Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa amewataka Makandarasi waliosimamisha kazi za ujenzi wa barabara nchini kuendelea na ujenzi baada ya Serikali kuanza kuwalipa madai yao.
Akizungumza mara
baada ya kukagua ujenzi wa barabara ya Magole-Turiani yenye urefu wa
kilomita 48.6 Wilayani Mvomero Mkoani Morogoro, Prof. Mbarawa alisema
tayari Serikali imeshalipa makandarasi mbalimbali nchini shilingi
bilioni 400 na itaendelea kufanya hivyo ili kumaliza madeni yao kwa
haraka.
“Hakikisheni
mnarejea kazini na kuwapa mikataba ya ajira wafanyakazi wenu katika
kipindi cha wiki mbili kuanzia sasa ili ujenzi wa barabara na madaraja
ukamilike kwa mujibu wa mkataba na hivyo kuondoa usumbufu kwa watumiaji
wa barabara hii”, alisema Prof Mbarawa.
Profesa
Mbarawa amemhakikishia mkandarasi China Civil Engineering Construction
Corporation anayejenga barabara ya Magole-Turiani kuwa tayari serikali
imeshamlipa zaidi ya kiasi cha dola za kimarekani zaidi ya laki 735 na
Shilingi za kitanzania zaidi ya Milioni 795 hivyo ni wakati wa
kukamilisha ujenzi huo hususan sehemu za madaraja kabla ya mvua za
masika kuaanza.
Akizungumza
katika ukaguzi huo Mbunge wa Mvomero Mhe. Sadick Murad ameiomba
Serikali kumalizia daraja la Diwale lenye urefu wa mita 75 ili liweze
kupitika.
Katika
hatua nyingine Waziri Prof. Mbarawa alikagua karakana ya ujenzi wa
vichwa vya treni mjini Morogoro na kumtaka mkandarasi anayekarabati
vichwa hivyo kufanya kazi hiyo kwa haraka na kutoa kazi nyingine kwa
watanzania ili kuwajengea uwezo wa kazi hizo.
Amewataka
wafanyakazi wa Shirika la Reli Tanzania (TRL) Kufanya kazi kwa ubunifu,
uadilifu na uwazi ili kufufua hadhi ya Shirika hilo ambalo ni muhimu
kwa uchumi wa nchi hii.
Alisema
takribani asilimia 96 ya mizigo inayoshushwa katika Bandari ya Dar es
salaam husafirishwa kwa njia ya barabara hivyo ni jukumu la TRL
kuhakikisha inapata mizigo ya kutosha ya kusafirisha ili kupunguza
mizigo hiyo kusafirishwa na barabara lakini kufufua uchumi wa TRL na
taifa kwa ujumla.
“Fanyeni
kazi kwa bidii, uwazi na kwa kushirikiana ili kujenga Shirika la Reli
la kisasa lenye uwezo wa kujitegemea acheni vitendo vya hujuma na migomo
vinavyoweza kudhoofisha shirika hili”, alisisitiza Prof. Mbarawa.
Naye Naibu Waziri wa Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani alikemea vitendo vya
wizi wa mafuta na kuhujumu Reli vinavyofanywa na watumishi wasio
waaminifu na kuwataka kuwa wazalendo kwa nchi yao ili kuchochea kasi ya
maendeleo.
Profesa
Mbarawa alikuwa kwenye ziara ya kukagua utendaji wa taasisi zilizo
chini ya Wizara Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano ambapo alipata
fursa ya kukagua ujenzi wa mizani ya kisasa ya Mikese na kituo cha
mtandao wa mawasiliano ya simu vijijini ya Halotel unaosambazwa katika
taasisi za Serikali ikiwemo Hospitali, Polisi, Mahakama na Shule hapa
nchini.