Alhamisi, 22 Januari 2015

DKT. MWANJELWA, NMB WAMWAGA MADAWATI MASHULENI



 Kulia ni Katibu wa Mbunge, Dkt. Mary Mwajelwa, Tumaini Mwakatika, akimkabidhi dawati moja jana, kama ishara yakukabidhi dawati 42, mkuu wa shule ya Msingi, Ivumwe, kata ya Mwakibete, Jijini Mbeya, Mwalimu Nectora Mbwanji.
 Madawati yaliyokabidhiwa jana katika shule ya Msingi Ivumwe, Jijini Mbeya jana.
 Baadhi ya viongozi wa Benki ya NMB, walimu, Katibu wa Mbunge wa viti maalum mkoa wa Mbeya, Dkt.Mary Mwanjelwa na wanafunzi wa darasa la saba wa shule ya Msingi Ivumwe Jijini Mbeya, wakiwa katika picha ya pamoja baada ya hafla ya kukabidhi madawati.
 Madawati yaliyoharibika katika shule ya Msingi, Ivumwe, Jijini Mbeya.
 Moja ya boma la darasa ambalo linahitaji kumaliziwa ujenzi kwa ajili ya madarasa ya shule ya Msingi Ivumwe Jijini Mbeya, ili kupunguza mrundikano wa wanafunzi madarasani, ambapo kwa sasa wanafunzi wa darasa la saba wanasoma katika chumba kimoja wakiwa zaidi ya 100.
 Katibu wa Mbunge, Dkt. Mary Mwanjelwa, Tumaini Mwakatika(kulia), akikabidhi magawati 42, katika shule ya Msingi, Itiji Jjini Mbeya, kwa niaba ya Mbunge na Benki ya NMB.

MBUNGE wa viti maalum mkoa wa Mbeya, Dkt. Mary Mwanjelwa(CCM), amekabidhi madawati 84 katika shule za Msingi Itiji na Ivumwe zilizopo katika Halmashauri ya Jiji la Mbeya.

Akikabidhi madawati hayo yenye thamani ya Shilingi Milioni tano jana, Katibu wa Mbunge huyo, Tumaini Mwakatika, alisema kuwa, Mbunge alipokea mahitaji ya shule hizo kutoka kwa viongozi wa maeneo ya shule, ndipo akaamua kuomba msaada huo kwa wahisani ambao ni Benki ya NMB.

Alisema, maombi ya viongozi hao yalikuwa mengi, lakini akaona ni vema akaanza na suala la madawati linalogusa moja kwa moja taaluma na Afya za wanafunzi.

“Mbunge anawashukuru NMB, lakini pia ametoa wito wa kutunza vema madawati hayo, na anawaombeni wanafunzi kuzingata masomo na kwamba wazazi waache ushabiki wa kisiasa na vyama katika mambo ya maendeleo”Alisema Tumaini katika hotuba zake wakati wa kukabidhi madawati 42 shule ya Msingi Itiji na 42 shule ya Msingi Ivumwe Jijini Mbeya.

Meneja biashara za Serikali kanda ya Nyanda za juu kusini wa benki hiyo ya NMB, Focus Lubende, alisema kuwa, benki yake iliamua kutoa msaada huo baada ya kupata maombi kutoka kwa Mbunge Dkt. Mwanjelwa.

“Baada ya kupata maombi, tukafanyia kazi. Na katika mkoa wa Mbeya ni shule mbli tu zimebahatika kupata msaada huu wa madawati ambazo ni Ivumwe na Itiji”alisema Lubende.

Mwalimu mkuu wa shule ya Msingi Itiji, Thomas Mwilenga, alishukuru kwa msaada huo wa madawati 42 kwa shule yake, huku akiahidi kuitisha mkutano wa wazazi na kuwaonesha madawati hayo yaliyotolewa na Mbunge kwa hisani ya benki ya NMB.

Diwani wa viti maalum kata ya Mwakibete, Agness Mangasila, alisema amefarijika baada ya kupata msaada wa madawati 42 kwa ajili ya shule ya Ivumwe, maana yeye ndiye alipeleka maombi hayo kwa Mbunge Dkt. Mwanjelwa, baada ya kupata changamoto kutoka kwa uongozi wa shule hiyo.

Mkuu wa shule hiyo ya Ivumwe, Nestora Mbwanji, mbali na kushukuru, alisema shule yake inakabiliwa na upungufu wa vyumba vya madarasa 18 ambapo kwa sasa vipo 10, matundu ya vyoo vya wanafunzi wavulana 18, wasichana matundu 24 na wanafunzi awali matundu manne.

“Tunashukuru wa madawati haya maana tulikuwa na upungufu wa madawati 72 na sasa tumepata 42, tuna upungufu wa vyumba vya madarasa na sasa kuna maboma matano yanayotakiwa kumaliziwa kwasababu mlundikano wa wanafunzi darasani unaathiri taaluma ingawa tumeendelea kushika nafasi za shule kumi bora katika mitihani ya Taifa” alisema Mwalimu Mbwanji.

Alipoulizwa idadi ya wanafunzi wa darasa la saba waliopo kwa mwaka huu na kulundikana katika chumba kimoja cha darasa, alisema kuwa wanafunzi wanaotarajia kuhitimu mwaka huu na wapo katika chumba kimoja ni 143.
 
Dkt. Mwanjelwa alisema huo ni utekelezaji wa ilani ya cham chake na  ni wajibu kwa kiongozi kutafuta wafadhili kwa kuandika michanganuo ya miradi ya maendeleo kwa wananchi.

Mwenyekiti wa kamati ya shule ya Ivumwe, Zawadi Ndassoni, alisema tangu kuanzishwa kwa shule hiyo mwaka 1976, madawati hayo ndiyo msaada mkubwa kuwahi kutolewa shuleni hapo, ambapo alibainisha kuwa, Mbunge huyo ameandika historia katika shule hiyo.

NAIBU WAZIRI WA KILIMO MHE MWANJELWA AMUAGIZA MRAJIS KUFANYA UCHUNGUZI SACCOS YA MADIBIRA-MBARALI NDANI YA SIKU 14

Naibu Waziri wa Wizara ya Kilimo, Mhe Mary Mwanjelwa akisisitiza jambo wakati akizungumza na Viongozi mbalimbali wa Mkoa na kamati ya uli...