Ijumaa, 27 Machi 2015

Watoto 13,600 Huzaliwa kila mwaka wakiwa na matatizo ya Magonjwa ya Moyo

  s
CHAMA cha Madaktari wa Watoto nchini, kimeeleza kuwepo kwa tatizo kubwa la watoto wengi nchini kuzaliwa wakiwa na matatizo ya moyo tayari, FikraPevu imebaini.


Kwa mujibu wa takwimu za chama hicho, takriban watoto 13,600 huzaliwa kila mwaka wakiwa na magonjwa ya moyo, huku watoto 3,400 kati yao wakihitaji kupatiwa matibabu kwa kufanyiwa upasuaji.


Akizungumzia ukubwa wa tatizo hilo la ugonjwa wa moyo kwa watoto nchini, jijini Dar es Salaam, Makamu wa Rais wa chama hicho cha Madaktari wa Watoto, Dk Namala Mkopi, anasema katika miaka michache iliyopita, idadi ya watoto waliohitaji matibabu ya upasuaji, imekuwa ikiongezeka mwaka hadi mwaka.

Kwa mujibu wa Dk Mkopi, katika mwaka 2013/2014 takriban watoto 332 waliogundulika kuwa na ugonjwa wa moyo, walihitaji kufanyiwa matibabu ya upasuaji, huku wengine 128 wakilazimika kusafirishwa kwenda nchini India kwa ajili ya kupatiwa matibabu hayo.

Kwa upande wake, Dk. Godfrey Mbawara, ambaye ni Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Watoto katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, anasema kwa mwaka jana pekee watoto zaidi ya 900 waligundulika kuwa na magonjwa hayo ya moyo.

Takwimu kuhusiana na vifo vinavyotokana na magonjwa ya moyo nchini kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), zinaonyesha kwamba watu 19,000, sawa na asilimia 4.3 ya vifo vyote vilivyotokea nchini, walifariki dunia katika kipindi cha mwaka 2011 kutokana na magonjwa ya moyo.

Aidha, kwa mujibu wa takwimu hizo, watu 117 katika kila watu 100,000 wanaobainika kuwa na uganjwa huo nchini, hufariki dunia kila mwaka kutokana na magonjwa ya moyo, wakati takriban watu milioni 12 hufariki kwa ugonjwa huo kila mwaka duniani.

Kwa mujibu wa WHO, Tanzania inatajwa kuwa miongoni mwa nchi zilizoathirika zaidi kwa magonjwa ya moyo, ikiwa inashika nafasi ya 87 katika nchi zote duniani zenye tatizo la magonjwa ya moyo.


Wakati hali ya magonjwa ya moyo kwa watoto nchini ikionyesha hivyo, FikraPevu imeelezwa kwamba hali ya ugonjwa wa kifua kikuu nayo inaonekana kuwa tishio kwa makundi ya vijana katika mataifa mengi ulimwenguni, Tanzania ikiwemo.

Takwimu za Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, zinaonyesha kwamba katika kipindi cha mwaka 2013 pekee, wagonjwa 65,000 waliogundulika kuwa na tatizo la kifua kikuu, wengi wao walikuwa ni vijana.


Mtafiti Mwandamizi kutoka Taasisi ya Magonjwa ya Binadamu (NIMRI), Kituo cha Muhimbili, Andrew Kilale, anasemna kundi la vijana nchini liko hatarini zaidi kutokana na shughuli wanazozifanya kila siku.


Kilale anazitaja dalili kuu za ugonjwa wa kifua kikuu kuwa ni pamoja na mgonjwa kukosa nguvu ya kufanya kazi, mgonjwa kupoteza hamu ya kula chakula, kukohoa mfululizo kwa muda wasiku zisizopungua wiki mbili hadi tatu, kupoteza uzito na mgonjwa kuwa na homa kali vipindi va jioni.

“Mambo yanayochangia kuongezeka kwa ugonjwa wa kifua kikuu nchini ni pamoja na kula vyakula vibichi vitokanavyo na wanyama, kunywa maziwa mabichi, kula nyama mbichi au kunywa damu mbichi,” amesema Kilale.

Kwa mujibu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, mikoa yenye tatizo kubwa la ugonjwa wa kifua kikuu nchini ni pamoja na Mbeya, Mara, Morogoro, Tanga, Dar es Salaam, Mwanza, Shinyanga na Arusha.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

NAIBU WAZIRI WA KILIMO MHE MWANJELWA AMUAGIZA MRAJIS KUFANYA UCHUNGUZI SACCOS YA MADIBIRA-MBARALI NDANI YA SIKU 14

Naibu Waziri wa Wizara ya Kilimo, Mhe Mary Mwanjelwa akisisitiza jambo wakati akizungumza na Viongozi mbalimbali wa Mkoa na kamati ya uli...