Ijumaa, 31 Julai 2015


Ripoti ya Twaweza: Asilimia 50 ya Wanafunzi S/Msingi nchini hawajui kusoma kwa Kiswahili

 
MATOKEO ya ripoti ya nne yaliyofanywa na taasisi ya Twaweza kuhusu uwezo wa kila mtoto nchini anayesoma darasa la 3 au zaidi kati ya wenye umri wa miaka (7-17) kupaswa kuwa na uwezo wa kusoma na kuandika kwa kiwango cha darasa 2, umebaini kwamba lengo hilo halijafikiwa katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita kwani asilimia 50% ya watoto hao hawajui kusoma kwa lugha ya kiswahili na asilimia 80% hawajui kusoma Kiingereza.
Ripoti hiyo iliyozinduliwa Dar es Salaam leo Julai 29, 2015, inaonyesha kwamba uwezo huo umebaki chini na kwa kiasi kikubwa haujabadilika hali ya uwezo wa kusoma ingawa uwezo wao wa hesabu umeonyesha kuboreka kidogo lakini watoto wengi wanakwenda shuleni lakini hawasomi kwa muda mrefu.
Akitoa matokea ya ripoti hiyo, Meneja wa Twaweza, Zaidi Magalla, (FikraPevu imepata nakala), ameeleza kuwa matokeo ya ripoti hiyo imebaini kwamba mtoto mmoja kati ya wanne wa darasa la tatu wanaweza kusoma hadithi ya darasa la pili kwa Kiswahili hadi wanapofikia darasa la tano ndipo wengi wa wanafunzi wanaweza kusoma kwa ngazi ya darasa la pili.
Sehemu ya ripoti hiyo inasema watoto wanne kati ya kumi wa darasa la tatu wamebainika kuwa wanaweza kuzidisha hesabu ngazi ya darasa la pili, wakati viwango vya ufaulu wa somo la hisabati katika utafiti wa mwaka 2012 vilikuwa juu zaidi kuliko miaka iliyopita.
“Kwa mfano 44% ya wanafunzi wa darasa la tatu walifaulu mtihani wa kuhesabu ikilinganishwa na asilimia 37% mwaka 2011. Hata hivyo, tathmini ya mwak 2012 haikuhusisah Wilaya Saba na matokeo haya yanahitaji kuthibitishwa zaidi katika miaka ijayo” alieleza sehemu ya ripoti hiyo.
Amesema kuwa umahiri katika kusoma na kufahamu hadithi kwa kiingereza bado uko chini katika maeneo mbalimbali nchini, kwani kwa mtoto mmoja kati ya kumi wa darasa la tatu imebainika kuwa wana uwezo wa kusoma hadithi ngazi ya darasa la pili kwa kiingereza huku tathmini ya Uwezo ya mwaka 2012 ikithibitisha kuwa viwango vya uelewa wa kiingereza katika kiwango cha msingi ni chini kwa kiasi kikubwa kuliko viwango vya uelewa kwa Kiswahili katika madarasa yote.
Ripoti-Twaweza
Taswira ya ripoti ya Taasisi hiyo
Takwimu za 2012 zilithibitisha wazi kati ya mikoa, Wilaya, mijini na vijijini katika matokeo ya watoto kujifunza imeonyesha kuwa watoto wanaoishi katika wilaya za mijini wamefanya vizuri kuliko watoto wanaoishi katika wilaya za vijijini.
Awali Mkurugenzi wa Twaweza, Aidan Eyakuze, alieleza kwamba tatizo la mahudhurio shule mbalimbali nchini ni tatizo kubwa kutokana na kasumba ya walimu kufika shuleni na kujaza daftari la mahudhurio bila kufundisha wanafunzi na kwamba tatizo hilo limepelekea asilimia 50% ya watoto kutojua kusoma kwa lugha ya kiswahili na asilimia 80% hawajui kusoma Kiingereza.
Afisa Programu wa Twaweza, Richard Temu, alieleza kuwa kumekuwepo na matokeo mabaya ya ufaulu kwa wanafunzi kwa familia maskini kabisa, familia zenye umaskini wa kati na matajiri na kwamba ili watoto hao waweze kupata elimu yenye tija ni wakati wa serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kuboresha mfumo wa elimu hususani katika sera mpya ya elimu iliyozinduliwa hivi karibuni Jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa Haki Elimu, John Kalage, akichangia katika ripoti hiyo amesema watoto wengi nchini hawasomi kutokana na sababu mbalimbali, ikiwa ni pamoja na motisha wa walimu wanaoupata kutoka serikali.
Amesema kwamba watoto wengi wanahudhuria shuleni lakini hawasomi, na wala hawawezeshwi na walimu ili kujua kusoma na kuandika. Amesema ili kuondoa tatizo hilo lazima rasilimali zote zifike kwa muda na kuunganisha nguvu kwa ngazi zote ili kutatua tatizo hilo.
Baadhi ya viongozi wa Twaweza wakishirikiana na wadau mbalimbali waliowezesha kupatikana kwa ripoti hiyo.
Baadhi ya viongozi wa Twaweza wakishirikiana na wadau mbalimbali waliowezesha kupatikana kwa ripoti hiyo.
Mathalani bendera ya taifa iliyopo kila mahali nchini hususani katika mazingira ya shule, watoto wengi hawaelewi maana ya rangi za bendera ambapo matokeo yanaonyesha kuwa asilimia 69% ya watoto wenye umri wa miaka 7-16 hawawezi kueleza maana ya rangi tatu za bendera na kwamba tofauti ipo kwa wale waliojiunga na shule na walio nje ya shule au kwa wale wa maeneo ya vijijini na mijini.

Alhamisi, 4 Juni 2015

LUTENGANO MWALWIBA (kulia), AKIWA NA MBUNGE VITI MAALUM MKOA WA MBEYA, DKT. MARY MWANJELWA


MAKUSANYO YA KAHAWA MKOANI YASHUKA






MAKUSANYO ya zao la kahawa mkoani Mbeya yameshuka kutoka tani 340 mwaka juzi hadi kufikia tani 120 mwaka jana kutokana na mgogoro wa kimaslahi ulioibuka kati ya Shirikisho la Vikundi vya Wakulima wa Kahawa Tanzania, SHIVIWAKA na baadhi ya wadau wa zao hilo.

Mwenyekiti wa SHIVIWAKA, Edward Masawe, alisema hali hiyo ilitokana na kampuni moja ya ununuzi wa kahawa mkoani hapa kuwarubuni baadhi ya wakulima waliokuwa wanachama wao na kusababisha kutouza kahawa yao kwa shirikisho hilo.

Masawe, alitoa taarifa hiyo wakati wa mkutano Mkutano wa mwaka wa shirikisho hilo ulioambatana na uchaguzi mkuu wa viongozi wake.

Alisema mgogoro huo wa kimaslahi ulitokana na msimamo wa SHIVIWAKA wa kuwahamasisha wakulima kutokubnali kuuza kahawa yao kwa bei nafuu kwa wanunuzi wanaotaka kuwanyionya wakulima hivyo kusababisha baadhi ya wanunuzi hao kulichukia shirikisho hilo.

“Kimsingi changamoto hii imetuathiri kwa kiasi kikubwa katika ununuzi wa kahawa kutoka kwa wakulima kwani baadhi yao walikataa kuuza kahawa yao kwa SHIVIWAKA na kuwauzia wengine na kusababisha makusanyo yetu kushuka ktoka tani 340 hadi 120.” Alisema Masawe.

Baadhi ya wakulima wa kahawa walisema wakulima wengi bado hawana ufahamu mzuri wa kubaini ujanja unaofanywa na wanunuzi katika kuwanyonya haki zao hivyo wamewashauri kuwa makini katika uuzaji wa kahawa yao.

Neema Mwaogoma, mkulima kutoka Mbozi alisema wakulima wengi wana haraka ya kuuza kahawa yao ili kujipatia pesa za haraka lakini hawachunguzi kwa makini bei zinazotolewa na wanunuzi hao.

Akitoa mfano, Neema, alisema katika msimu uliopita baadhi ya wakulima waliouza kahawa yao kwa wanunuzi binafsi waliuza kwa bei ya kati ya shilingi 3,000 hadi 3,500 kwa kilo moja wakati SHIVIWAKA ilinunua kahawa hiyo kwa bei ya shilingi 5,000.

Kutokana na hali hiyo, Masawe, alisema SHIVIWAKA imeweka mikakati ya kuwashawishi wakulima wa kahawa kuliamini shirikisho hilo na kuendelea kuliuzia zao hilo badala ya wanunuzi binafsi.

Miongoni mwa mikakati hiyo ni pamoja kufungua vituo vipya vua ununuzi wa kahawa katika maeneo ya wakuima, kuongeza bei ya zao hilo na kuimarisha mfumo wa uongozi wa shirikisho hilo.

Jumanne, 2 Juni 2015

HOTUBA YA PROF. MARK MWANDOSYA AKITANGAZA NIA MBEYA JANA TAREHE 1.6.2015, KATIKA VIWANJA VYA MKAPA HALL, HII HAPA.


PROFESA M. J. MWANDOSYA 

Nianze kuwa kumshukuru Mwenyezi Mungu,muweza wa yote kwa rehema nyingi alizotushushia kutuwezesha kuifikia siku hii ya leo.
 

Kwani hatukustahili zaidi ya wengi waliotutangulia mbele za haki. Nawashukuru ninyi nyote mliofika kuungana nami katika siku hii muhimu katika kukuza,kuimarisha na kuendeleza demokrasia ndani ya Chama chetu,Chama Cha Mapinduzi. 
 

Wazee wangu,  Waheshimiwa Maaskofu, Viongozi wa Dini na madhehebu mbalimbali,Waheshimiwa viongozi wa kimila,Waheshimiwa Machifu,Mama yangu Helena Mwaipasi, Mzee wangu Chifu Mwakibwili,akina mama,vijana,WanaCCM wenzangu,Viongozi wa vyama vya siasa,Wananchi,Wana Mbeya, Wajumbe wa NEC ya CCM Taifa,Wahashimiwa Wabunge wenzangu, Marafiki zetu kutoka Zanzibar,Watanzania wenzangu.
 

Asanteni sana kwa uwepo wenu, na pale popote mnapotusikiliza na kutuona.Nawashukuru. Nimehemewa.



Ndugu zangu, Kwa muda mrefu na kwa njia mbalimbali za mawasiliano mmekuwa mkinidadisi Mbona kimya kuhusu mwaka 2015? Pamoja na kwamba mliutaja mwaka tu, lakini niliwaelewa.
 

Wengi mliushangaa ukimya wangu.Pamoja na kwamba ukimya ni sehemu ya haiba yangu na daima nimeupokea kama ni karama aliyonitunuku Mwenyezi Mungu,Muweza wa yote,baadhi yenu niliwajibu " Ukimya una Kishindo"! 
 
 

Kuhusu Sultan Qabus wa Oman,mwandishi mmoja maarufu aitwae Robert Kaplan amemwelezea ifuatavyo: Ni mtu mkimya, mpole, hapendi kuzungumza na waandishi wa habari mara kwa mara, hapendi habari zake ziandikwe kwenye magazeti mara kwa mara,lakini ameibadilisha nchi ya Oman kutoka makundi hasimu ya makabila na kuwa taifa linaloheshimika na linaloendelea kwa kasi sana na kuwa mfano wa kuigwa...." Sijifananishi na Sultan Qabus, la hasha.
 
 

Isipokuwa najaribu kusisitiza kwamba mara nyingi ni bora katika maisha kuwa mjenga hoja na mtendaji makini kuliko kuwa  mpayukaji na mwenye maamuzi ya papo kwa papo yenye matokeo hasi na yenye hasara kwa taifa. 
 
 

Nimeenda nje kidogo ya mada yangu!


Kwa staili ya siku hizi wagombea watarajiwa huwa tunajitokeza na kusema : tutatangaza nia siku hii au ile! Nadhani tunawashangaza na mtuwie radhi. 


Kwani kwa kusema hivyo tunakua  tayari tumetangaza nia!Basi nami kwa staili hiyo hiyo naomba kutangaza rasmi mbele ya kadamnasi hii kama mashahidi,kwamba  kwa unyenyekevu mkubwa, nitaomba ridhaa ya kuchaguliwa kuwa mgombea wa nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. 
 

Natarajia kuendeleza rasmi safari niliyoianza leo kwa kuchukua fomu za maombi hayo pale Dodoma,Makao Makuu ya CCM, jumatano, tarehe 3 Juni,2015, saa 4 barabara.



Kipindi cha mpito kutoka awamu moja ya uongozi kwenda awamu nyingine kingekuwa kigumu sana kwa nchi nyingi hasa nchi zetu za kiafrika. Mifano iko wazi.Majirani zetu wamepata shida.Lakini waasisi wetu Hayati Mwalimu Nyerere na Hayati Abeid Amani Karume wametujengea misingi imara. 
 

Tuna kila sababu ya kuwashukuru na tuna kila sababu ya kujivunia misingi hiyo.

 
CCM haijayumba na CCM haitayumba. Baadhi ya wanachama inawezekana wameyumba. Hebu tuzirudie Ahadi za mwana CCM: binadamu wote ni ndugu zangu na Afrika ni moja; nitaitumikia nchi yangu na watu wake wote; nitajitolea nafsi yangu kuondoa umaskini, ujinga, magonjwa na dhuluma;rushwa ni adui wa haki sitapokea wala kutoa rushwa; cheo ni dhamana, sitatumia cheo changu wala cha mtu mwingine kwa faida yangu binafsi; nitajielimisha kadri ya uwezo wangu na kuitumia elimu yangu kwa faida ya wote; nitashirikiana na wenzangu wote kujenga nchi yetu; nitakuwa mwanachama mwaminifu wa CCM na raia mwema wa Tanzania na Afrika nzima; nitasema kweli daima fitna kwangu ni mwiko. Hii ndiyo CCM tunayoijua na atoaye ahadi mbele ya Mwenyezi Mungu ndiye Mwana CCM,na si vinginevyo.
 
 


Ahadi ya mwanaCCM ya kuondoa umaskini inanipa nafasi ya kuelezea na kusisitiza kipaumbele muhimu sana cha serikali iliyodhamiria kuwaondoa wananchi wake kutoka lindi la umasikini ni kukuza uchumi,uchumi wa kisasa,uliojikita katika misingi ya sayansi na teknolojia na kutumia teknolojia ya habari na mawasiliano kama kichocheo cha maendeleo hayo.
 
 

Kama sayansi na teknolojia  ndio msingi wa uchumi wa kisasa basi naweza kusema,tena kwa unyenyekevu mkubwa kwamba aliye mbele yenu ndiye pekee mwenye ujuzi,uelewa,na uzoefu wa masuala haya. 
 

Ninalotaka kusisitiza hapa ni kwamba kukuza na kusimamia uchumi ndio utakuwa kipaumbele namba moja. Jenga kwanza uchumi imara na mengine yatafuata.


Uchumi imara unajengwa hasa pale panapokuwa na lengo la kitaifa.Lengo katika Dira ya Taifa ya Maendeleo ni Tanzania kufikia nchi yenye kipato cha kati ifikapo mwaka 2025. 
 

Lengo hilo liliwekwa mwaka 2000. Tudhamiria sasa kwamba ifikapo mwaka 2030 Tanzania iwe nchi  za juu zenye kipato cha kati (High Middle Income),na kwamba ifikapo 2050 Tanzania iwe nchi iliyoendelea.
 


Tunawezaje kuyafikia malengo hayo? Tunawezaje kukuza uchumi na ukuaji huo uwe endelevu?Hili ndilo swali.
 

1.Kilimo cha kisasa na cha kisayansi kupitia matumizi zaidi na bora ya mbolea; kuendeleza utafiti kwa kuboresha miundombinu,vifaa, na kuendekeza rasilimali watu;kuboresha mifumo na aina ya mikopo kwa wakulima wadogo; kuboresha barabara za vijijini; kuendeleza ujenzi wa maghala kwa ajili ya kutunza nafaka;kuwa na migumo ya uhakika ya masoko ya mazao;na kuhakikisha kiwanda cha kimkakati cha mbolea itokanayo na gesi asilia kinajengwa haraka iwezekanavyo.
 

2.Kuanzisha na kuendeleza viwanda,kwa kuanzia viwanda vinavyoongeza thamani ya mazao na rasilimali asili
 

3.Kuendeleza kilimo cha umwagiliaji ili kuwa na uhakika wa upatikanaji wa chakula.
 

4.Kuendelea kusimamia kutengemaa kwa uchumi mpana
 

5.Kuondoa vikwazo vinavyozuia uwekezaji wa ndani na kutoka nje
 

6.Kuhakikisha sekta ya utalii inakuwa ipasavyo kwa kufungua fursa nyingi za utalii wa ndani na utalii katika sekta ya kusini.
 

7.Kuongeza tija katika utendaji wa kazi kwa kuthamini kazi (kufanya kazi kwa bidii,kwa uadilifu,na kwa kujituma), kusimamia kanuni,maadili na miiko ya utumishi wa umma na kuufanya utumishi wa umma usiwe wa mazoea tu bali wa ushindani unaopimika katika kutoa huduma kwa wananchi. Hii itakwenda sambamba na kulinda haki na kuboresha msilahi ya wafanyakazi.

 
8.Kuchukia,kuzuia na kupambana na ufisadi na rushwa. Kuondoa vikwazo vinavyoonekana kuwepo  kwa matabaka mawili ya wananchi; wale wanaoshughulikiwa na takukuru moja kwa moja,na wale ambao kibali kinahitajika kuwashtaki,kwa kuipa Takukuru uwezo wa kisheria kufanya kazi bila kuingiliwa na chombo chochote,wakati huohuo kuhakikisha haki za wananchi wema zinalindwa kupitia chombo cha kusimamia malalamiko (ombudsman).
 

9.Kuendeleza na ikibidi kuimarisha uhuru wa Benki Kuu  na uhuru wa vyombo vya udhibiti wa huduma za kiuchumi,mifuko ya jamii, bima.
 

10.Serikali kuwa injini ya ukuaji wa uchumi lakini kuweka mazingira mazuri kwa sekta binafsi,mtu mmoja,vikundi vya wajasiriamali,saccos,na kampuni binafsi kuchochea ukuaji wa uchumi.



Uchumi unapokua,basi serikali itakuwa katika nafasi nzuri ya kutekeleza vipaumbele katika maendeleo ya jamii: Elimu, maji safi na salama,afya, na miundombinu. Kuhusu elimu,lengo litakuwa ni kuboresha mitaala ili iendane na matumizi ya sayansi na teknolojia katika ngazi zote;kuhakikisha kila mtanzania ana nafasi sawa ya kujiendeleza kielimu kuanzia ngazi ya awali mpaka elimu ya juu; kuendeleza elimu ya ufundi na kilimo; kuandaa na kutekeleza mipango kwa hatua kuifanya elimu ya msingi ifikie kidato cha pili, cha nne na hatimaye kidato cha sita;kuongeza wingi wa udahili  wa wasichana katika katika ngazi ya elimu ya juu;kuboresha hali na ari ya utendaji wa  kazi kwa walimu,ikiwa ni pamoja na ujenzi nyumba za kuishi na kuongeza ujira.



Katika maeneo mengine ya huduma za kijamii,lengo la serikali litakuwa ni kutekeleza sera zilizopo na kuhakikisha malengo yanatekelezwa na yanapimika.Katika kuleta afya bora kwa wananchi lengo litakuwa ni kuweka mizania katika kuzuia na kupambana na magonjwa.



Uchumi hauwezi kukua pasipokuwa na amani na utulivu. Amani usalama na utulivu ni tunu.Waasisi wetu wametujengea msingi wa tunu hii. Viashiria vya kupotea kwa amani vinaanza kuonekana kutoka ndani na nje.


Hali inahitaji kuimarisha vyombo vyetu vya usalama katika maeneo yote hususan mafunzo,vitendea kazi,vifaa, miundombinu na silaha za kisasa.
 

Hatimaye ulinzi wa nchi unaanzia mwananchi mwenyewe.


Nafasi ya Zanzibar katika ukuaji wa uchumi wa Tanzania ni kubwa. Hii inatokana na asili na haiba ya nchi zenye visiwa, Zanzibar ikiwa mojawapo. Historia ya Zanzibar inatukumbusha hili.Kwani katika karne ya kumi na tisa Zanzibar iliongoza eneo lote la Afrika ya Mashariki kiuchumi na maendeleo,ukuondoa biashara ya utumwa.
 

Ilisemekana Ikipigwa zumari Zanzibar wanacheza ngoma maziwa makuu. Kila linalowezekana litafanywa kuondoa kabisa hali inayoweza kuikwaza Zanzibar kufikia uwezo wake mkubwa kiuchumi.Muungano utaimarika na uchumi wa Tanzania utakuwa kwa kasi zaidi.



Nahitimisha na suala muhimu la uzalendo.Kwa tafsiri isiyo rasmi,Uzalendo  ni upendo kwa nchi. Tumeanza kushuhudia kupungua kwa uzalendo. Upungufu huo unajionesha katika kuenzi tamaduni za nje,kubeza juhudi za maendeleo yaliyopatikana, viongozi kutoa matamshi yanayo kebehi nchi wakiwa nje ya nchi,kutojivunia historia yetu iliyojikita katika michango ya mashujaa wetu. Hawa ni pamoja na  wale waliopambana na wakoloni,akina Kinjeketile,  Mkwawa ,Mirambo, Chaburuma na wengineo ambao walitoa uhai wao kulinda na kutetea heshima ya mwafrika dhidi ya ukoloni.Aidha waasisi wa TANU,Hayati Mwalimu Nyerere,Sykes,Mzee Kawawa, na wenzao;
 

Waasisi wa Mapinduzi matukufu ya Zanzibar, Hayati Abeid Amani Karume na wenzake akina Mzee Thabit Kombo,Kanali Seif Bakari,Hamis Darwesh,Edington Kisasi,Yusuf Himpid,Said Washoto na wengineo;ambao walionesha upendo na uzalendo wa hali ya juu.Vilevile tuna mashujaa wa ukombozi wa Kusini mwa Afrika akina  Sebastian Chale,George Magombe na Hashim Mbita na wanajeshi wetu waliopoteza maisha yao katika mapambano ya ukombozi wa Afrika. 
 

Tutaendelea kuenzi, kuthamini,na kuiendeleza  mchango mikubwa wa Marais wetu wastaafu,Mzee Aboud Jumbe, Mzee Ali Hassan Mwinyi, Hayati Idris Abdulwakil,Dr Salmin Amour,Dr Amani Abeid Karume,na Mzee Benjamin William Mkapa.



Kipekee napenda kuwashukuru Marais wetu wa sasa; Mheshimiwa Dr Jakaya Mrisho Kikwete,Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,na Mheshimiwa Dr Ali Mohamed Shein ambao wamefanya kazi kubwa ya kuimarisha uchumi na umoja wa nchi yetu. Daima nitaenzi mchango wao.

 
Naishukuru familia yangu,Mke wangu Lucy,Watoto wetu Max, Sekela, na Emmanuel.Nawashukuru wazazi wangu ambao wametutangulia mbele za haki.
 

Wazee wa Mbeya na Lufilyo walionilea, Nawashukuru kwa michango yenu, ni baraka zitakazonifikisha Magogoni.


Tujivunie Nchi Yetu; na Kwa Pamoja Tutaijenga  Tanzania tunayoitaka.
 

Jumatatu, 1 Juni 2015

MWANAMKE MWENYE HEKIMA NI NGUZO YA FAMILIA NA TAIFA LENYE MAADILI MEMA.

MCHUJO WA SHINDANO LA MAMA SHUJAA WA CHAKULA 2015 WAANZA LEO JIJINI DAR

 Eluka Kibona, Meneja Utetezi na Ushawishi wa Oxfam akielezea juu ya shindano la Mama shujaa wa Chakula na kumkaribisha Mgeni Rasmi kufungua rasmi hafla ya Maamuzi ya fomu za shindano la Mama shujaa wa Chakula 2015 leo.
 Muwakilishi wa Mgeni Rasmi Mkurugenzi Mtendaji wa TBS Joseph Masikitiko  katika Hafla ya maamuzi ya fomu za shindano la mamashujaa wa Chakula Bi. Stella E. Mrosso ambaye ni Mkuu wa mahabara ya Chakula TBS akifungua rasmi hafla hiyo ya kuanza kuzihakiki fomu hizo .
 Mkurugenzi Mkazi wa Oxfam Tanzania Jane Foster akiwashukuru TBS , Majaji pamoja na washiriki ambao ndio watazipitia fomu hizo kabla hazijafika kwa majaji.
 Mratibu wa Programu kutoka Care International in Tanzania Maureen Kwilasa akisisitiza jambo wakati wa Hafla hiyo
Mkurugenzi Mkazi wa Oxfam Tanzania Jane Foster, Mkuu wa maabara chakula TBS Stella E. Mrosso, Tusfaye Legesse Obole President's Delivery Bureau, Manager Agriculture Productivity na  Mratibu wa Programu kutoka Care International in Tanzania Maureen Kwilasa wakiwa katika hafla hiyo.
 Mkuu wa maabara chakula TBS Stella E. Mrosso aliye Mwakilisha Mgeni rasmi katika hafla hiyo akimkabidhi rasmi fomu za shindano la mama shujaa wa chakula  Mkurugenzi Mkazi wa Oxfam Tanzania Jane Foster kwa ajili ya kuanza kufanya maamuzi.
Vijana wenye fani mbalimbali  kutoka vyuo vikuu na taasisi mbalimbali  wakiwa katika mchakato kwa kuzipitia Fomu zote za maombi ya kushiriki shindano la mama shujaa wa Chakula 2015
 ******
 Shindano la mama shujaa wa chakula limeingia katika hatua mpya baada ya zoezi la kukusanya fomu za washiriki kutoka mikoa mbalimbali nchini kupitiwa na majaji kwa ajili ya mchujo ambapo washiriki 18 watapatikana kisha baadaye 15 bora ambao wataingia kijijini kwa ajili ya mchakato wa kugombea nafasi ya mama shujaa wa chakula mwaka 2015.

zoezi la kusahihishwa fomu  limezinduliwa mapema leo hii na mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa TBS, Joseph Masikitiko ambaye ni Mkuu wa Maabara na Chakula TBS, Bi. Stella Mrosso akiwa sambamba na Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Oxfam Tanzania, Jenny Foster na majaji watakaopitia zoezi zima la mchujo wa fomu hizo.

 akizungumza na wageni waandishi wa habari katika uzinduzi huo Mkuu wa Maabara na Chakula, Bi. Stella Mrosso alilisifu shirika la Oxfam kuwa mstari wa mbele katika kupigania haki za wanawake, umiliki wa ardhi na kuhamasisha uzalishaji wa chakula kwa wazalishaji wadogo wadogo.

Bi. Stella alisisitiza kuwa kila mzalishaji anapaswa kuzalisha bidhaa bora ili kushindana na soko la ndani na la nje huku akifafanua kuwa kwa kupitia SIDO, TFDA na Wizara ya Afya, wazalishaji wadogowadogo watakuwa na uwezo wa kupata kibali kutoka TBS bure na kuongeza kuwa wakina mama nchini watumie shindano la mama shujaa wa Chakula kama chachu ya kujitokeza kwa wingi katika mashindano yanayofuata huku wengine wakijifunza uzalishaji bora kupitia mashindano hayo.

NAIBU WAZIRI WA KILIMO MHE MWANJELWA AMUAGIZA MRAJIS KUFANYA UCHUNGUZI SACCOS YA MADIBIRA-MBARALI NDANI YA SIKU 14

Naibu Waziri wa Wizara ya Kilimo, Mhe Mary Mwanjelwa akisisitiza jambo wakati akizungumza na Viongozi mbalimbali wa Mkoa na kamati ya uli...