Ripoti ya Twaweza: Asilimia 50 ya Wanafunzi S/Msingi nchini hawajui kusoma kwa Kiswahili
Ripoti hiyo iliyozinduliwa Dar es Salaam leo Julai 29, 2015, inaonyesha kwamba uwezo huo umebaki chini na kwa kiasi kikubwa haujabadilika hali ya uwezo wa kusoma ingawa uwezo wao wa hesabu umeonyesha kuboreka kidogo lakini watoto wengi wanakwenda shuleni lakini hawasomi kwa muda mrefu.
Akitoa matokea ya ripoti hiyo, Meneja wa Twaweza, Zaidi Magalla, (FikraPevu imepata nakala), ameeleza kuwa matokeo ya ripoti hiyo imebaini kwamba mtoto mmoja kati ya wanne wa darasa la tatu wanaweza kusoma hadithi ya darasa la pili kwa Kiswahili hadi wanapofikia darasa la tano ndipo wengi wa wanafunzi wanaweza kusoma kwa ngazi ya darasa la pili.
Sehemu ya ripoti hiyo inasema watoto wanne kati ya kumi wa darasa la tatu wamebainika kuwa wanaweza kuzidisha hesabu ngazi ya darasa la pili, wakati viwango vya ufaulu wa somo la hisabati katika utafiti wa mwaka 2012 vilikuwa juu zaidi kuliko miaka iliyopita.
“Kwa mfano 44% ya wanafunzi wa darasa la tatu walifaulu mtihani wa kuhesabu ikilinganishwa na asilimia 37% mwaka 2011. Hata hivyo, tathmini ya mwak 2012 haikuhusisah Wilaya Saba na matokeo haya yanahitaji kuthibitishwa zaidi katika miaka ijayo” alieleza sehemu ya ripoti hiyo.
Amesema kuwa umahiri katika kusoma na kufahamu hadithi kwa kiingereza bado uko chini katika maeneo mbalimbali nchini, kwani kwa mtoto mmoja kati ya kumi wa darasa la tatu imebainika kuwa wana uwezo wa kusoma hadithi ngazi ya darasa la pili kwa kiingereza huku tathmini ya Uwezo ya mwaka 2012 ikithibitisha kuwa viwango vya uelewa wa kiingereza katika kiwango cha msingi ni chini kwa kiasi kikubwa kuliko viwango vya uelewa kwa Kiswahili katika madarasa yote.
Taswira ya ripoti ya Taasisi hiyo
Takwimu za 2012 zilithibitisha wazi kati ya mikoa, Wilaya, mijini na
vijijini katika matokeo ya watoto kujifunza imeonyesha kuwa watoto
wanaoishi katika wilaya za mijini wamefanya vizuri kuliko watoto
wanaoishi katika wilaya za vijijini.
Awali Mkurugenzi wa Twaweza, Aidan Eyakuze, alieleza kwamba tatizo la mahudhurio shule mbalimbali nchini ni tatizo kubwa kutokana na kasumba ya walimu kufika shuleni na kujaza daftari la mahudhurio bila kufundisha wanafunzi na kwamba tatizo hilo limepelekea asilimia 50% ya watoto kutojua kusoma kwa lugha ya kiswahili na asilimia 80% hawajui kusoma Kiingereza.
Afisa Programu wa Twaweza, Richard Temu, alieleza kuwa kumekuwepo na matokeo mabaya ya ufaulu kwa wanafunzi kwa familia maskini kabisa, familia zenye umaskini wa kati na matajiri na kwamba ili watoto hao waweze kupata elimu yenye tija ni wakati wa serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kuboresha mfumo wa elimu hususani katika sera mpya ya elimu iliyozinduliwa hivi karibuni Jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa Haki Elimu, John Kalage, akichangia katika ripoti hiyo amesema watoto wengi nchini hawasomi kutokana na sababu mbalimbali, ikiwa ni pamoja na motisha wa walimu wanaoupata kutoka serikali.
Amesema kwamba watoto wengi wanahudhuria shuleni lakini hawasomi, na wala hawawezeshwi na walimu ili kujua kusoma na kuandika. Amesema ili kuondoa tatizo hilo lazima rasilimali zote zifike kwa muda na kuunganisha nguvu kwa ngazi zote ili kutatua tatizo hilo.
Baadhi ya viongozi wa Twaweza wakishirikiana na wadau mbalimbali waliowezesha kupatikana kwa ripoti hiyo.
Mathalani bendera ya taifa iliyopo kila mahali nchini hususani katika
mazingira ya shule, watoto wengi hawaelewi maana ya rangi za bendera
ambapo matokeo yanaonyesha kuwa asilimia 69% ya watoto wenye umri wa
miaka 7-16 hawawezi kueleza maana ya rangi tatu za bendera na kwamba
tofauti ipo kwa wale waliojiunga na shule na walio nje ya shule au kwa
wale wa maeneo ya vijijini na mijini.