
Rais
 wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete 
ameunda Tume ya Uchunguzi (Commission Inquiry) Kuhusu Vitendo 
vilivyotokana na Uendeshaji wa Operesheni Tokomeza. 
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Dar Es Salaam jioni
 ya Ijumaa, Mei 2, 2014 na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue, 
Rais ameunda Tume hiyo kwa mujibu wa kifungu cha tatu cha Sheria ya 
Uchunguzi Sura ya 32.
Kutokana
 na hatua yake ya kuunda Tume hiyo, Rais Kikwete amemteua Mheshimiwa 
Jaji na Balozi Mstaafu Hamisi Amiri Msumi kuwa Mwenyekiti wa Tume hiyo.
Aidha,
 Rais Kikwete amewateua Mheshimiwa Jaji Mstaafu Stephen Ernest Mtashiwa 
Ihema na Mheshimiwa Jaji Mstaafu Vincent Kitubio Damian Lyimo kuwa 
Makamishna. 
Taarifa ya Balozi Sefue inasema kuwa uteuzi huu ulianza jana, Alhamisi, Mei Mosi 2014.
Taarifa ya Balozi Sefue iliyataja majukumu ya Tume hiyo yatakuwa yafuatayo:
Kuchunguza na kubaini Operesheni Tokomeza ilivyoendeshwa.
Kuchunguza na kubaini iwapo Sheria, Kanuni, Taratibu na Hadidu za Rejea zilifuatwa na watu waliotekeleza Operesheni Tokomeza.
Kuchunguza na kubaini iwapo yupo mtu yeyote aliyekiuka Sheria, Taratibu na Hadidu za Rejea wakati wa Operesheni Tokomeza.
Kuchunguza
 na kubaini kama wapo watu wowote waliokiuka Sheria yoyote wakati wa 
utekelezaji wa Operesheni Tokomeza na kupima kama hatua zilizochukuliwa 
dhidi yao au mali zao zilikuwa stahiki.
Kupendekeza
 hatua zozote zinazopaswa kuchukuliwa dhidi ya mtu yeyote atakayebainika
 kukiuka Sheria, Taratibu na Hadidu za Rejea za Operesheni Tokomeza.
Kupendekeza mambo ya kuzingatiwa wakati wa kuandaa na kutekeleza operesheni nyingine siku zijazo ili kuepuka kasoro.
Uteuzi
 huo wa Tume hiyo unatekeleza ahadi ya Rais Kikwete ambayo aliitoa 
wakati anahutubia Bunge Novemba 18, mwaka jana, 2013 mjini Dodoma.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
 
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni