Nianze kuwa kumshukuru Mwenyezi Mungu,muweza wa yote kwa
rehema nyingi alizotushushia kutuwezesha kuifikia siku hii ya leo.
Kwani
hatukustahili zaidi ya wengi waliotutangulia mbele za haki. Nawashukuru ninyi
nyote mliofika kuungana nami katika siku hii muhimu katika kukuza,kuimarisha na
kuendeleza demokrasia ndani ya Chama chetu,Chama Cha Mapinduzi.
Wazee wangu,
Waheshimiwa Maaskofu, Viongozi wa Dini na madhehebu
mbalimbali,Waheshimiwa viongozi wa kimila,Waheshimiwa Machifu,Mama yangu Helena Mwaipasi, Mzee wangu
Chifu Mwakibwili,akina mama,vijana,WanaCCM wenzangu,Viongozi wa vyama vya siasa,Wananchi,Wana Mbeya,
Wajumbe wa NEC ya CCM Taifa,Wahashimiwa Wabunge wenzangu, Marafiki zetu kutoka Zanzibar,Watanzania wenzangu.
Asanteni sana kwa uwepo wenu, na pale popote mnapotusikiliza
na kutuona.Nawashukuru. Nimehemewa.
Ndugu zangu, Kwa muda mrefu na kwa njia mbalimbali za mawasiliano mmekuwa
mkinidadisi Mbona kimya kuhusu mwaka 2015? Pamoja na kwamba mliutaja mwaka tu, lakini niliwaelewa.
Wengi
mliushangaa ukimya wangu.Pamoja na kwamba ukimya ni sehemu ya haiba yangu na daima nimeupokea kama ni karama
aliyonitunuku Mwenyezi Mungu,Muweza wa yote,baadhi yenu niliwajibu " Ukimya una Kishindo"!
Kuhusu Sultan
Qabus wa Oman,mwandishi mmoja maarufu aitwae Robert Kaplan amemwelezea ifuatavyo: Ni mtu mkimya, mpole, hapendi
kuzungumza na waandishi wa habari mara kwa mara, hapendi habari zake ziandikwe kwenye magazeti mara kwa mara,lakini
ameibadilisha nchi ya Oman kutoka makundi hasimu ya makabila na kuwa taifa linaloheshimika na linaloendelea kwa
kasi sana na kuwa mfano wa kuigwa...." Sijifananishi na Sultan Qabus, la hasha.
Isipokuwa najaribu kusisitiza kwamba mara
nyingi ni bora katika maisha kuwa mjenga hoja na mtendaji makini kuliko kuwa
mpayukaji na mwenye maamuzi ya papo kwa papo yenye matokeo hasi na yenye
hasara kwa taifa.
Nimeenda nje kidogo ya mada yangu!
Kwa staili ya siku hizi wagombea watarajiwa huwa
tunajitokeza na kusema : tutatangaza nia siku hii au ile! Nadhani tunawashangaza na mtuwie radhi.
Kwani kwa kusema hivyo
tunakua tayari tumetangaza nia!Basi nami
kwa staili hiyo hiyo naomba kutangaza rasmi mbele ya kadamnasi hii kama
mashahidi,kwamba kwa unyenyekevu mkubwa,
nitaomba ridhaa ya kuchaguliwa kuwa mgombea wa nafasi ya Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania.
Natarajia kuendeleza rasmi safari niliyoianza leo kwa kuchukua fomu za maombi hayo pale
Dodoma,Makao Makuu ya CCM, jumatano, tarehe 3 Juni,2015, saa 4 barabara.
Kipindi cha mpito kutoka awamu moja ya uongozi kwenda awamu
nyingine kingekuwa kigumu sana kwa nchi nyingi hasa nchi zetu za kiafrika. Mifano iko wazi.Majirani zetu wamepata shida.Lakini
waasisi wetu Hayati Mwalimu Nyerere na Hayati Abeid Amani Karume wametujengea misingi imara.
Tuna kila sababu ya
kuwashukuru na tuna kila sababu ya kujivunia misingi hiyo.
CCM haijayumba na CCM haitayumba. Baadhi
ya wanachama
inawezekana wameyumba. Hebu tuzirudie Ahadi za mwana CCM: binadamu wote
ni ndugu zangu na Afrika ni moja;
nitaitumikia nchi yangu na watu wake wote; nitajitolea nafsi yangu
kuondoa umaskini, ujinga, magonjwa na dhuluma;rushwa ni adui
wa haki sitapokea wala kutoa rushwa; cheo ni dhamana, sitatumia cheo
changu wala cha mtu mwingine kwa faida yangu binafsi; nitajielimisha
kadri ya uwezo wangu na kuitumia elimu yangu kwa faida ya wote;
nitashirikiana na wenzangu wote
kujenga nchi yetu; nitakuwa mwanachama mwaminifu wa CCM na raia mwema wa
Tanzania na Afrika nzima; nitasema kweli daima
fitna kwangu ni mwiko. Hii ndiyo CCM tunayoijua na atoaye ahadi mbele ya
Mwenyezi Mungu ndiye Mwana CCM,na si vinginevyo.
Ahadi ya mwanaCCM ya kuondoa umaskini
inanipa nafasi ya
kuelezea na kusisitiza kipaumbele muhimu sana cha serikali iliyodhamiria
kuwaondoa wananchi wake kutoka lindi la
umasikini ni kukuza uchumi,uchumi wa kisasa,uliojikita katika misingi ya
sayansi na teknolojia na kutumia teknolojia ya habari na mawasiliano
kama kichocheo cha maendeleo hayo.
Kama sayansi na teknolojia ndio
msingi wa uchumi wa kisasa basi naweza kusema,tena kwa unyenyekevu mkubwa
kwamba aliye mbele yenu ndiye pekee mwenye ujuzi,uelewa,na uzoefu wa masuala
haya.
Ninalotaka kusisitiza hapa ni kwamba kukuza na kusimamia uchumi ndio utakuwa kipaumbele namba moja. Jenga
kwanza uchumi imara na mengine yatafuata.
Uchumi imara unajengwa hasa pale panapokuwa na lengo la
kitaifa.Lengo katika Dira ya Taifa ya Maendeleo ni Tanzania kufikia nchi yenye kipato cha kati ifikapo mwaka 2025.
Lengo
hilo liliwekwa mwaka 2000. Tudhamiria sasa kwamba ifikapo mwaka 2030 Tanzania iwe nchi
za juu zenye kipato cha kati (High Middle Income),na kwamba ifikapo 2050
Tanzania iwe nchi iliyoendelea.
Tunawezaje kuyafikia malengo hayo? Tunawezaje kukuza uchumi
na ukuaji huo uwe endelevu?Hili ndilo swali.
1.Kilimo cha kisasa na cha kisayansi kupitia matumizi zaidi
na bora ya mbolea; kuendeleza utafiti kwa kuboresha miundombinu,vifaa, na kuendekeza rasilimali watu;kuboresha
mifumo na aina ya mikopo kwa wakulima wadogo; kuboresha barabara za vijijini; kuendeleza ujenzi wa maghala kwa ajili
ya kutunza nafaka;kuwa na migumo ya uhakika ya masoko ya mazao;na kuhakikisha kiwanda cha kimkakati cha mbolea
itokanayo na gesi asilia kinajengwa haraka iwezekanavyo.
2.Kuanzisha na kuendeleza viwanda,kwa kuanzia viwanda vinavyoongeza thamani ya mazao na rasilimali asili
3.Kuendeleza kilimo cha umwagiliaji ili kuwa na uhakika wa
upatikanaji wa chakula.
4.Kuendelea kusimamia kutengemaa kwa uchumi mpana
5.Kuondoa vikwazo vinavyozuia uwekezaji wa ndani na kutoka
nje
6.Kuhakikisha sekta ya utalii inakuwa ipasavyo kwa kufungua
fursa nyingi za utalii wa ndani na utalii katika sekta ya kusini.
7.Kuongeza tija katika utendaji wa kazi kwa kuthamini kazi (kufanya kazi kwa bidii,kwa uadilifu,na kwa kujituma), kusimamia kanuni,maadili na miiko ya utumishi wa umma na kuufanya
utumishi wa umma usiwe wa mazoea tu bali wa ushindani unaopimika katika kutoa huduma kwa wananchi. Hii itakwenda
sambamba na kulinda haki na kuboresha msilahi ya wafanyakazi.
8.Kuchukia,kuzuia na kupambana na ufisadi na rushwa. Kuondoa
vikwazo vinavyoonekana kuwepo kwa
matabaka mawili ya wananchi; wale wanaoshughulikiwa na takukuru moja kwa
moja,na wale ambao kibali kinahitajika kuwashtaki,kwa kuipa Takukuru uwezo wa kisheria kufanya kazi bila kuingiliwa na
chombo chochote,wakati huohuo kuhakikisha haki za wananchi wema zinalindwa kupitia chombo cha kusimamia malalamiko
(ombudsman).
9.Kuendeleza na ikibidi kuimarisha uhuru wa Benki Kuu na uhuru wa vyombo vya udhibiti wa huduma za
kiuchumi,mifuko ya jamii, bima.
10.Serikali kuwa injini ya ukuaji wa
uchumi lakini kuweka mazingira mazuri kwa sekta binafsi,mtu
mmoja,vikundi vya wajasiriamali,saccos,na kampuni binafsi kuchochea
ukuaji wa
uchumi.
Uchumi unapokua,basi serikali itakuwa katika nafasi nzuri ya
kutekeleza vipaumbele katika maendeleo ya jamii: Elimu, maji safi na salama,afya, na miundombinu. Kuhusu elimu,lengo
litakuwa ni kuboresha mitaala ili iendane na matumizi ya sayansi na teknolojia katika ngazi zote;kuhakikisha kila mtanzania
ana nafasi sawa ya kujiendeleza kielimu kuanzia ngazi ya awali mpaka elimu ya juu; kuendeleza elimu ya ufundi na kilimo;
kuandaa na kutekeleza mipango kwa hatua kuifanya elimu ya msingi ifikie kidato cha pili, cha nne na hatimaye kidato
cha sita;kuongeza wingi wa udahili wa
wasichana katika katika ngazi ya elimu ya juu;kuboresha hali na ari ya utendaji wa kazi kwa walimu,ikiwa ni pamoja na ujenzi
nyumba za kuishi na kuongeza ujira.
Katika maeneo mengine ya huduma za kijamii,lengo la serikali
litakuwa ni kutekeleza sera zilizopo na kuhakikisha malengo yanatekelezwa na yanapimika.Katika kuleta afya bora kwa
wananchi lengo litakuwa ni kuweka mizania katika kuzuia na kupambana na magonjwa.
Uchumi hauwezi kukua pasipokuwa na amani na utulivu. Amani
usalama na utulivu ni tunu.Waasisi wetu wametujengea msingi wa tunu hii. Viashiria vya kupotea kwa amani vinaanza
kuonekana kutoka ndani na nje.
Hali inahitaji kuimarisha vyombo vyetu vya usalama katika maeneo yote hususan
mafunzo,vitendea kazi,vifaa, miundombinu na silaha za kisasa.
Hatimaye ulinzi wa nchi unaanzia mwananchi mwenyewe.
Nafasi ya Zanzibar katika ukuaji wa uchumi wa Tanzania ni
kubwa. Hii inatokana na asili na haiba ya nchi zenye visiwa, Zanzibar ikiwa mojawapo. Historia ya Zanzibar inatukumbusha
hili.Kwani katika karne ya kumi na tisa Zanzibar iliongoza eneo lote la Afrika ya Mashariki kiuchumi na maendeleo,ukuondoa
biashara ya utumwa.
Ilisemekana Ikipigwa zumari Zanzibar wanacheza ngoma maziwa makuu. Kila linalowezekana litafanywa
kuondoa kabisa hali inayoweza kuikwaza Zanzibar kufikia uwezo wake mkubwa kiuchumi.Muungano utaimarika na uchumi wa
Tanzania utakuwa kwa kasi zaidi.
Nahitimisha na suala muhimu la uzalendo.Kwa tafsiri isiyo
rasmi,Uzalendo ni upendo kwa nchi.
Tumeanza kushuhudia kupungua kwa uzalendo. Upungufu huo unajionesha katika
kuenzi tamaduni za nje,kubeza juhudi za maendeleo yaliyopatikana, viongozi kutoa matamshi yanayo kebehi nchi
wakiwa nje ya nchi,kutojivunia historia yetu iliyojikita katika michango ya mashujaa wetu. Hawa ni pamoja na wale waliopambana na wakoloni,akina
Kinjeketile, Mkwawa ,Mirambo, Chaburuma na wengineo ambao walitoa uhai wao kulinda na
kutetea heshima ya mwafrika dhidi ya ukoloni.Aidha waasisi wa TANU,Hayati Mwalimu Nyerere,Sykes,Mzee Kawawa, na
wenzao;
Waasisi wa Mapinduzi matukufu ya Zanzibar, Hayati Abeid Amani Karume na wenzake akina Mzee Thabit Kombo,Kanali Seif
Bakari,Hamis Darwesh,Edington Kisasi,Yusuf Himpid,Said Washoto na wengineo;ambao walionesha upendo na uzalendo wa
hali ya juu.Vilevile tuna mashujaa wa ukombozi wa Kusini mwa Afrika akina
Sebastian Chale,George Magombe na Hashim Mbita na wanajeshi wetu
waliopoteza maisha yao katika mapambano ya ukombozi wa Afrika.
Tutaendelea kuenzi, kuthamini,na kuiendeleza mchango mikubwa wa Marais wetu wastaafu,Mzee
Aboud Jumbe, Mzee Ali Hassan Mwinyi, Hayati Idris Abdulwakil,Dr Salmin Amour,Dr
Amani Abeid Karume,na Mzee Benjamin William Mkapa.
Kipekee napenda kuwashukuru Marais wetu wa sasa; Mheshimiwa
Dr Jakaya Mrisho Kikwete,Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,na Mheshimiwa Dr Ali Mohamed Shein ambao
wamefanya kazi kubwa ya kuimarisha uchumi na umoja wa nchi yetu. Daima nitaenzi mchango wao.
Naishukuru familia
yangu,Mke wangu Lucy,Watoto wetu Max, Sekela, na Emmanuel.Nawashukuru wazazi
wangu ambao wametutangulia mbele za haki.
Wazee wa Mbeya na Lufilyo walionilea, Nawashukuru kwa michango yenu, ni baraka zitakazonifikisha Magogoni.
Tujivunie Nchi Yetu; na Kwa Pamoja Tutaijenga
Tanzania tunayoitaka.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni