Alhamisi, 4 Juni 2015
MAKUSANYO YA KAHAWA MKOANI YASHUKA
MAKUSANYO
ya zao la kahawa mkoani Mbeya yameshuka kutoka tani 340 mwaka juzi hadi kufikia
tani 120 mwaka jana kutokana na mgogoro wa kimaslahi ulioibuka kati ya
Shirikisho la Vikundi vya Wakulima wa Kahawa Tanzania, SHIVIWAKA na baadhi ya
wadau wa zao hilo.
Mwenyekiti
wa SHIVIWAKA, Edward Masawe, alisema hali hiyo ilitokana na kampuni moja ya
ununuzi wa kahawa mkoani hapa kuwarubuni baadhi ya wakulima waliokuwa wanachama
wao na kusababisha kutouza kahawa yao kwa shirikisho hilo.
Masawe,
alitoa taarifa hiyo wakati wa mkutano Mkutano wa mwaka wa shirikisho hilo
ulioambatana na uchaguzi mkuu wa viongozi wake.
Alisema
mgogoro huo wa kimaslahi ulitokana na msimamo wa SHIVIWAKA wa kuwahamasisha
wakulima kutokubnali kuuza kahawa yao kwa bei nafuu kwa wanunuzi wanaotaka
kuwanyionya wakulima hivyo kusababisha baadhi ya wanunuzi hao kulichukia
shirikisho hilo.
“Kimsingi
changamoto hii imetuathiri kwa kiasi kikubwa katika ununuzi wa kahawa kutoka
kwa wakulima kwani baadhi yao walikataa kuuza kahawa yao kwa SHIVIWAKA na
kuwauzia wengine na kusababisha makusanyo yetu kushuka ktoka tani 340 hadi
120.” Alisema Masawe.
Baadhi
ya wakulima wa kahawa walisema wakulima wengi bado hawana ufahamu mzuri wa
kubaini ujanja unaofanywa na wanunuzi katika kuwanyonya haki zao hivyo
wamewashauri kuwa makini katika uuzaji wa kahawa yao.
Neema
Mwaogoma, mkulima kutoka Mbozi alisema wakulima wengi wana haraka ya kuuza
kahawa yao ili kujipatia pesa za haraka lakini hawachunguzi kwa makini bei
zinazotolewa na wanunuzi hao.
Akitoa
mfano, Neema, alisema katika msimu uliopita baadhi ya wakulima waliouza kahawa
yao kwa wanunuzi binafsi waliuza kwa bei ya kati ya shilingi 3,000 hadi 3,500 kwa
kilo moja wakati SHIVIWAKA ilinunua kahawa hiyo kwa bei ya shilingi 5,000.
Kutokana
na hali hiyo, Masawe, alisema SHIVIWAKA imeweka mikakati ya kuwashawishi
wakulima wa kahawa kuliamini shirikisho hilo na kuendelea kuliuzia zao hilo
badala ya wanunuzi binafsi.
Miongoni
mwa mikakati hiyo ni pamoja kufungua vituo vipya vua ununuzi wa kahawa katika
maeneo ya wakuima, kuongeza bei ya zao hilo na kuimarisha mfumo wa uongozi wa
shirikisho hilo.
Jumanne, 2 Juni 2015
HOTUBA YA PROF. MARK MWANDOSYA AKITANGAZA NIA MBEYA JANA TAREHE 1.6.2015, KATIKA VIWANJA VYA MKAPA HALL, HII HAPA.
Nianze kuwa kumshukuru Mwenyezi Mungu,muweza wa yote kwa
rehema nyingi alizotushushia kutuwezesha kuifikia siku hii ya leo.
Kwani
hatukustahili zaidi ya wengi waliotutangulia mbele za haki. Nawashukuru ninyi
nyote mliofika kuungana nami katika siku hii muhimu katika kukuza,kuimarisha na
kuendeleza demokrasia ndani ya Chama chetu,Chama Cha Mapinduzi.
Wazee wangu,
Waheshimiwa Maaskofu, Viongozi wa Dini na madhehebu
mbalimbali,Waheshimiwa viongozi wa kimila,Waheshimiwa Machifu,Mama yangu Helena Mwaipasi, Mzee wangu
Chifu Mwakibwili,akina mama,vijana,WanaCCM wenzangu,Viongozi wa vyama vya siasa,Wananchi,Wana Mbeya,
Wajumbe wa NEC ya CCM Taifa,Wahashimiwa Wabunge wenzangu, Marafiki zetu kutoka Zanzibar,Watanzania wenzangu.
Asanteni sana kwa uwepo wenu, na pale popote mnapotusikiliza
na kutuona.Nawashukuru. Nimehemewa.
Ndugu zangu, Kwa muda mrefu na kwa njia mbalimbali za mawasiliano mmekuwa
mkinidadisi Mbona kimya kuhusu mwaka 2015? Pamoja na kwamba mliutaja mwaka tu, lakini niliwaelewa.
Wengi
mliushangaa ukimya wangu.Pamoja na kwamba ukimya ni sehemu ya haiba yangu na daima nimeupokea kama ni karama
aliyonitunuku Mwenyezi Mungu,Muweza wa yote,baadhi yenu niliwajibu " Ukimya una Kishindo"!
Kuhusu Sultan
Qabus wa Oman,mwandishi mmoja maarufu aitwae Robert Kaplan amemwelezea ifuatavyo: Ni mtu mkimya, mpole, hapendi
kuzungumza na waandishi wa habari mara kwa mara, hapendi habari zake ziandikwe kwenye magazeti mara kwa mara,lakini
ameibadilisha nchi ya Oman kutoka makundi hasimu ya makabila na kuwa taifa linaloheshimika na linaloendelea kwa
kasi sana na kuwa mfano wa kuigwa...." Sijifananishi na Sultan Qabus, la hasha.
Isipokuwa najaribu kusisitiza kwamba mara
nyingi ni bora katika maisha kuwa mjenga hoja na mtendaji makini kuliko kuwa
mpayukaji na mwenye maamuzi ya papo kwa papo yenye matokeo hasi na yenye
hasara kwa taifa.
Nimeenda nje kidogo ya mada yangu!
Kwa staili ya siku hizi wagombea watarajiwa huwa
tunajitokeza na kusema : tutatangaza nia siku hii au ile! Nadhani tunawashangaza na mtuwie radhi.
Kwani kwa kusema hivyo
tunakua tayari tumetangaza nia!Basi nami
kwa staili hiyo hiyo naomba kutangaza rasmi mbele ya kadamnasi hii kama
mashahidi,kwamba kwa unyenyekevu mkubwa,
nitaomba ridhaa ya kuchaguliwa kuwa mgombea wa nafasi ya Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania.
Natarajia kuendeleza rasmi safari niliyoianza leo kwa kuchukua fomu za maombi hayo pale
Dodoma,Makao Makuu ya CCM, jumatano, tarehe 3 Juni,2015, saa 4 barabara.
Kipindi cha mpito kutoka awamu moja ya uongozi kwenda awamu
nyingine kingekuwa kigumu sana kwa nchi nyingi hasa nchi zetu za kiafrika. Mifano iko wazi.Majirani zetu wamepata shida.Lakini
waasisi wetu Hayati Mwalimu Nyerere na Hayati Abeid Amani Karume wametujengea misingi imara.
Tuna kila sababu ya
kuwashukuru na tuna kila sababu ya kujivunia misingi hiyo.
CCM haijayumba na CCM haitayumba. Baadhi
ya wanachama
inawezekana wameyumba. Hebu tuzirudie Ahadi za mwana CCM: binadamu wote
ni ndugu zangu na Afrika ni moja;
nitaitumikia nchi yangu na watu wake wote; nitajitolea nafsi yangu
kuondoa umaskini, ujinga, magonjwa na dhuluma;rushwa ni adui
wa haki sitapokea wala kutoa rushwa; cheo ni dhamana, sitatumia cheo
changu wala cha mtu mwingine kwa faida yangu binafsi; nitajielimisha
kadri ya uwezo wangu na kuitumia elimu yangu kwa faida ya wote;
nitashirikiana na wenzangu wote
kujenga nchi yetu; nitakuwa mwanachama mwaminifu wa CCM na raia mwema wa
Tanzania na Afrika nzima; nitasema kweli daima
fitna kwangu ni mwiko. Hii ndiyo CCM tunayoijua na atoaye ahadi mbele ya
Mwenyezi Mungu ndiye Mwana CCM,na si vinginevyo.
Ahadi ya mwanaCCM ya kuondoa umaskini
inanipa nafasi ya
kuelezea na kusisitiza kipaumbele muhimu sana cha serikali iliyodhamiria
kuwaondoa wananchi wake kutoka lindi la
umasikini ni kukuza uchumi,uchumi wa kisasa,uliojikita katika misingi ya
sayansi na teknolojia na kutumia teknolojia ya habari na mawasiliano
kama kichocheo cha maendeleo hayo.
Kama sayansi na teknolojia ndio
msingi wa uchumi wa kisasa basi naweza kusema,tena kwa unyenyekevu mkubwa
kwamba aliye mbele yenu ndiye pekee mwenye ujuzi,uelewa,na uzoefu wa masuala
haya.
Ninalotaka kusisitiza hapa ni kwamba kukuza na kusimamia uchumi ndio utakuwa kipaumbele namba moja. Jenga
kwanza uchumi imara na mengine yatafuata.
Uchumi imara unajengwa hasa pale panapokuwa na lengo la
kitaifa.Lengo katika Dira ya Taifa ya Maendeleo ni Tanzania kufikia nchi yenye kipato cha kati ifikapo mwaka 2025.
Lengo
hilo liliwekwa mwaka 2000. Tudhamiria sasa kwamba ifikapo mwaka 2030 Tanzania iwe nchi
za juu zenye kipato cha kati (High Middle Income),na kwamba ifikapo 2050
Tanzania iwe nchi iliyoendelea.
Tunawezaje kuyafikia malengo hayo? Tunawezaje kukuza uchumi
na ukuaji huo uwe endelevu?Hili ndilo swali.
1.Kilimo cha kisasa na cha kisayansi kupitia matumizi zaidi
na bora ya mbolea; kuendeleza utafiti kwa kuboresha miundombinu,vifaa, na kuendekeza rasilimali watu;kuboresha
mifumo na aina ya mikopo kwa wakulima wadogo; kuboresha barabara za vijijini; kuendeleza ujenzi wa maghala kwa ajili
ya kutunza nafaka;kuwa na migumo ya uhakika ya masoko ya mazao;na kuhakikisha kiwanda cha kimkakati cha mbolea
itokanayo na gesi asilia kinajengwa haraka iwezekanavyo.
2.Kuanzisha na kuendeleza viwanda,kwa kuanzia viwanda vinavyoongeza thamani ya mazao na rasilimali asili
3.Kuendeleza kilimo cha umwagiliaji ili kuwa na uhakika wa
upatikanaji wa chakula.
4.Kuendelea kusimamia kutengemaa kwa uchumi mpana
5.Kuondoa vikwazo vinavyozuia uwekezaji wa ndani na kutoka
nje
6.Kuhakikisha sekta ya utalii inakuwa ipasavyo kwa kufungua
fursa nyingi za utalii wa ndani na utalii katika sekta ya kusini.
7.Kuongeza tija katika utendaji wa kazi kwa kuthamini kazi (kufanya kazi kwa bidii,kwa uadilifu,na kwa kujituma), kusimamia kanuni,maadili na miiko ya utumishi wa umma na kuufanya
utumishi wa umma usiwe wa mazoea tu bali wa ushindani unaopimika katika kutoa huduma kwa wananchi. Hii itakwenda
sambamba na kulinda haki na kuboresha msilahi ya wafanyakazi.
8.Kuchukia,kuzuia na kupambana na ufisadi na rushwa. Kuondoa
vikwazo vinavyoonekana kuwepo kwa
matabaka mawili ya wananchi; wale wanaoshughulikiwa na takukuru moja kwa
moja,na wale ambao kibali kinahitajika kuwashtaki,kwa kuipa Takukuru uwezo wa kisheria kufanya kazi bila kuingiliwa na
chombo chochote,wakati huohuo kuhakikisha haki za wananchi wema zinalindwa kupitia chombo cha kusimamia malalamiko
(ombudsman).
9.Kuendeleza na ikibidi kuimarisha uhuru wa Benki Kuu na uhuru wa vyombo vya udhibiti wa huduma za
kiuchumi,mifuko ya jamii, bima.
10.Serikali kuwa injini ya ukuaji wa
uchumi lakini kuweka mazingira mazuri kwa sekta binafsi,mtu
mmoja,vikundi vya wajasiriamali,saccos,na kampuni binafsi kuchochea
ukuaji wa
uchumi.
Uchumi unapokua,basi serikali itakuwa katika nafasi nzuri ya
kutekeleza vipaumbele katika maendeleo ya jamii: Elimu, maji safi na salama,afya, na miundombinu. Kuhusu elimu,lengo
litakuwa ni kuboresha mitaala ili iendane na matumizi ya sayansi na teknolojia katika ngazi zote;kuhakikisha kila mtanzania
ana nafasi sawa ya kujiendeleza kielimu kuanzia ngazi ya awali mpaka elimu ya juu; kuendeleza elimu ya ufundi na kilimo;
kuandaa na kutekeleza mipango kwa hatua kuifanya elimu ya msingi ifikie kidato cha pili, cha nne na hatimaye kidato
cha sita;kuongeza wingi wa udahili wa
wasichana katika katika ngazi ya elimu ya juu;kuboresha hali na ari ya utendaji wa kazi kwa walimu,ikiwa ni pamoja na ujenzi
nyumba za kuishi na kuongeza ujira.
Katika maeneo mengine ya huduma za kijamii,lengo la serikali
litakuwa ni kutekeleza sera zilizopo na kuhakikisha malengo yanatekelezwa na yanapimika.Katika kuleta afya bora kwa
wananchi lengo litakuwa ni kuweka mizania katika kuzuia na kupambana na magonjwa.
Uchumi hauwezi kukua pasipokuwa na amani na utulivu. Amani
usalama na utulivu ni tunu.Waasisi wetu wametujengea msingi wa tunu hii. Viashiria vya kupotea kwa amani vinaanza
kuonekana kutoka ndani na nje.
Hali inahitaji kuimarisha vyombo vyetu vya usalama katika maeneo yote hususan
mafunzo,vitendea kazi,vifaa, miundombinu na silaha za kisasa.
Hatimaye ulinzi wa nchi unaanzia mwananchi mwenyewe.
Nafasi ya Zanzibar katika ukuaji wa uchumi wa Tanzania ni
kubwa. Hii inatokana na asili na haiba ya nchi zenye visiwa, Zanzibar ikiwa mojawapo. Historia ya Zanzibar inatukumbusha
hili.Kwani katika karne ya kumi na tisa Zanzibar iliongoza eneo lote la Afrika ya Mashariki kiuchumi na maendeleo,ukuondoa
biashara ya utumwa.
Ilisemekana Ikipigwa zumari Zanzibar wanacheza ngoma maziwa makuu. Kila linalowezekana litafanywa
kuondoa kabisa hali inayoweza kuikwaza Zanzibar kufikia uwezo wake mkubwa kiuchumi.Muungano utaimarika na uchumi wa
Tanzania utakuwa kwa kasi zaidi.
Nahitimisha na suala muhimu la uzalendo.Kwa tafsiri isiyo
rasmi,Uzalendo ni upendo kwa nchi.
Tumeanza kushuhudia kupungua kwa uzalendo. Upungufu huo unajionesha katika
kuenzi tamaduni za nje,kubeza juhudi za maendeleo yaliyopatikana, viongozi kutoa matamshi yanayo kebehi nchi
wakiwa nje ya nchi,kutojivunia historia yetu iliyojikita katika michango ya mashujaa wetu. Hawa ni pamoja na wale waliopambana na wakoloni,akina
Kinjeketile, Mkwawa ,Mirambo, Chaburuma na wengineo ambao walitoa uhai wao kulinda na
kutetea heshima ya mwafrika dhidi ya ukoloni.Aidha waasisi wa TANU,Hayati Mwalimu Nyerere,Sykes,Mzee Kawawa, na
wenzao;
Waasisi wa Mapinduzi matukufu ya Zanzibar, Hayati Abeid Amani Karume na wenzake akina Mzee Thabit Kombo,Kanali Seif
Bakari,Hamis Darwesh,Edington Kisasi,Yusuf Himpid,Said Washoto na wengineo;ambao walionesha upendo na uzalendo wa
hali ya juu.Vilevile tuna mashujaa wa ukombozi wa Kusini mwa Afrika akina
Sebastian Chale,George Magombe na Hashim Mbita na wanajeshi wetu
waliopoteza maisha yao katika mapambano ya ukombozi wa Afrika.
Tutaendelea kuenzi, kuthamini,na kuiendeleza mchango mikubwa wa Marais wetu wastaafu,Mzee
Aboud Jumbe, Mzee Ali Hassan Mwinyi, Hayati Idris Abdulwakil,Dr Salmin Amour,Dr
Amani Abeid Karume,na Mzee Benjamin William Mkapa.
Kipekee napenda kuwashukuru Marais wetu wa sasa; Mheshimiwa
Dr Jakaya Mrisho Kikwete,Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,na Mheshimiwa Dr Ali Mohamed Shein ambao
wamefanya kazi kubwa ya kuimarisha uchumi na umoja wa nchi yetu. Daima nitaenzi mchango wao.
Naishukuru familia
yangu,Mke wangu Lucy,Watoto wetu Max, Sekela, na Emmanuel.Nawashukuru wazazi
wangu ambao wametutangulia mbele za haki.
Wazee wa Mbeya na Lufilyo walionilea, Nawashukuru kwa michango yenu, ni baraka zitakazonifikisha Magogoni.
Tujivunie Nchi Yetu; na Kwa Pamoja Tutaijenga
Tanzania tunayoitaka.
Jumatatu, 1 Juni 2015
MCHUJO WA SHINDANO LA MAMA SHUJAA WA CHAKULA 2015 WAANZA LEO JIJINI DAR
Eluka
Kibona, Meneja
Utetezi na Ushawishi wa Oxfam akielezea juu ya shindano la Mama shujaa
wa Chakula na kumkaribisha Mgeni Rasmi kufungua rasmi hafla ya Maamuzi
ya fomu za shindano la Mama shujaa wa Chakula 2015 leo.
Muwakilishi
wa Mgeni Rasmi Mkurugenzi Mtendaji wa TBS Joseph Masikitiko katika
Hafla ya maamuzi ya fomu za shindano la mamashujaa wa Chakula Bi. Stella
E. Mrosso ambaye ni Mkuu wa mahabara ya Chakula TBS akifungua rasmi
hafla hiyo ya kuanza kuzihakiki fomu hizo .
Mkurugenzi
Mkazi wa Oxfam Tanzania Jane Foster akiwashukuru TBS , Majaji pamoja na
washiriki ambao ndio watazipitia fomu hizo kabla hazijafika kwa majaji.
Mratibu wa Programu kutoka Care International in Tanzania Maureen Kwilasa akisisitiza jambo wakati wa Hafla hiyo
Mkurugenzi
Mkazi wa Oxfam Tanzania Jane Foster, Mkuu wa maabara chakula TBS Stella
E. Mrosso, Tusfaye Legesse Obole President's Delivery Bureau, Manager
Agriculture Productivity na Mratibu wa Programu kutoka Care
International in Tanzania Maureen Kwilasa wakiwa katika hafla hiyo.
Mkuu
wa maabara chakula TBS Stella E. Mrosso aliye Mwakilisha Mgeni rasmi
katika hafla hiyo akimkabidhi rasmi fomu za shindano la mama shujaa wa
chakula Mkurugenzi Mkazi wa Oxfam Tanzania Jane Foster kwa ajili ya
kuanza kufanya maamuzi.
Vijana
wenye fani mbalimbali kutoka vyuo vikuu na taasisi mbalimbali wakiwa
katika mchakato kwa kuzipitia Fomu zote za maombi ya kushiriki shindano
la mama shujaa wa Chakula 2015
******
Shindano
la mama shujaa wa chakula limeingia katika hatua mpya baada ya zoezi la
kukusanya fomu za washiriki kutoka mikoa mbalimbali nchini kupitiwa na
majaji kwa ajili ya mchujo ambapo washiriki 18 watapatikana kisha
baadaye 15 bora ambao wataingia kijijini kwa ajili ya mchakato wa
kugombea nafasi ya mama shujaa wa chakula mwaka 2015.
zoezi
la kusahihishwa fomu limezinduliwa mapema leo hii na mwakilishi wa
Mkurugenzi Mtendaji wa TBS, Joseph Masikitiko ambaye ni Mkuu wa Maabara
na Chakula TBS, Bi. Stella Mrosso akiwa sambamba na Mkurugenzi Mkazi wa
Shirika la Oxfam Tanzania, Jenny Foster na majaji watakaopitia zoezi
zima la mchujo wa fomu hizo.
akizungumza
na wageni waandishi wa habari katika uzinduzi huo Mkuu wa Maabara na
Chakula, Bi. Stella Mrosso alilisifu shirika la Oxfam kuwa mstari wa
mbele katika kupigania haki za wanawake, umiliki wa ardhi na kuhamasisha
uzalishaji wa chakula kwa wazalishaji wadogo wadogo.
Bi.
Stella alisisitiza kuwa kila mzalishaji anapaswa kuzalisha bidhaa bora
ili kushindana na soko la ndani na la nje huku akifafanua kuwa kwa
kupitia SIDO, TFDA na Wizara ya Afya, wazalishaji wadogowadogo watakuwa
na uwezo wa kupata kibali kutoka TBS bure na kuongeza kuwa wakina mama
nchini watumie shindano la mama shujaa wa Chakula kama chachu ya
kujitokeza kwa wingi katika mashindano yanayofuata huku wengine
wakijifunza uzalishaji bora kupitia mashindano hayo.
Serikali yatoa changamoto kwa watafiti wa sayansi ya afya
SERIKALI imewaomba watafiti wa masuala ya afya hapa nchini kuhakikisha kwamba wanaibua hoja mpya zitakazosaidia kuleta mabadiliko kwenye sera za kitaifa zinazohusu sekta hiyo muhimu. Wito huo umetolewa jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki na Katibu Mkuu Wizara ya Afya na ustawi wa jamii Dk. Donan Mbando mara tu baada ya kufunga mkutano mkuu watatu wa sayansi ya afya uliondaliwa na chuo kikuu cha Afya na Sayansi shirikishi cha Muhimbili (MUHAS).
“Kwa sasa taifa linashuhudia ongezeko kubwa la idadi ya watu wanaosumbuliwa na magonjwa yasiyoyakuwa ya mbukiza kama vile kisukari, shinikizo la damu na kisukari. Kwa bahati mbaya sana vituo vyetu vingi vya afya havijaandaliwa vizuri kukabiliana na magonjwa haya kwasababu sera zetu wakati zinaandaliwa hazikujika zaidi kwenye magonjwa yasiyoyakuwa ya kuambukiza na ndio maana tunahitaji mabadiliko kwenye hili,’’ alisema Dr. Mbando.
Dr. Mbando alizataja sababu kubwa zinazochangia ongezeko la magonjwa hayo kuwa ni pamoja na matumizi ya pombe kupita kiasi, aina ya vyakula vinavyotumiwa na watanzania hususani wale wanaoishi maeneo ya mijini, kutokufanya mazoezi pamoja na uvutaji wa sigara. Aidha aliiongeza kuwa kwa sasa serikali ipo kwenye mpango wa kuandaa mkakati wanne wa huduma za afya hapa nchini (health care financing strategy) utakao muwezesha kila mtanzania kuwa na bima ya afya.
“Kwa sasa ni asilimia 20 tu ya watanzania ndio wanamiliki bima za afya zinazotolewa na shirika la bima ya afya la taifa na mashirika binafsi na hivyo kufanya asilimia 80 ya watanzania kuishi bila kuwa na uhakika wa masuala ya tiba….hili tumelianza tayari,’’ alibainisha.
Kuhusu mlipuko wa ugonjwa wakipundupindu kwenye mikoa ya kagera na kigoma uliosababishwa na kuingia kwa wakimbizi kutoka Burundi, Dr. Mbando alisema kwa sasa serikali kwa kushirikiana na Wananchi, wadau wa maendeleo na asasi zisizo za kiraia wanapambana kuhakikisha tatizo hilo linakwisha.
Akizungumza kwenye mkutano huo Makamu mkuu wa MUHAS, Prof. Ephata Kaaya alisema kwa sasa taifa linahitaji zaidi tafiti za kiafya hususani kwenye magonjwa yasiyo ya kuambukiza na ndio sababu mkutano huo ulijikita zaidi kujadili tatizo hilo.
“Kama wataalamu wa masuala ya afya tunaona kuna haja kubwa tukiwekeza katika tafiti zinazolenga kuibua changamoto na suluhisho kwenye magonjwa haya,’’ alisema. Mkutano huo wa siku mbili ulihudhuriwa na washiriki zaidi ya 300 wakiwemo madaktari, viongozi na wanafunzi wa udaktari kutoka MUHAS na vyuo vingine vya afya.
Jisajili kwenye:
Machapisho (Atom)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO MHE MWANJELWA AMUAGIZA MRAJIS KUFANYA UCHUNGUZI SACCOS YA MADIBIRA-MBARALI NDANI YA SIKU 14
Naibu Waziri wa Wizara ya Kilimo, Mhe Mary Mwanjelwa akisisitiza jambo wakati akizungumza na Viongozi mbalimbali wa Mkoa na kamati ya uli...