CHAMA cha Madaktari wa Watoto nchini, kimeeleza kuwepo kwa tatizo kubwa
la watoto wengi nchini kuzaliwa wakiwa na matatizo ya moyo tayari,
FikraPevu imebaini.
Kwa mujibu wa takwimu za chama hicho, takriban watoto 13,600 huzaliwa
kila mwaka wakiwa na magonjwa ya moyo, huku watoto 3,400 kati yao
wakihitaji kupatiwa matibabu kwa kufanyiwa upasuaji.
Akizungumzia ukubwa wa tatizo hilo la ugonjwa wa moyo kwa watoto
nchini, jijini Dar es Salaam, Makamu wa Rais wa chama hicho cha
Madaktari wa Watoto, Dk Namala Mkopi, anasema katika miaka michache
iliyopita, idadi ya watoto waliohitaji matibabu ya upasuaji, imekuwa
ikiongezeka mwaka hadi mwaka.
Kwa mujibu wa Dk Mkopi, katika mwaka 2013/2014 takriban watoto 332
waliogundulika kuwa na ugonjwa wa moyo, walihitaji kufanyiwa matibabu ya
upasuaji, huku wengine 128 wakilazimika kusafirishwa kwenda nchini
India kwa ajili ya kupatiwa matibabu hayo.
Kwa upande wake, Dk. Godfrey Mbawara, ambaye ni Daktari Bingwa wa
Magonjwa ya Watoto katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, anasema kwa
mwaka jana pekee watoto zaidi ya 900 waligundulika kuwa na magonjwa hayo
ya moyo.
Takwimu kuhusiana na vifo vinavyotokana na magonjwa ya moyo nchini kwa
mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), zinaonyesha kwamba watu 19,000,
sawa na asilimia 4.3 ya vifo vyote vilivyotokea nchini, walifariki
dunia katika kipindi cha mwaka 2011 kutokana na magonjwa ya moyo.
Aidha, kwa mujibu wa takwimu hizo, watu 117 katika kila watu 100,000
wanaobainika kuwa na uganjwa huo nchini, hufariki dunia kila mwaka
kutokana na magonjwa ya moyo, wakati takriban watu milioni 12 hufariki
kwa ugonjwa huo kila mwaka duniani.
Kwa mujibu wa WHO, Tanzania inatajwa kuwa miongoni mwa nchi
zilizoathirika zaidi kwa magonjwa ya moyo, ikiwa inashika nafasi ya 87
katika nchi zote duniani zenye tatizo la magonjwa ya moyo.
Wakati hali ya magonjwa ya moyo kwa watoto nchini ikionyesha hivyo,
FikraPevu
imeelezwa kwamba hali ya ugonjwa wa kifua kikuu nayo inaonekana kuwa
tishio kwa makundi ya vijana katika mataifa mengi ulimwenguni, Tanzania
ikiwemo.
Takwimu za Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, zinaonyesha kwamba katika
kipindi cha mwaka 2013 pekee, wagonjwa 65,000 waliogundulika kuwa na
tatizo la kifua kikuu, wengi wao walikuwa ni vijana.
Mtafiti Mwandamizi kutoka Taasisi ya Magonjwa ya Binadamu (NIMRI),
Kituo cha Muhimbili, Andrew Kilale, anasemna kundi la vijana nchini liko
hatarini zaidi kutokana na shughuli wanazozifanya kila siku.
Kilale anazitaja dalili kuu za ugonjwa wa kifua kikuu kuwa ni pamoja na
mgonjwa kukosa nguvu ya kufanya kazi, mgonjwa kupoteza hamu ya kula
chakula, kukohoa mfululizo kwa muda wasiku zisizopungua wiki mbili hadi
tatu, kupoteza uzito na mgonjwa kuwa na homa kali vipindi va jioni.
“Mambo yanayochangia kuongezeka kwa ugonjwa wa kifua kikuu nchini ni
pamoja na kula vyakula vibichi vitokanavyo na wanyama, kunywa maziwa
mabichi, kula nyama mbichi au kunywa damu mbichi,” amesema Kilale.
Kwa mujibu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, mikoa yenye tatizo
kubwa la ugonjwa wa kifua kikuu nchini ni pamoja na Mbeya, Mara,
Morogoro, Tanga, Dar es Salaam, Mwanza, Shinyanga na Arusha.