IKIWA mkoa
wa Mbeya una asilimia 57 ya wajawazito wanaojifungulia hospitali na vituo vya
afya, wito umetolewa kwao kujitokeza kwa wingi kuhudhuria Kliniki ili kupunguza
vifo vya mama na mtoto.
Wito huo
umetolewa mwishoni mwa wiki na Mhadhiri, kaimu mkuu wa taasisi ya tiba ya St.
Aggrey Jijini Mbeya, Dr. Karim Segumba.
Dr. Karim
alisema kuwa faida wanazozipata wajawazito wanapohudhuria Kliniki ni pamoja na mjamzito
kuchunguzwa afya yake kwa undani, ikiwemo umri wa mimba, kimo cha mimba,
historia ya uzazi wa awali, uwingi wa damu, mkojo kwa protini na kutoa wasiwasi
wa kifafa cha mimba.
‘’Mwanamke
anachunguzwa shinikizo la damu, mlalo wa mtoto, mapigo ya moyo ya mtoto,
ikibidi ultrasound kuangalia kama mtoto yupo hai, au ni mlemavu, ukubwa wa
mtoto, kondo la nyuma la mama, kukomaa kwa mtoto, nyonga za mama kama
zinaruhusu kujifungua kwa njia ya kawaida au upasuaji na anaelezwa tarehe ya
makisio ya kujifungua’’ alisema Dr. Karim.
Mbali na
uchunguzi huo, alisema kuwa mjamzito anayehudhuria kliniki anapimwa pia VVU na
anapoonekana kuwa ana maambukizi anapewa mbinu za kumkinga mtoto aliye tumboni.
Alipoulizwa madhara
yanayoweza kuwapata wajawazito ambao hawaendi kliniki na hawajifungulii
hospitali na vituo vya afya, alisema ni pamoja na mjamzito kutoelewa maendeleo
ya mimba yake na hatari ambazo zingeweza kugundulika na kutatuliwa na wataalam
ili kuzuia kifo chake na mtoto.
‘’Hivyo ili
kupunguza vifo vya mama na mtoto ni muhimu wajawazito wakahudhuria kliniki na
kujifungulia katika vituo vya tiba na kizuri zaidi huduma zote hizo kwa mama
mjamzito na mtoto chini ya miaka mitano hutolewa bure kote nchini’’ alisema
mhadhili huyo.
Mratibu wa
huduma ya mama na mtoto katika hospitali ya mkoa wa Mbeya Prisca Butuyuyu,
alisema kwa sasa mkoa wa Mbeya, wajawazito wengi wanahudhuria kliniki lakini
wengi wao wanajifunguli nyumbani.
Aliitaja wilaya
ya Ileje kuwa ndiyo wilaya inayoongoza kwa wajawazito kujifungulia nyumbani,
ambapo Jiji la Mbeya linaongoza kwa wajawazito wengi kujifungulia katika vituo
vya tiba.
‘’Zaidi ya
asilimia 40 wajawazito wanajifungulia nyumbani lakini baadhi wanajifungulia kwa
wakunga wa jadi na njiani ingawa hatuna takwimu sahihi zaidi’’ alisema
Butuyuyu.
Alisema Jiji
la Mbeya wajawazito wanajifungulia hospitali hasa hospitali ya wazazi Meta kwa
asilimia 109, Kyela 67, Chunya 58, Rungwe 55, Mbozi 45, Mbeya Vijijini asilimia
38 na wilaya ya Ileje asilimia 33.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni