Na Saidi Mkabakuli, Kagera
Mkoa wa Kagera na maeneo ya jirani wataanza
kujivunia uwanja wa ndege wa kisasa kufuatia kukamilika kwa Kiwanja cha Ndege
cha Bukoba.
Akizungumza na Wakaguzi wa Miradi ya Maendeleo toka
Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango, Meneja Mradi wa Upanuzi wa Kiwanja cha Ndege cha
Kagera, Mhandisi Suleiman Athuman, amesema kwamba maendeleo ya ujenzi wa jengo la
abiria la kiwanja hicho upo kwenye hali nzuri na mkandarasi atabidhi kazi hiyo
mapema mwakani.
“Katika mwaka wa fedha wa 2013/14 kazi zilizopangwa
ni ukarabati na upanuzi wa miundombinu ya kiwanja, ikijumuisha barabara ya
kuruka na kutua ndege, maegesho ya ndege, barabara ya kiungio, kwa sasa ujenzi
unaendelea vizuri na Mkandarasi atatukabidhi kazi mapema mwakani,” alisema Mhandisi
Athuman.
Akitoa taarifa ya maendeleo ya ujenzi wa Kiwanja cha
Bukoba, Mhandisi Mshauri wa ujenzi wa kiwanja hiko, Mhandisi Pius Gobolo
amesema kuwa kazi za usimikaji wa mfumo wa taa za kuongozea ndege, ujenzi wa
jengo jipya la abiria na uzio wa usalama zimeshakamilika kwa asilimia 80.
“Kama unavyojionea, sehemu kubwa ya kazi
imekamilika, kwa makadirio ni zaidi ya asilimia 80 ya ujenzi wa kiwanja hiki
imeshakamilika,” aliongeza Mhandisi Gobolo.
Kwa mujibu wa mpangokazi wa ujenzi wa kiwanja hicho
hadi kufikia mwezi Juni 2014, hatua iliyofikiwa ni pamoja na kukamilika kwa
ukarabati wa barabara ya kuruka na kutua ndege, barabara ya kiungio na maegesho
ya ndege kwa kiwango cha lami; na ujenzi wa jingo jipya la abiria kufikia hatua
ya usimikaji wa paa na mifumo ya maji safi, maji taka na umeme; na kuendelea
kwa ujenzi wa jengo la abiria na kituo cha umeme.
Naye, Kiongozi wa Timu ya Ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo kutoka Ofisi ya Rais,
Tume ya Mipango, Bibi Florence Mwanri amesema kuwa Serikali imeazimia
kuendelea kuboresha miundombinu ya viwanja vya ndege hususan miradi
iliyoibuliwa katika Programu ya Matokeo Makubwa Sasa.
“Kwa mujibu Programu ya Matokeo Makubwa Sasa,
serikali kupitia Mamlaka ya
Viwanja vya Ndege nchini ipo kwenye mkakati wa kuuendeleza viwanja vya ndege
vyote ili viwe na kiwango kizuri kwa watumiaji wa viwanja hivyo,” alisema Bibi
Mwanri.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni