Katibu wa chama cha Walimu Mkoa wa Mbeya (CWT) Kasuku Bilago akitoa taarifa ya Mkoa
TAARIFA KWA VYOMBO VYA
HABARI
Ndugu Waandishi wa habari,
CWT mkoa wa Mbeya kinawasilisha hoja mbalimbali
za walimu kwa serikali yao kama ifuatavyo:-
1. MADAI YA WALIMU YA MUDA MREFU
Walimu wa mkoa wa Mbeya wana madai yao serikalini ambayo
yalihakikiwa Septemba 2013. Baada ya uhakiki huo uliofanyika nchi nzima kiasi
cha madai ya mkoa wa Mbeya yaliyokubaliwa na serikali yalikuwa kiasi cha zaidi
ya sh. 4.6 Bilioni. Serikali haijaonyesha nia thabiti ya kumaliza madai haya
kwa walimu wa mkoa wa Mbeya kwani walimu
bado wanaidai serikali kwa mchanganuo ufuatao:-
JUMLA
YA MADENI YA WALIMU MKOA WA MBEYA MPAKA DISEMBA 2014
|
|
WILAYA
|
KIASI
CHA DENI
|
MBEYA JIJI
|
1,220,620,843.00
|
MBEYA VIJIJINI
|
154,436,695.07
|
RUNGWE
|
220,000,000.00
|
KYELA
|
165,723,474.00
|
MBOZI/MOMBA
|
998,554,540.83
|
ILEJE
|
164,418,518.00
|
CHUNYA
|
463,871,400.24
|
MBARALI
|
230,666,235.66
|
JUMLA
KUU
|
3,618,291,706.80
|
Kwa hali hiyo CWT Mkoa wa Mbeya kinaitaka serikali kulipa
madai haya kabla au ifikapo tarehe 30/4/2015 ili kurudisha ari ya ufundishaji
kwa walimu. Kama serikali haitalipa madai haya Chama cha Walimu kitawaelekeza
walimu kuchukua maamuzi magumu kwa serikali mwaka huu wa 2015. Aidha, ieleweke
kuwa madai haya ni ya muda mrefu kuanzia 2007 hadi 2014 jambo ambalo CWT
hakiwezi kuvumilia kuendelea kuona serikali inavunja Sheria na Kanuni za
utumishi wa umma. Madai haya yalikubalika kwenye Kamati ya uhakiki.
Aidha, kuna baadhi ya watendaji wa serikali ambao wamekuwa na
upotoshaji mkubwa juu ya madai ya walimu kwamba yamelipwa yote au yamebaki
kidogo sana kama milioni 200 tu. CWT inasikitishwa sana na kauli kama hizo
kwani ni za uchochezi na kuwakatisha tamaa walimu. Mfano halisi ni madai
yaliyohakikiwa mkoa wa Mbeya ambayo hayajalipwa hadi sasa ni zaidi ya 3.6
Bilioni.
2. MALIPO YA LIKIZO KUTOLIPWA
Tangu Desemba 2013 serikali ilibadili utaratubu wa kulipa
walimu nauli za likizo kabla ya kwenda likizo zao. Hivyo, walimu wamekuwa
wakienda likizo bila kulipwa stahili zao. Likizo zifuatazo walimu hawajalipwa;
Desemba 2013, Juni 2014 na Desemba 2014 jambo linalokwenda kinyume na Kanuni za
Utumishi wa Umma, 2003; Kifungu cha 97 (5) kinachomtaka mwajiri kulipa nauli ya
likizo kwa kila mtum ishi wa umma mara moja katika kipindi cha miaka miwili.
3. KUTOPANDA KWA MADARAJA YA WALIMU KWA WAKATI
Kwa kawaida walimu wanatakiwa kupanda madaraja yao kila baada
ya miaka 3 kama hakuna tatizo la kiutumishi. Utaratibu huu umekiukwa na serikali
kwa madai ya ukomo wa bajeti (ceiling) jambo linaloathiri maslahi na haki ya
walimu ya kupanda daraja. CWT kinaitaka serikali kuwapandisha madaraja walimu
wote wa mkoa wa Mbeya waliofikia muda wa kupanda ili kuwapa motisha wa kuipenda
kazi yao.
4. KUUNGA MKONO TAMKO LA BARAZ LA CWT TAIFA
Chama cha Walimu Tanzania mkoa wa Mbeya kinapenda kuunga
mkono maazimio manne ya Baraza la CWT taifa lililofanyika mjini Morogoro katika
ukumbi wa Midland Hotel kuanzia tarehe 21-23 Januari, 2015. Maazimio haya yanataka
uwajibikaji wa dhati wa Serikali ikiwa ndio mwajiri Mkuu wa walimu wote wa
shule na Taasisi za Umma kama ifuatavyo:-
(i)
Utekelezaji
wa Waraka wa maendeleo ya utumishi Na.1 wa 2014 juu ya miundo ya utumishi wa
kada za ualimu chini ya WEMU Kumb. Na.AC.87/260/01/G/9.15/7 wa 2014 unaohusisha
miundo ya watumishi wa kada za walimu walio chini ya Wizara ya Elimu na Mafunzo
ya Ufundi uliopanua wigo wa ngazi za mishahara ya walimu na kuagiza utekelezaji
wake kuanza tarehe 01 Julai, 2014.
AZIMIO:
Walimu wote waliogota muda mrefu kwenye ngazi zilizofunguliwa
wapandishwe vyeo kuanzia tarehe 01 Julai, 2014 na kulipwa malimbikizo ya
mishahara hiyo kabla au ifikapo tarehe 30 Aprili, 2015.
(ii)
Walimu/Wanachama wa CWT wamekopwa na Serikali
stahili zao kwa muda mrefu. Hadi
mwishoni mwa Desemba, 2014 walimu wanaidai Serikali jumla ya T.sh 16 Bilioni.
Kwa mujibu wa uhakiki uliofanyika Desemba, 2013.
AZIMIO:
Baraza linaitaka Serikali kuwa imelipa madeni yote ya walimu
kabla au ifikapo tarehe 30 Aprili, 2015.
(iii)
Mamlaka
ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) ilibadili vikokotoo vya mafao kwa ajili ya wastaafu
bila kushirikisha wala kupata ridhaa ya wadau ambao ni wanachama wa Mifuko ya
Hifadhi husika wakiwemo walimu.
AZIMIO:
Kuitishwe mjadala wa wadau wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii,
wadau na SSRA kabla au ifikapo tarehe 30 Aprili, 2015 ili kutafuta ufumbuzi wa
suala hilo. Hiyo itakuwa ni kutekeleza
ahadi ya Mhe. Waziri Mkuu aliyoitoa
katika hotuba aliyoitoa katika Sherehe za Siku ya Mwalimu Duniani iliyofanyika
Mjini Bukoba-Kagera Kitaifa tarehe 5 Oktoba, 2014 juu ya kuliangalia upya suala
hilo.
(iv)
Madai
na kilio cha muda mrefu cha walimu tangu awamu ya tatu ya uongozi wa Taifa hili
ni kuwa na mwajiri mmoja- Chombo kimoja cha kushughulikia huduma zote za walimu
kuliko ilivyo leo ambapo walimu wanaajiriwa na kuhudumiwa na Wizara na Taasisi
zaidi ya nne. Sasa kilio hiki kifike
mwisho kwa kuwa hata Bunge la 16 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilipitisha
Azimio la kuanzishwa kwa chombo kimoja cha kuajiri walimu.
AZIMIO:
Baraza la Taifa lina tamka kuwa chombo kimoja cha ajira ya
walimu kiundwe na kuanza utekelezaji wake kabla au ifikapo tarehe 30 Aprili,
2015. Aidha mchakato wa Sheria ya kutaka
walimu waajiriwe na Mamlaka za Halmashauri za Wilaya uachwe mara moja kwani
hauna tija kwa walimu na Elimu ya nchi hii.
MWISHO:
CWT mkoa wa Mbeya kinaitaka serikali kuhakikisha kwamba
inawalipa madai walimu wote pamoja na kuwapandisha madaraja wanaostahili
sambamba na kulipa fedha za likizo zao. Endapo haya hayatatekelezwa kwa muda
mwafaka Chama kitawaelekeza
walimu/wanachama wake kuchukua maamuzi magumu juu ya serikali mwaka huu wa
2015.
Taarifa hii imetolewa na:
NELUSIGWE KAJUNI
MWENYEKITI CWT MKOA WA MBEYA
31/1/2015
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni