Kuapishwa kwa mwanasheria huyo kunakuja ndani ya saa 24 baada ya Dk. Magufuli kuapishwa jana Novemba 5, 2015 kuwa Rais wa awamu ya tano wa Jamhuri ya Muungano, ambapo hapo jana muda mfupi baada ya kukabidhiwa madaraka kama Rais wa nchi aliweza kumteua Masaju kushika nafasi hiyo.
Taarifa ya Katibu Mkuu Kiongozi, Ombeni Sefue kwa waandishi wa habari jana Jijini Dar es Salaam, ilieleza kuwa Rais Magufuli atamuapisha mwanasheria huyo leo asubuhi ili kuanza majukumu yake mara moja kwa mujibu wa sheria.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju akila kiapo Ikulu Jijini Dar es Salaam mbele ya Rais John Magufuli
Katibu Mkuu Kiongozi alikaririwa na FikraPevu akisema pia kuwa Rais Magufuli atarajiwa kupendekeza jina la Waziri Mkuu ambalo litawasilishwa katika Bunge hilo jipya Novemba 19 ili lipigiwe kura.
Kabla ya uteuzi wake, Masaju alikuwa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya awamu ya nne baadae aliteuliwa kuwa Mwanasheria Mkuu baada ya aliyekuwa anashikilia nafasi hiyo Jaji Fredrick Werema kujiuzulu nafasi yake.
Jaji Werema alijiuzulu nafasi hiyo kutokana na sakata la Akaunti ya Tegeta Escrow kwa madai kuwa ushauri wake alioutoa kuhusu suala hilo haukueleweka na badala yake alichafua hali ya hewa.
Hata hivyo, Masaju pia amepata kuwa Mshauri wa Sheria wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika serikali ya awamu ya nne.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni