Naibu Waziri wa Wizara ya Kilimo Mhe Mary Mwanjelwa akizungumza na wafanyakazi wa Taasisi ya Udhibiti wa Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI) wakati wa ziara yake ya kikazi Mkoani Morogoro, Jana 30 Disemba 2017.
Naibu Waziri wa Wizara ya Kilimo Mhe Mary Mwanjelwa akikagua Maabara ya Kutazama kiwango cha Uotaji wa Mbegu Mkoani Morogoro wakati wa ziara yake ya kikazi alipotembelea Taasisi ya Udhibiti wa Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI), Jana 30 Disemba 2017.
Naibu Waziri wa Wizara ya Kilimo Mhe Mary Mwanjelwa akisisitiza jambo wakati akizungumza na wafanyakazi wa Taasisi ya Udhibiti wa Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI) Mkoani Morogoro wakati wa ziara yake ya kikazi, Jana 30 Disemba 2017.
Na Mathias Canal, Morogoro
Naibu Waziri wa Wizara ya Kilimo Mhe Mary Mwanjelwa, Jana 30 Disemba 2017 ametangaza KIAMA kwa wafanyabiashara wa mbegu nchini wanaouza Mbegu feki zilizopigwa marufuku na serikali.
Amewataka wafanyabiashara wote wa mbegu ambao wamekuwa wakifanya biashara hiyo kwa kuwauzia wakulima mbegu feki zilizopigwa marufuku na serikali kuacha haraka iwezekanavyo kwani serikali itawachukulia hatua za kisheria wale wote watakaobainika kukiuka maagizo ya serikali.
Ametoa agizo hilo akiwa ziarani Mkoani Morogoro ambapo pamoja na mambo mengine alitembelea Taasisi ya Udhibiti wa Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI), Taasisi iliyopewa jukumu na serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania la usajili wa wafanyabiashara wa mbegu (Seed Dealers).
"Serikali imepokea malalamiko mengi kwa wananchi kuhusu Ubovu wa mbegu jambo ambalo limepelekea kwa kiasi kikubwa kuwa na mavuno kidogo pasina kukidhi matakwa ya wakulima wetu nchini" Alikaririwa Mhe Mwanjelwa
Naibu Waziri huyo pia ameiagiza Taasisi ya udhibiti Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI) kujitathmini kwa utendaji duni kwani wameshindwa kutimiza majukumu yao kwa kuwabaini wafanyabiashara wanaokiuka maagizo ya serikali pamoja na taratibu na sheria za nchi.