HALI si shwari katika Kanisa la
Moravian Jimbo la Kusini Magharibi kufuatia mgogoro wa muda mrefu ambapo safari
hii baadhi ya waumini na wachungaji walitaka kufunga ofisi za Jimbo hilo
wakishinikiza kujiuzulu kwa Askofu, Alinikisa Cheyo.
Tukio la kufunga ofisi za Jimbo hilo
limetokea leo majira ya saa 12 asubuhi
ambapo baadhi ya Wachungaji na waumini wa kanisa hilo walifika katika
makao makuu ya Jimbo yaliyoko Jakaranda jijini Mbeya wakiwa na makufuri yao.
Kanisa la Moraviani Tanzania, jimbo la
kusini Magharibi kwa zaidi ya mwaka mmoja limekuwa katika mgogoro wa kiuongozi,
baada ya kamati tendaji (KTM-JKM) kumsimamisha Mwenyekiti aliyechaguliwa
kihalali kupitia mkutano Mkuu (Sinod), Nosigwe Buya, kwa madai ya kushindwa
kulisimamia kanisa na kumpandisha aliyekuwa Makamu wake, Zacharia Sichone,
jambo lililoibua mpasuko.
Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Prof. Norman
Sigalla King ndiye aliyenusuru kufungwa kwa kanisa hilo baada ya kuwasihi wachungaji na Waumini
wenye jazba kuwa na subira wakati Serikali ikijaribu kuona namna ya kutatua
mgogoro huo.
Akizungumza na kundi hilo, Prof. Sigalla aliyefika eneo hilo majira ya saa 3:20 aliwaomba wachungaji
hao, kusitisha azima yao hiyo ya kuzifunga ofisi za Makao Makuu ya kanisa na
kuwa na subira kwani siku inayofuata serikali ingetoa msimamo juu ya mgogoro huo.
Akizungumza baada ya kukubali ombi la
Mkuu wa Wilaya, mmoja wa wachungaji hao, Edward Chilale, alisema wamefika hatua
hiyo baada ya Askofu Mkuu wa kanisa hilo,kupuuza madai yao ya kutaka kuitishwa
kwa Mkutano Mkuu wa kanisa (Sinod) utakaoamua hatima ya mgogoro baada ya
kusimamishwa kwa aliyekuwa Mwenyekiti wa jimbo hilo, Mwenyekiti Buya.
Mchungaji Chilale alisema licha ya
kuheshimu kauli ya serikali ya kutaka kusitisha mpango wao wa kulifunga kanisa,
bado shinikizo lao la kutaka Askofu Cheyo kujiuzulu bado liko palepale, kwani
yeye ndio chanzo cha yote.
Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti jimbo
hilo, Sichone, alisema kuwa amesikitishwa na kitendo kilichofanywa na kundi
hilo ndani ya kanisa kwa kuwa kimeenda tofauti na taratibu za kanisa, ambapo
mambo yote hufanywa kupitia vikao.
Alisema tayari wametoa taarifa jeshi la
polisi na kwamba tukio hilo liliongozwa na wachungaji sita wa ushirika wa
Bethlehemu ambalo kwa muda mrefu limekuwa likiendesha mambo kinyume na taratibu
za kanisa.
Wachungaji hao pamoja na kukubali
kufungua ofisi waliweka misimamo yao ambayo Miongoni mwa maazimio hayo ni
kuutaka uongozi huo wa kanisa kubatilisha mara moja maamuzi yake ya
kumsimamisha kazi Mwenyekiti huyo na asibughudhiwe hadi Mkutano Mkuu wa Sinodi.
Pia waliitaka halmashauri kuu iwe
imeitisha Mkutano Mkuu wa Sinodi Machi 3 mwaka huu na kwamba isipotii
maazimio hayo ya wakristo watachukua hatua ya kuzifunga ofisi zote za jimbo na
kufanya maandamano ya amani kwa kibali cha vyombo vya dola.
Credit; mbeya yetu
|
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni