Bwawa la Bubinza hatarini Kutoweka kutokana na Miundombinu yake Kuhujumiwa
Kwa sasa bwawa hilo limeanza kuota majani na magugumaji, huku likionekana kugeuzwa kuwa sehemu ya kunyweshea maji mifugo yao, baada ya miundombinu yake ya mabomba kuharibiwa na watu wasiojulikana.
Baadhi ya wakazi wa eneo hilo, wameiambia FikraPevu kwamba hujuma hizo za wizi na uharibifu wa miundombinu ya bwawa hilo, si tu unahatarisha uhai wa bwawa hilo, bali unaweza kusababisha zaidi ya watu 10,000 wa vijiji vinavyolizunguka kukosa maji kwa ajili ya matumizi yao ya nyumbani. Bwawa hilo ndilo pekee linategemewa kwa maji na wananchi wa vijiji vya Bubinza, Ihale na Sola.
Baadhi ya wananchi hao wamelalamikia kitendo cha baadhi ya watu kuanza kuharibu kwa makusudi mabomba ya bwawa hilo, huku wakitoa ombi maalum kwa vyombo vya dola kufanyia uchunguzi suala hilo na hatimaye kuwakamata wahusika.
“Kuna koki mbili za mabomba ya bwawa hili la Bubinza zimeharibiwa, na inabidi kuingiza miti ili kuzuia maji yasiendelee kutoka. Wizi huu unafanyika huku viongozi wa Serikali ya Kijiji wakiwa wapo hapa hapa. Kwanini wahusika hawakamatwi?” amehoji Kiongozi wa Kamati ya Kusimamia Miradi Eendelevu (CMC) Kijiji cha Bubinza, Mathayo Lugwisha.
Kwa upande wao, Mariam Joseph na Kabihe Merick, wakazi wa kijiji cha Kisamba kinachozunguka bwawa hilo la Bubinza, wamesema iwapo mradi huo utakufa kutokana na maji yake kukauka, wananchi hasa wanawake wa maeneo hayo watalazimika kutembea umbali wa kilometa zaidi ya 10 kwa ajili ya kupata maji kutoka Ziwa Victoria.
“Kule Kisamba, pindi visima vinapokauka maji, ndoo moja ya maji inauzwa kati ya Sh 500 na 1,000. Sasa ukiangalia hili bwawa la Bubinza limejaa magugumaji. Watu wananyweshea mifugo yao na maji yanachafuka mno. Wanawake watateseka sana kama bwawa hili litafutika,” amesema Mariam.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Bubinza, Juma Kasomi, amekiri kuwepo kwa hujuma hiyo, akisema wanafanya uchunguzi ili kuwabaini wahusika wa hujuma hizo, na kwamba yeyote atakayebainika kufanya uharibifu huo atachukuliwa hatua za kisheria.
Mratibu wa Shirika la Uangalizi wa Miradi Eendelevu (TCSD) nchini, Damas Nderumaki amesema uharibifu huo na uchafuzi wa mazingira unatokana na uelewa mdogo wa jamii kuhusu faida ya utunzaji mazingira.
“Wananchi wa Kijiji na Kata ya Lubugu, lazima watambue kwamba wanao wajibu wa kulinda rasilimali zote zinazowazunguka, ikiwemo miradi ya maendeleo. Inawapasa washirikiane kuondoa magugumaji ambayo yameanza kujaa kwenye bwawa la Bubinza,” amesema.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni