu Kilumbu,
alisema kuwa katika kata yake wamejiwekea mikakati ya kuendelea kutoa elimu kwa
wananchi, kufanya mashindano ya usafi na kwamba ni wakati muhafaka kwa viongozi
wote kuwa na mipango na tathimini shirikishi kuhusu suala la usafi wa
mazingira.
Afisa afya
mkoa wa Mbeya, Salehe Mwango, alisema kuwa katika kijiji cha Mjele kuna udhaifu
wa mashimo ya takataka, ambapo mashimo yapo lakini hayatumiki hivyo aliwataka
viongozi wa eneo hilo kufanyia kazi jambo hilo.
Afisa
Mtendaji wa Kijiji cha Mjele, Evarist, alisema jamii ina elimu ya masuaa ya
usafi lakini haitaki kuitikia na katika suala la ujenzi wa vyoo vyenye kuta za
nyasi katika eneo lake alisema ni kutokana na kijiji hicho kutokuwa na maji hivyo
wanashindwa kufyatua tofali.
Kuhusu
tatizo la upatikanaji wa takwimu sahihi kutoka kwenye kata na vijiji, Afisa
Afya wilaya ya Mbeya, Emmanuel Mwaigugu, alisema kuwa ni kutokana na uhaba wa
watumishi wa sekta ya afya akitolea mfano katika wilaya yake kuwa katika kata
za Ilungu, Ilembo na Iwiji hakuna watendaji wa idara yake.