Jumatano, 9 Machi 2016

Maongezi Ya Rais Magufuli na Rais Truong Wa Vietnam Baada Ya Kukutana IKULU


Rais wa Jamhuri ya Kisoshalisti ya Vietnam Mheshimiwa Truong Tan Sang ambaye amewasili hapa nchini jana jioni tarehe 08 Machi, 2016 kwa ziara ya kiserikali ya siku nne, amepokelewa rasmi na Mwenyeji wake Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, Ikulu Jijini Dar es salaam.

Katika lango kuu lililopo Mashariki mwa Ikulu, Rais Truong Tan Sang amekagua gwaride rasmi lililoandaliwa kwa heshima yake na amepigiwa mizinga 21 iliyokwenda sambamba na nyimbo za mataifa yote mawili.

Pamoja na mapokezi hayo, Marais hao wawili wamefanya mazungumzo ya faragha ambayo yamehudhuriwa pia na makamu wa Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, na baadaye kufuatiwa na mazungumzo rasmi kati ya Rais Magufuli na ujumbe wake na Rais Truong na Ujumbe wake.

Katika Mazungumzo hayo, Rais Magufuli ameahidi kuuendeleza na kuuimarisha zaidi uhusiano na ushirikiano kati ya Tanzania na Vietnam ambao ulijengwa na waasisi wa mataifa haya mawili Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Hayati Ho Chi Minh, hata kabla ya Uhuru, huku akitilia mkazo juu ya ushirikiano katika maendeleo ya kiuchumi.

Rais Magufuli amemweleza Rais Truong Tan Sang kuwa katika miaka mitano ijayo, Tanzania imedhamiria kujikita katika uanzishwaji wa viwanda vingi, na hivyo ametaka mahusiano kati ya Tanzania na Vietnam yajielekeze katika kuendeleza Kilimo na ufugaji na hivyo kuiwezesha nchi kuwa na uhakika wa chakula na pia kupata ziada itakayouzwa nchi.

"Tunatambua jinsi Vietnam ilivyopiga hatua kubwa katika uvuvi, uzalishaji wa kahawa na uzalishaji wa mpunga. Uzalishaji katika maeneo hayo umeiwezesha kuwa nchi inayoongoza duniani, na sisi Tanzania tunataka kujifunza kutoka kwenu" Amesisitiza Rais Magufuli.

Kufuatia hali hiyo, Rais Magufuli amemuomba Rais Truong Tan Sang, kuwa uhusiano na ushirikiano kati ya nchi hizi mbili ujikite katika kuendeleza kilimo hususani kutumia zana bora za kilimo badala ya jembe la mkono, Kilimo cha umwagiliaji badala ya kutegemea mvua, kuzingatia mbinu bora za ugani, kukabiliana na wadudu waharibifu wa mazao na kupata masoko ya mazao.

Kwa upande wake Rais wa Vietnam Mheshimiwa Truong Tan Sang amempongeza Rais Magufuli kwa kuchaguliwa kuiongoza awamu ya Tano na amemhakikishia kuwa Vietnam itaendelea kushirikiana na Tanzania, huku ikitambua mchango mkubwa uliotolewa na watu wa Tanzania walioiunga mkono juhudi za kuiunganisha nchi hiyo na kuwa Jamhuri ya Kisoshalisti mwaka 1968.

Amesema kwa kuzingatia mazingira bora ya Tanzania yenye amani na utulivu, Vietnam imedhamiria kuwa Tanzania iwe kituo chake cha kuzifikia nchi nyingine za Afrika Mashariki na sehemu nyingine za Afrika.

Rais Truong Tan Sang ameomba mahusiano ya Tanzania na Vietnam, sasa yajielekeze katika kuongeza Biashara, huku akieleza kuwa biashara ya Dola za Marekani milioni takribani milioni 300 haitoshi, na hivyo amependekeza wafanyabiashara wa Tanzania kuunganishwa na wenzao wa Vietnam ili mauzo ya bidhaa kutoka pande zote mbili yaongezeke hadi kufikia dola za Marekani bilioni 1 ifikapo mwaka 2020.

Ameongeza kuwa Vietnam ipo tayari kutiliana saini mikataba mbalimbali ya ushirikiano katika biashara, Viwanda na Kilimo, na ametoa mwaliko kwa wakulima wa Tanzania kwenda kujifunza nchini Vietnam.

Mara baada ya Mazungumzo hayo, Marais wote wawili wamezungumza na wananchi kupitia vyombo vya habari ambapo wote wawili wamesisitiza kuwa, nchi zao zipo tayari kukuza zaidi mahusiano na ushirikiano kwa faida ya wananchi wake.

Gerson Msigwa.
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam-09 Machi, 2016.

Jumanne, 8 Machi 2016

DR MARY MWANJELWA MWENYEKITI WA KAMATI YA ARDHI,MALIASILI NA UTALII ATOA MSAADA WA MAGODORO NA MASHUKA SHULE YA IYUNGA MBEYA

KATIBU WA MBUNGE TUMAINI AMBAKISYE AKIKABIDHI MSAADA WA MAGODORO 20 NA MASHUKA 40 KWA NIABA YA MBUNGE WA VITI MAALUMU DR MARY MWANJELWA

WANAFUNZI WA IYUNGA SEKONDARI WAKIPOKEA MSAADA WA MAGODORO NA MASHUKA TOKA KWA MWAKILISHI WA MBUNGE DR MARY MWANJELWA TUMAINI AMBAKISYE
WANAFUNZI WA IYUNGA SEKONDARI WAKIWA WANABEBA MAGODORO KWENDA STOO BAADA YA KUPEWA MSAADA NA MBUNGE DR MARY MWANJELWA

Jumapili, 6 Machi 2016

Serikali Yaanzisha Mfumo Mpya Wa Malipo Ya Mishahara Kwa Watumishi Wa Umma


SERIKALI imeanzisha mfumo wa Kielektroniki wa malipo ya mishahara kwa watumishi wa umma ambao unalenga kuondoa tatizo la madai ya malimbikizo ya stahili zao.

Hayo yamesemwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa jana (Jumamosi, Machi 5, 2016) wakati akizungumza na watumishi wa sekta mbalimbali  katika wilaya ya Meatu, mkoani Simiyu.
 
Waziri Mkuu alisema mfumo huo ujulikanao kama LAWSON, unatumika kwenye ajira za watumishi wote nchini, wa Serikali Kuu na wale wa Serikali za Mitaa  
 
Waziri Mkuu alisema mfumo huo unasaidia kutunza, kutuma na kuhuisha  taarifa za watumishi kwa wakati na kwa ufanisi tangu mtu anapoajiriwa hadi inapofikia wakati wa kupandishwa madaraja na hadi anapostaafu.

Kabla ya kuanzishwa kwa mfumo huo, maafisa utumishi walipaswa kukusanya taarifa za watumishi wote walioajiriwa na kuzipeleka Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma ili zikathibitishwe kabla ya kuzipeleka HAZINA kwa maandalizi ya mishahara. 
 
Akitolea mfano wa kada ya ualimu, Waziri Mkuu alisema ajira za walimu zilikuwa zinaanzia Idara ya Utumishi wa Walimu  (TSD)  lakini anapaswa aende kuripoti kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri  (DED) ambaye ni mwajiri wake chini ya TAMISEMI.
 "Hii ilileta ugumu wa malipo ya kupanda madaraja, uhamisho ama likizo kwa sababu mwajiri anakuwa hajatenga hizo fedha."
 
"Sasa hivi tuna Tume ya Utumishi wa Walimu  (TSC) ambayo iko chini ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri. Kwa hiyo ni rahisi wao kukaa pamoja na kuamua tuwapandishe daraja walimu 10 na wote hao wakalipwa bila bila kuchelewa," alisema.
 
Alisema mfumo huo umeanza kutumika tangu mwaka 2012 na ulianza kwa ajira mpya za walimu na hadi sasa umethibitisha kuwa inawezekana kumlipa mtumishi mshahara wake hata kama ameajiriwa ndani ya mwezi huohuo.
 
"Kama mtumishi anaripoti kwenye kituo kipya hata iwe wilaya ya wapi ili mradi amefika na barua zake zote na ziko sahihi mtu huyu ataingiziwa taarifa zake na wakati huohuo taarifa zitaonekana Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na pia zitapokelewa kwa maafisa wanaoshughikia mishahara kule HAZINA."
 
Alisema changamoto pekee waliyokutana nayo wakati mfumo huo umeanza ilikuwa ni kutoingizwa taarifa za wale ambao wameripoti baada ya tarehe 10 ya mwezi husika. 
"Hii ni kwa sababu matayarisho ya mishahara yanakuwa yameshaanza. Kwa hiyo wengi walishauriwa kuripoti kati ya tarehe 25 hadi tarehe 9 ya mwezi uliofuata na wote hawa hawakupata matatizo ya kucheleweshewa mshahara," alisema.
 
Akifafanua kuhusu upandishaji madaraja ya watumishi, Waziri Mkuu alisema  Serikali imeondoa utaratibu wa mtumishi kulazimika kuandika barua ya kukiri kupandishwa daraja/cheo ndipo aanze kupata stahili zake mpya. 
"Hii imeondoa ucheleweshaji wa kufanyika marekebisho ya mshahara  na pili imeondoa tofauti za mishahara kwa watumishi wenye ngazi moja (sifa sawa za kitaaluma, tarehe moja ya kuajiriwa) ambao walikuwa wakilipwa tofauti kwa sababu mmoja aliwahi kuandika barua ya kukiri na mwingine alichelewa kuandika barua hiyo hiyo " alisema

AKATISHA ZIARA KUTOKANA NA MSIBA
Wakati huohuo, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amelazimika kukatisha ziara ya mkoa wa Simiyu ambayo ilikuwa imalizike kesho kutokana na msiba wa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa ambayo alipangiwa kuitembelea leo.
 
Mkurugenzi huyo Bw. Traceas Kagenzi alifariki dunia usiku wa kuamkia jana kutokana na shinikizo la damu. Atasafirishwa kwenda Muleba  kwa mazishi.

Akitoa salamu za rambirambi kwenye ibada ya kumuombea marehemu Kagenzi iliyofanyika nyumbani kwake Maswa mjini, Waziri Mkuu alisema ameshtushwa na msiba huo uliotokea ghafla na kwamba Taifa limempoteza mtumishi mahiri ambaye bado Taifa lilikuwa likimtegemea.

"Nimeshtushwa sana na taarifa za msiba huu. Nimeambiwa hadi juzi usiku alikuwa akishirikiana na Mkuu wa Wilaya hii kuandika taarifa ya ziara ya wilaya hii. Kwa niaba ya Serikali, ninawapa pole sana wafiwa na Mungu awape uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha majonzi," alisema.

"Nimelazimika kukatisha ziara ya mkoa huu kwa sababu huyu ni mtumishi mwenzetu" alisema Waziri Mkuu.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAPILI, MACHI 6, 2016.

NAIBU WAZIRI WA KILIMO MHE MWANJELWA AMUAGIZA MRAJIS KUFANYA UCHUNGUZI SACCOS YA MADIBIRA-MBARALI NDANI YA SIKU 14

Naibu Waziri wa Wizara ya Kilimo, Mhe Mary Mwanjelwa akisisitiza jambo wakati akizungumza na Viongozi mbalimbali wa Mkoa na kamati ya uli...