Ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za
Serikali (CAG) iliyotolewa hivi karibuni imebainisha kuwepo kwa kiasi kikubwa
cha fedha za miradi ya UKIMWI ambazo hazikutumika kwa mwaka wa fedha 2013/14.
Jumla ya Halmashauri 58 zimeshindwa kutumia kiasi cha shilingi bilioni 2.3 za Tanzania.
Kiasi kingine cha fedha za VVU na UKIMWI
ambacho hakikutumika ni shilingi milioni 624.49 za Mradi wa Taifa wa Kudhibiti
UKIMWI (NACP), shilingi milion 307.2 za
Tume ya Taifa ya Kudhibiti UKIMWI (TACAIDS) pamoja na milioni
428.49 za Tanzania zilizotengwa kwa TAMISEMI. Inasikitisha kuona kwamba kiasi
hiki kikubwa cha fedha hakikutumika wakati utoaji wa huduma za VVU na UKIMWI ukikabiliwa
na changamoto nyingi. Kama CAG alivyoainisha, hali hii inasababisha
kutokukamilika ama kutokutekelezwa kabisa kwa shughuli zilizopangwa.
Baadhi ya sababu za kutotumika kwa kiasi hicho
cha fedha zilitajwa na CAG kuwa ni ucheleweshwaji wa fedha kutoka Hazina na urasimu
katika matumizi ya fedha za miradi kwenye halmashauri. Inahuzunisha kwamba haya
yanatokea wakati bado kuna uhitaji mkubwa wa huduma za VVU na UKIMWI katika
jamii.
Mapema mwaka huu, vyombo vya habari viliripoti
kuwepo kwa uhaba mkubwa wa dawa za kupunguza makali ya VVU (ARVs) hususani
katika mikoa ya Dar es salaam, Kilimanjaro and Mara. Sikika pia ilibaini upungufu
wa dawa hususan Combivir na Septrin katika baadhi ya vituo wilayani
Iramba, huku mkoa wa Manyara ukiripotiwa kuwa na tatizo
kubwa la ucheleweshwaji wa usambazaji wa dawa kutoka MSD. Katika mkoa wa Dar es
Salaam, baadhi ya Watu wanaoishi na VVU (WAVIU) waliripoti kubadilishiwa dawa
bila kupewa maelezo na wahudumu wa afya. Wakati huohuo, baadhi ya watoa huduma
katika wilaya ya Ilala walieleza kuwa iliwalazimu kutoa dawa za mwezi mmoja kwa
wagonjwa badala ya miezi miwili kama ilivyozoeleka kutokana na upungufu wa dawa
hizo katika vituo vyao.
Utafiti juu ya Maoni ya watumia huduma za VVU na UKIMWI uliochapishwa na Sikika mwaka
2013, ulionesha kuwa upungufu wa upatikanaji wa huduma za VVU na UKIMWI una athari
za moja kwa moja kwa WAVIU. Athari hizo
ni pamoja na gharama kubwa za usafiri kufuata huduma za afya, kukosa usiri
wakati wa kutoa ushauri nasaha kutokana na uhaba wa vyumba katika vituo vya huduma,
kutokuwepo kwa huduma endelevu za vipimo vya CD4 na wagonjwa kutozingatia
matibabu kunakochangiwa na uhaba wa dawa za ARVs.
Mkakati wa Tatu wa Taifa wa Kudhibiti UKIMWI Tanzania
(NMSF III) umetaja sababu za upatikanaji wa huduma duni za VVU na UKIMWI kuwa
ni uhaba na kutokuwa na uhakika wa fedha; umbali wa kufikia vituo vya huduma
hususan vijijini, hali inayochangia WAVIU kutohudhuria kliniki. Huduma tembezi
zimeanzishwa ili kupunguza tatizo la umbali wa kufika vituoni. Hata hivyo,
uhaba wa rasilimali unakwamisha utolewaji wa huduma hii. Upungufu wa ARVs na huduma za mashine za CD4
na miundombinu duni, kwa pamoja
vinaathiri matunzo, matibabu na misaada kwa WAVIU. Swali la kujiuliza ni: Kama nchi imeweka mkakati wa kuwezesha upatikanaji wa huduma bora za
viwango vya juu kama ilivyoainishwa katika NMSF III; na kama bado sekta
inakabiliwa na changamoto nyingi, kwanini basi kiasi hicho kikubwa cha fedha
hakikutumika?
Wadau wa maendeleo wanachangia kiasi kikubwa
cha rasilimali ili kusaidia utekelezaji wa shughuli za VVU na UKIMWI nchini.
Kwa mujibu wa NMSF III, sekta ya VVU na UKIMWI ni moja kati ya sekta zenye
utegemezi mkubwa wa fedha za wafadhili, takribani 97%. Kwa vile mchango wa
serikali katika huduma za VVU na UKIMWI ni mdogo; ufanisi kwenye matumizi na
usimamizi wa fedha hauna budi kupewa kipaumbele. Serikali inatakiwa ioneshe wananchi, mamlaka
za serikali za mitaa pamoja na wadau wa maendeleo ni kwa jinsi gani rasilimali
chache zilizopo zimetumika kwa ufanisi.
Tunatoa wito kwa Hazina kuhakikisha fedha
zinatolewa kwa wakati ili kuwezesha utekelezaji wa shughuli zilizopangwa.
Mamlaka za serikali za mitaa zitekeleze shughuli kulingana na mipango na bajeti
bila kuchelewa na TAMISEMI isimamie utekelezaji wa shughuli hizo ngazi ya
halmashauri. Hii itapunguza ama kumaliza tatizo la bakaa ya kiasi kikubwa cha fedha
mwishoni mwa mwaka. Kushindwa kutumia fedha za miradi ambazo asilimia kubwa
zimetolewa na wafadhili, tena kwa miaka
mitatu mfululizo si jambo la kufumbiwa macho; ni lazima hatua za haraka
zichukuliwe na watendaji wasiowajibika ni wawajibishwe.
Mr.
Irenei Kiria, Mkurugenzi wa Sikika, S.L.P 12183 Dar es Salaam,
Simu:
+255 222 666355/57, Nukushi: 2668015, Barua pepe: info@sikika.or.tz,
Twitter:
@sikika1, Facebook: Sikika Tanzania, Tovuti: www.sikika.or.tz
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni